CCM WAMVAA MKUU WA MKOA WA ARUSHA.....WANADAI AMEMUONGEZEA UMAARUFU GODBLESS LEMA
VIGOGO
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwemo wabunge, wamemjia juu Mkuu wa
Mkoa (RC) wa Arusha, Magessa Mulongo kwa jinsi alivyoshughulikia kesi ya
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA).
Wabunge hao waliliambia gazeti hili mjini Dodoma kuwa kesi ya uchochezi iliyofunguliwa na serikali dhidi ya Lema kwa shinikizo la mkuu huyo, itaiathiri kwa kiasi kikubwa CCM.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alisema kuwa amefuatilia kwa makini chanzo cha kesi ya Lema na hatimaye kukamatwa na polisi mithili ya gaidi, na kubaini kuwa hulka
za utendaji kazi wa baadhi ya viongozi wa serikali zinawapa sifa na umaarufu zaidi CHADEMA.
“Mimi
sitaki kuingilia kesi, lakini ukiangalia kuanzia ile inayoitwa video ya
vurugu za Chuo cha Uhasibu Arusha na jinsi Mkuu wa Mkoa alivyofika eneo
la tukio na kuondoka, utabaini udhaifu mkubwa wa kiongozi huyo ambao
leo unamfanya Lema aonekane shujaa.
“Leo
tunaingia kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani pale Arusha, tunaweza
tukashinda, lakini tutafanya kazi ya ziada kwa sababu tu ya udhaifu wa
Mkuu wa Mkoa wa Arusha,” alisema Lugola.
Mbunge
mwingine ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema alichokifanya
Mulongo ni sehemu ya tatizo kubwa la viongozi wa serikali kujihusisha na
ukereketwa wa kisiasa.
“Baba
wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa kuna kiongozi, tena
hakumtaja jina, kwamba anapendwa kubebwa, alisema mwacheni abebwe.
Alisema vile kuwazuia polisi kukabiliana na watu wanaopenda kumbeba
kiongozi huyo.
“Mkuu
wa Mkoa Arusha na wengine wanaokabiliana na wapinzani kwa nguvu kubwa
bila sababu, hii inawaongezea umaarufu,” alisema mbunge huyo kutoka moja
ya majimbo ya kanda ya kati.
Mjumbe
mmoja wa Kamati Kuu (CC) ya CCM ambaye pia hakutaka kutaja jina lake,
alilaani jinsi mkuu wa mkoa huyo alivyojikoroga katika kushughulikia
mzozo wa Chuo cha Uhasibu Arusha.
“Niliposoma
ujumbe wa simu ya mkononi wa Lema ambao alidai umetoka kwa Mkuu wa
Mkoa, nilishangaa sana. Sijui kwanini amefanya vile,” alisema kigogo
huyo.
Aprili
24 mwaka huu, Mulongo aliliamuru Jeshi la Polisi mkoani Arusha
kumkamata Lema kwa madai kuwa aliwachochea wanafunzi wa chuo hicho cha
IAA kumzomea na kumrushia mawe.
Lema
alizingirwa nyumbani kwake na maofisa wa polisi kitengo cha upelelezi
na wale wa doria Ijumaa saa 5.30 usiku kisha kuchukuliwa hadi Kituo
Kikuu cha Polisi kuhojiwa na kuwekwa rumande siku tatu hadi Jumatatu
wiki hii alipofikishwa mahakamani.
Hata
hivyo, madai ya Mulongo kuwa Lema alichochea wanafuzni hao yanakinzana
na ushahidi wa video unaoonesha kuwa mbunge huyo alitumia kila aina ya
ushawishi kuwasihi wasiandamane kufuatia mwenzao Elly Kago (22) kuuawa
na watu wasiojulikana jirani na chuo.
Mapema
kabla ya kukamatwa, Lema aliitisha mkutano na waandishi wa habari
akidai kutishiwa na Mulongo kupitia ujumbe wa maandishi wa simu.
“Umeruka
kihunzi cha kwanza, nitakuonyesha kuwa mimi ni serikali, ulikojificha
nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi,’’ ulisomeka ujumbe huo
uliotumwa kupitia simu namba 0752 960276 ambayo Lema alidai ni ya
Mulungo.
Atisha waandishi
Wakati
CCM wakiendelea kumlalamikia Mulongo kwa hatua zake dhidi ya Lema,
kiongozi huyo jana aliwageukia waandishi wa habari wa Arusha akiwataka
wawe makini kipindi hiki, akidai kuwa nao wanatumika na wanasiasa.
Akihutubia katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi, alisema kuwa ikibainika wanatumika nao watafikishwa katika vyombo vya sheria.
“Mimi
nilikuwa Mkuu wa Wilaya Bagamoyo, hivi hivi wakawa hawanielewi na
ikafika wakati wakanielewa kwani kuna miongoni mwao tulitaka kuwafikisha
katika sheria, lakini tukayaacha kwa kuwa sisi ndio walezi,” alisema.
Mulongo
aliongeza kuwa vitu ambavyo vinaandikwa si kweli kabisa, na kwamba
wataendelea kufuatilia kwani baadhi ya waandishi wanashirikiana na
wanasiasa kuwachafua viongozi wa serikali.
Alisema
baadhi ya waandishi mkoani Arusha wamekuwa wakifanya kazi zao kwa
ushabiki wa kisiasa na kuandika mambo ambayo hawana uhakika nayo.
“Unapoingia katika mkakati wa kudhalilisha kiongozi wa serikali unakuwa umeiweka roho yako rehani, kuweni makini,” alisema.
Aidha
alivionya vyama vya wafanyakazi mkoani Arusha kutoruhusu kutumiwa na
watu kwa malengo ya kisiasa na pia waajiri waache kufanya kazi bila
kufuata taratibu na sheria.
TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment