AZAM FC YATUPWA NJE SHIRIKISHO YAFUNGWA NA AS FAR - RABAT 2-1
Azam vs AS FAR Rabat
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe
Safari ya wawakilishi pekee wa
Tanzania katika michuano ya kimataifa, klabu ya Azam fc yenye makazi
yake Mbande Chamazi jijini Dar es salaam imeishia mikokoni mwa waarabu
wa Morroco, AS FAR Rabat baada ya kukubali kufungwa mabao 2-1 huku Azam
wakikosa penati dakika za lala salama za mechi iliyopigwa katika uwanja
wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat nchini Morroco.
Wana lambalamba hao wametoka kwasababu katika mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa taifa jijini Dar es salaam wiki mbili zilizopita walitoka suluhu pacha ya bila kufungana na leo hii wamefunga mabao hayo na kutoka kwa wastani wa mabao mawili kwa moja.
Endapo Azam wangetoa sare yoyote ile wangesonga mbele katika michuano hiyo kwa faida ya bao la ugenini.
Azam waliingia uwanjani kwa kujiamini na kupata bao la kuongoza katika dakika ya 6 ya mchezo kupitia kwa John Raphael Bocco “Adebayor” na dakika sita baadaye FAR Rabat wakasawazisha bao hilo.
Dakika ya 43 Azam walifungwa bao la pili na la ushindi kwa wenyeji wao na kuwaacha Watanzania wachache waliokuwepo huko wakiwa na butwaa baada ya taifa kubaki bila timu katika michuano ya kimataifa.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa wenyeji kucheza pungufu baada ya mchezaji mmoja kupewa kadi nyekundu kwa kosa la kumfanyia madhambi Brian Umony.
Kipindi cha pili kipute hicho Azam walilazimika kucheza pungufu kipindi cha pili baada ya walinzi wake David Mwantika na Waziri Omary kuoneshwa kadi nyekundu kwa nyakati tofauti.
Matumaini ya Azam kusonga mbele yaliongezeka katika dakika ya 81 baada ya kuzawadiwa penati lakini Bocco alikosa mkwaju huo na kuwaacha mashabiki wa soka Tanzania vichwa chini.
Kwa ujumla katika mchezo wa leo makosa ya mabeki wa Azam kukaba vibaya ndio chanzo cha kupoteza mchezo huo.
Pia washambulaiji wa wana lambalamba hao wakiongozwa na John Bocco na Kipre Herman Tchetche walipoteza nafasi za kufunga na wangeongeza umakini basi wangeibuka kidedea na kuendelea kuwapa raha Watanzania.
AS FAR Rabat walicheza soka la kasi licha ya kuwa pungufu, lakini walipoteza nafasi nyingi na mashambulizi ya kushitukiza yalitawala kwa timu zote.
Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Kipre Tchetche, Salum Abubakar, John Bocco, Humprey Mieno/Gaudence Mwaikimba dk79 na Brian Umony/Khamis Mcha dk70.
AS FAR Rabat; Ali Grouni, Anouar Younes/Ennajar Tarik, Younes Hammal, Younes Belakhdar, Kaddoui Youssef, Abdelrahim Achchakir, Aqqal Salaheddine/Alloudi Soufiane, Mustafa Allaoui, El Kodry Yassine, El Bakkali Medamine na El Yousfi Mostafa.
No comments:
Post a Comment