LANCE AKIRI KUTUMIA MADAWA YA KULEVYA
LANCE Armstrong hatimaye amekiri kutumia dawa zinazokatazwa michezoni katika sehemu kubwa ya enzi zake za mafanikio na wakati akishinda mataji yote saba ya mbio za baiskeli ya Tour de France.
Katika mahojiano maalum yaliyorushwa na OWN channel ya Oprah Winfrey alfajiri ya leo, mwendesha baiskeli huyo mwenye umri wa miaka 41 na ambaye amenusurika kwa ugonjwa wa saratani, amekiri kutumia dawa za kuongeza nguvu zikiwemo testosterone, za kusaidia kukuza homoni, na EPO Erythropoietin — inayozalisha seli nyekundu za damu ambazo huongeza oxygen kwenye misuli na stamina kwa ujumla.
Mwendesha baiskeli huyo alikiri mfululizo wa maswali kwa kujibu ‘ndiyo au hapana’ na alijibu "ndiyo" kwa maswali yote yakiwamo:
"Umewahi kutumia dawa zinazokatazwa ili kukuongeza nguvu katika kiwango chako mashindanano?"
"Miongoni mwa dawa hizo imo inayokatazwa ya EPO?"
"Umewahi kutumia dawa zozote zinazokatazwa kama testosterone, cortisone, au za kukuza homoni?'
"Katika ushindi wa mataji yako yote saba ya Tour de France ulitumia dawa zinazokatazwa?"
Na zaidi, Armstrong amekiri kwamba “kwa maoni yangu” isingewezekana kibinadamu kwake kushinda mataji yote saba ya mbio za Tour de France bila ya kutumia dawa za kuingoza nguvu.
"Mapema wakati naibukia katika mbio hizi, kulikuwa na dawa na cortisone, na kisha kizazi cha EPO kikaanza. Kwangu mimi, katikati ya miaka ya 90,” alikiri.
Alipoulizwa kwanini hatimaye amekiri kutumia dawa hizo baada ya kuidanganya jamii na kukanusha kutumia dawa hizo kwa miaka mingi mfululizo, Armstrong alisema, "Sijui kama nina jibu zuri. Naweza kuanza kujibu kwa kusema hii imeshachelewa sana. Imeshachelewa kwa watu wengi. Na hilo ni kosa langu. Naliona suala hili kama ni udanganyifu mkubwa ambao niliurudia mara nyingi mno."
Armstrong amekiri kwamba amejikuta amejifungafunga kwenye mtandao wa uongo.
"Najua ukweli. Ukweli haukutoka. Ukweli si ule niliokuwa nikiusema. Habari hii ilikuwa ni ya ukweli kabisa kwa miaka mingi mno," alisema.
"Unapambana na ugonjwa, unashinda Tour de France mara saba, unakuwa na ndoa yenye furaha, unakuwa na watoto. Namaanisha stori nzuri, haikuwa ya kweli."
Akibeba lawama zote za mahala alipo leo, Armstrong alisema uongo wake uligeuka sumu.
"Makosa yote na lawama zote zinaniangukia mimi. Lakini nyuma ya picha hiyo na nyuma ya stori kulikuwa na jambo linaendelea. Iwe ni mashabiki ama ama vyombo vya habari, ila lilikuwa linaendelea, na nimepoteza kila kitu katika hilo,” alisema.
"Nilikuwa najua kudhibiti kila kitu katika maisha. Nilikuwa nadhibiti kila kinachotokea maishani mwangu… Hivi sasa stori ni mbaya na ni sumu, na mengi ni kweli."
Armstrong alikuwa muwazi kama ilivyotabiriwa.
"Si mimi niliyeanzisha utamaduni, lakini sikujaribu kuuzuia. Na hilo ni kosa langu. Na hicho ndicho ninachoombea radhi,” Armstrong alisema, akijaribu kuokoa sehemu ya heshima yake.
"Na sasa mchezo unaadhbiwa kwa makosa hayo. Na samahani sana kwa hilo."
Alipoulizwa kuhusu tuhuma kwamba yeye na timu ya taifa ya baiskeli ya Marekani zimetoa moja ya kashfa kubwa zaidi za kutumia dawa katika mchezo huo, Armstong alikuwa makini kutotaja majina wala kutuhumu wengine.
"Sitaki kumtuhumu yeyote mwingine, sitaki kumzungumzia mtu mwingine yetote," alisema.
"Nimefanya maamuzi yangu. Ni makosa yangu. Na nimekaa hapa leo kusema kwamba samahani kwa hilo."
Sehemu ya pili ya mahojiano ya Armstrong yatarushwa alfajiri ya kesho kwenye OWN.
No comments:
Post a Comment