AZAM KAMBINI KUJIANDAA DHIDI YA MGAMBO

Baada ya kutolewa katika kombe la
shirikisho barani Africa, klabu ya Azam fc maarufu kama “Lambalamba”
imesema kuwa sasa imerudisha akili yake katika michuano ya ligi kuu soka
Tanzania bara inayoelekea ukingoni kwa msimu huu wa 2012/2013.
Afisa habari wa klabu hiyo, Jafar Idd
Maganga amsema kuwa klabu hiyo inaingia kambini katika hosteli zao za
Chamazi Mbande, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam kujiandaa na mchezo
wa jumapili dhidi ya maafande wa jeshi la kujenga taifa kutoka mkoani
Pwani Mgambo Shooting.
“Wachezaji wote wamerudi salama baada
ya kuhuzunishwa na matokeo ya Morroco, lakini hili ndio soka, tunajua
wazi kuwa matokeo yale yaliwashangaza wengi hasa baada ya mchezaji wetu
Bocco kukosa penati dakika za lala salama, lakini soka lina mambo yake
na sasa tunajiandaa na ligi kuu”. Alisema Jafar.
Jafar alisisitiza kuwa azima yao ni
kushiriki kwa mara ya pili michuano ya kimataifa mwakani na ndio maana
wanaanza kampeni ya kuchukua nafasi ya pili msimu huu kwa kushinda mechi
zilizosalia.
Afisa habari huyo alisema licha ya
kutupwa nje na AS FAR Rabat ya Morroco lakini wamejifunza mengi kwani
wao bado ni wachanga sana katika mashindano ya kimataifa kwani ndio kwa
mara ya kwanza wameshiriki mwaka huu.
Azam fc mpaka sasa wapo nafasi ya pili
ya ligi hiyo wakijikusanyia pointi 48 huku nyuma yao wakiwemo simba
wenye pointi 42 nafasi ya tatu na leo hii wanashuka dimbani kumenyana na
Mgambo Shooting ya Mkoani Tanga katika uwanja wa taifa jijini Dar es
salaam. Chanzo: www.fullshangweblog.com
No comments:
Post a Comment