GHANA NA HOFU YA WACHEZAJI WAKE KUCHEZA SOKA LA KULIPWA TP MAZEMBE
Sio mara nyingi unaweza ukasikia mashabiki wa nchi fulani wakiwa na wasiwasi juu ya wachezaji wa taifa lao kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ili kuendeleza vipaji vyao.
Walinzi Daniel Nii Adjei, Yaw Frimpong, Richard Kissi Boateng kiungo Gladson Awako na mshambuliaji Solomon Asante wote waliondoka Ghana kwa muda mmoja mwanzoni mwa msimu.
"Watu wanaweza wakaona kama ni dalili ya kushuka kwa ligi ya Ghana kiasi kwamba wachezaji wakubwa wa Ghana wanaenda kucheza soka Congo," alisema mwandishi wa BBC Michael Oti Adjei.
Inaweza ikawa ni hofu isiyo sahihi ya mashabiki wa Ghana, lakini wanaweza wakawa na pointi nzuri kwenye hili kwamba klabu nyingine za Afrika zinawapita kwa umbali mrefu timu za Ghana kama Accra Hearts of Oak na Asante Kotoko.
"Watu wanapishana kwenye maoni.
Wengine wanadhani wachezaji wale wapo Congo kwa sababu za michezo,
wengine wanadhani sababu ya fedha," aliongeza Oti Adjei.
Kisoka, Ghana na Congo zipo mbalimbali - wanatenganishwa kwa pengo la nafasi 63 kwa viwango vya FIFA vya mwezi wa nne. Wakati Black Stars wameshiriki mara mbili fainali za kombe la dunia tangu mwaka 2006, huku wachezaji wake wengi wakicheza katika ligi kubwa barani ulaya, Congo imeweza kushiriki fainali hizo mara moja tu, mwaka 1974 wakati ikiitwa Zaire.
Wakati huo wakaweka rekodi ya kipigo kikubwa zaidi kwenye fainali hizo kwa kufungwa 9-0 na Yugoslavia.
Lakini mabingwa wa mara nne wa kombe la mabingwa wa Afrika TP Mazembe, imekuwa ndio timu ya kwanza ya Afrika kucheza fainali ya klabu bingwa ya dunia mnamo mwaka 2010, na sasa wapo kwenye hali nzuri kisoka na kifedha kuliko vilabu vingi vya Ghana.
Ikiwa ipo kwenye eneo lilo na utajiri wa madini la Katanga, klabu inamiliki uwanja, ndege mbili, gym na kliniki.
Wapo chini ya uongozi wa tajiri mkubwa, Moise Katumbi, ambaye pia ni Gavana wa eneo hilo.
Wachezaji wa Ghana wanajua uhamisho wao kwenda Congo umegawanya maoni ya mashabiki lakini wanapenda maisha yao ya soka ndani ya Congo.
Beki Richard Kissi Boateng aliiambia BBC : "Kujiunga TP Mazembe ilikuwa ni hatua nzuri. Kama unavyoona wana ushawishi mkubwa katika soka la Afrika.
"Kwenye maisha inabidi uendele mbele. Tumejiunga nao ili tuweze kutengeneza majina katika soka la Afrika. Kila kitu ni kikubwa hapa, wachezaji, mashabiki na hata miundo mbinu ya klabu ni mizuri kufananisha na ya vilabu vingine na nafikiri soka la Congo limeendelea sasa kuliko la Ghana."
Mazembe wana wachezaji kutoka Zambia, Malawi, Tanzania, Ivory Coast, Uganda, Senegal na katika miaka miwili iliyopita klabu imeweza kuajiri wachezaji kutoka Zimbabwe, Brazil na Cameroon.
"Sipo hapa kwa sababu ya fedha. Katika maisha, ikiwa hautoweza kupambana na changamoto, huwezi kujipima mwenye dhidi ya kitu chochote," aliendelea Boateng.
Na akakiri kwamba rekodi ya Mazembe ya kuiwakilisha mara mbili Afrika katika kombe la dunia ngazi ya vilau iliupa ushawishi uamuzi wake wa kujiunga nao.
"Wachezaji wengine wakubwa tu barani ulaya hawajawahi kucheza kwenye michuano hiyo," alisisitiza.
No comments:
Post a Comment