ZANZIBAR YACHAFUKA KWA KUKAMATWA KWA KIONGOZI WA UAMSHO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewataka wananchi kuendelea na shughuli 
zao kama kawaida na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimedhibiti hali
 ya  ulinzi na imeimarishwa katika maeneo yote ya Zanzibar.
 Taarifa ya Serikali iliyotolewa leo 
usiku na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud 
Mohammed imesema Zanzibar bado ni shwari na inaendelea kuwa katika hali 
ya amani na utulivu.
 
Akizungumzia tukio la vurugu zilizofanywa na wananchi wachache, Waziri 
Mohamed Aboud alisema vikundi vya vijana vinavyosadikiwa kuwa ni wafuasi
 wa Sheikh Farid Hadi walifanya vurugu hizo katika mitaa ya Darajani, 
Michenzani, Muembeladu,Magomeni,Amani wakidai Sheikh wao haonekani na 
kudhani amekamatwa na vyombo vya Dolan a kuwekwa ndani. 
Waziri Mohamed Abud alisema Serikali 
imewasiliana na vyombo vya Dola ikiwemo Polisi,Jeshi la wananchi wa 
Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa, Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi 
Zanzibar,KMKM,JKU,Chuo cha Mafunzo,Zimamoto na Valantia ambapo vyombo 
vyote hivyo vimeeleza kutoelewa chochote kuhusu Sheikh Farid. 
Waziri huyo alisema kwamba Jeshi la 
Polisi limepokea taarifa ya kutoonekana kwa Sheikh Farid  ambapo kwa 
sasa Jeshi hilo linaendelea kumtafuta na kufanya uchunguzi juu ya tukio 
hilo ili kupata ukweli wake na kuchukua hatua zinazofaa.
 
Alisema kwamba wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wake, 
wananchi wameombwa kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa vituo vya Polisi 
 au kupitia Masheha, Ofisi za Wilaya na Mikoa katika maeneo yao.
 Waziri Mohamed Aboud amesema Serikali 
inawasihi wwananchi  waache kujiingiza katika vitendo vya fujo na vurugu
 kwani kutenda hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na Serikali 
haitovumilia vitendo hivyo.
 
Katika tukio la leo mchana, vijana hao wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa 
Sheikh Farid Hadi walifanya vitendo vya vurugu ikiwemo kuchoma moto 
Maskazini za CCM,kuvunja maduka,kupora mali za watu na kuharibu 
miundombinu ya barabara na kusababisha hasara kubwa.


No comments:
Post a Comment