SERIKALI YALIFUFUA SHIRIKA LA RELI
SERIKALI
imetangaza hatua kubwa na kabambe za kufufua usafiri wa abiria na
mizigo, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mabehewa na injini za treni,
katika hatua kubwa za aina yake kuchukuliwa na Serikali kwa muda mrefu
katika kurekebisha usafiri wa treni nchini.
Waziri wa
Uchukuzi, Mheshimiwa Harrison George Mwakyembe ametangaza hatua hizo
leo, Alhamisi, Januari 10, 2013, wakati alipokuwa anamkaribisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuweka
jiwe la msingi kwenye ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Tabora
ikiwa ni tukio la mwisho la ziara yenye mafanikio makubwa ya siku tano
ya Rais Kikwete katika Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa
Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete na mamia kwa mamia ya wananchi
waliohudhuria sherehe ya uwekaji jiwe hilo la msingi kwenye Uwanja huo
kuwa Wizara yake imeanza kubadilisha reli nyepesi, iliyochakaa na yenye
uzito mdogo kwa Reli ya Kati.
Amesema
kuwa kwa kupitia mashirika yake ya RAHCO na Shirika la Reli Tanzania
(TRL) Serikali itafanya marekebisho hayo makubwa njia mzima ya Reli ya
kati na kuwa mafundi wa mashirika hayo tayari wamefika Mkoa wa Morogoro.
Waziri
Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa Serikali kupitia Wizara yake na
mashirika yake hayo, imeagiza mabehewa mapya ya mizigo 274, imeagiza
mabehewa mapya ya abiria 22, imeagiza mabehewa mapya ya kubebea kokoto
25 na pia imeagiza mabehewa ya breki (brake vans) 34 na tayari malipo ya
awali yamefanyika.
Katika
namna inayothibitisha dhamira ya Serikali kurekebisha hali ya usafiri wa
reli nchini, Mheshimiwa Mwakyembe pia amewaambia wananchi kuwa Wizara
yake pia imeagiza crane mpya na kubwa ya kubebea mizigo yenye uzito
unaofikia kilo 100.
Kuhusu injini za treni, Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa zabuni kwa ajili ya kutengeneza upya (re-manufacturing) injini nane za treni imetolewa ili utengenezaji huo ufanyike, iwe ni ndani ama nje ya nchi.
Pia Waziri
amesema kuwa oda imetolewa kwa ajili ya utengenezaji wa injini mpya 13
za treni ambazo malipo yake yatafanyika katika mwaka ujao wa fedha hata
kama utengenezaji wa injini hizo utaanza.
Aidha,
Waziri amesema kuwa Wizara kupitia mashirika yake hayo mawili imeagiza
spea za kutosha kuweza kufanya ukarabati mkubwa wa injini tano kwenye
karakana zilizoko hapa nchini.
“Mheshimiwa
Rais, kwa hesabu nyepesi tu ni kwamba katika kipindi kifupi tutaweza
kuwa na injini kiasi cha 26 ambazo zitarudisha uhai wa usafiri wetu wa
reli kwa kiasi kikubwa sana,” Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
10 Januari, 2013
No comments:
Post a Comment