MAJINA YA SHULE 24 ZITAKAZITOA WANAFUNZI KUJIUNGA NA JKT MWAKA HUU
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha |
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limetaja shule 24 za sekondari ambazo zitatoa wanafunzi 5,000 waliomaliza kidato cha sita watakaojiunga na jeshi hilo.
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Raphael Mahuga alisema katika taarifa yake jana kuwa wanafunzi hao watatakiwa kujiunga na jeshi hilo ifikapo Machi 2, mwaka huu.
Shule hizo za sekondari ni Kibondo, Musoma, Kibaha, Ilboru, Bagamoyo, Jitegemee, Tabora Wavulana na Nganza.
Shule nyingine ni Mtwara Wasichana, Ihungo, Kilakala, Benjamin Mkapa, Maswa Wasichana, Dodoma, Tumain-Singida na Galanos.
Nyingine ni Ashira, Nangwa-Manyara, Iyunga, Mpanda, Lindi, Iringa Wasichana, Kawawa-Iringa na Ruhuwiko-Songea.
Taarifa hiyo ilisema maofisa wa JKT watakwenda kwenye shule hizo kuanzia Januari 9, mwaka huu kwa ajili ya kutoa utaratibu wa mafunzo na kambi ambazo watakwenda.
“Mkuu wa JKT kwa mamlaka aliyopewa kisheria ya mwaka 1964 na kufanyiwa mapitio mwaka 2002, chini ya kifungu cha sheria namba 5,” ilisema taarifa hiyo.
Iliongeza kuwa “Anawaita vijana watakaohitimu kidato cha sita mwaka 2013 kujiunga na JKT kwa mujibu wa sheria ifikapo terehe 2, Machi 2013.”
Utaratibu wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria ulisimamishwa tangu mwaka 1994.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Jeshi la Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Julai mwaka jana, Waziri wake, Shamshi Vuai Nahodha alisema kambi zilizopo za JKT zina uwezo wa kuchukua vijana 20,000 kwa wakati mmoja, lakini kutokana na ufinyu wa bajeti mwaka huu wataanza kwa majaribio na vijana 5,000.
Alisema wanafunzi 41,348 wanatarajiwa kuhitimu elimu ya kidato cha sita katika mwaka 2013 na kwamba vilikuwa vikiandaliwa vigezo ili kuwapata vijana 5,000 ili kujiunga na JKT.
Kwa mujibu wa jarida la JKT, mafunzo hayo yatakuwa ya miezi sita katika Kambi za JKT Bulombora na Kanembwa mkoani Kigoma.
Nyingine ni Mlale (Ruvuma), Mafinga (Iringa), Msange (Tabora) na Oljoro(Arusha).
No comments:
Post a Comment