Katika hali inayoonyesha kuwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli,
anautamani urais, amesema anaweza kutangaza nia hiyo kama atakidhi
masharti yatakayowekwa kwenye Katiba mpya.
Alisema iwapo Katiba ijayo itakuja na sifa ambazo atakidhi vigezo kuna
uwezekano mkubwa wa kuwania nafasi hiyo na kwamba iwapo atapungukiwa
sifa zinazohitajika kwa mujibu wa Katiba hataingia kwenye kinyang’anyiro
hicho.
Dk. Magufuli ambaye pia ni Mbunge wa Chato alitoa kauli hiyo wakati
akizungumza na wazee wa wilaya hiyo kwenye ukumbi wa ‘Mshikamano
Saccos’, muda mfupi baada ya mzee Paschal Nyambibo (87) kumsihi agombee
nafasi hiyo mwaka 2015 kutokana na sifa zake za uchapakazi ndani ya
serikali.
Nyambibo alisema kutokana na uwajibikaji mzuri aliouonyesha Dk. Magufuli
tangu mwaka 2000 akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi na katika wizara
mbalimbali, Watanzania wamekuwa na imani kubwa na uwajibikaji wake na
kwamba anastahili kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
ifikapo mwaka 2015.
Licha ya kauli hiyo kusababisha minong’ono mingi kwa wazee waliohudhuria
kikao hicho, Dk. Magufuli alionekana kutuliza hali hiyo kwa kusema
isubiriwe Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano iwapo itakuwa na masharti
ambayo yatamfanya kujitathimini iwapo ana sifa za kugombea au
vinginevyo.
Hata hivyo, Dk. Magufuli hakusita kuonyesha hisia zake za kukerwa na
baadhi ya wananchi wanaobeza maendeleo aliyotekeleza katika jimbo lake
tangu alipochaguliwa kuwa Mbunge.
Alimshutumu hadharani aliyekuwa Katibu wa CCM wilaya ya Chato kabla ya
kuhamishiwa wilayani Mbogwe, Gervas Stephano, kuwa hana shukrani.
Dk. Magufuli alimwelezea katibu huyo kuwa hana fadhila kutokana na mambo
mengi aliyomtendea tangu akiwa katibu wa ofisi yake ya jimbo ambapo
alimsaidia kupanda ngazi na kuwa Katibu wa CCM wilaya Chato, Kwimba,
Kasulu, Kilosa na kurejea tena Chato kabla ya kuhamishiwa wilaya ya
Mbogwe mkoani Geita kuendelea na wadhifa huo.
“Tatizo lenu watu wa Chato hamna shukrani…mambo mengi nimefanya hapa
Chato, lakini yote mnaona ziro…hata niliowasaidia kama Gervas naye sasa
hivi ananiponda…lakini nawashukuru sana wazee wangu kwa kunikumbusha
niliyoyafanya kwenye jimbo letu kupitia risala yenu nzuri,” alisema Dk.
Magufuli.
“Kutokana na hali hiyo ninawazawadia Sh. 1,000,000 mfanye sherehe ya
kujipongeza kwa kuwa natambua mmejitesa sana mpaka kufanikisha kikao
hiki cha leo…na kwa kuwa hamna mradi wowote wa kuwaingizia kipato kama
wazee, ninaahidi kuwapa Sh. 3,000,000 kutoka mfuko wa jimbo, ili
muanzishe walau saccos ya kukopeshana,” alisema.
Baadhi ya viongozi na wananchi wamekuwa wakilitaja mara kwa mara jina la
Waziri Magufuli miongoni mwa watu wanaodhaniwa kutaka kugombea nafasi
ya urais wa Tanzania mwaka 2015, ingawa mwenyewe amekuwa akikanusha
uvumi huo.
Mbali na Dk. Magufuli, wengine ndani ya CCM wanaotajwa ni pamoja na
aliyekuwa Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa;
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye anajiita
mtaji wa urais; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa Ushirikiano wa Kimataifa –CCM, Dk. Asha-Rose
Migiro na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Mambo ya Nje, Bernard
Membe, ambaye alipata kusema anasubiri kuiteshwa na Mungu kuwania
nafasi hiyo.
Nipashe:
No comments:
Post a Comment