TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, January 8, 2013

ADC YATISHIA KUANIKA UOVU WA MAALIM SEIF




















CHAMA cha Aliance For Democratic (ADC) kimemwonya Katibu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad kwamba iwapo ataendelea kukishambulia majukwaani, kitaanika maovu yake yote aliyoyafanya ndani ya chama chake na Watanzania kwa ujumla.
 Kimeeleza kushangazwa kwake na kitendo cha Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kutumia majukwaa kuwashambulia viongozi wa ADC badala ya kueleza sera za CUF na mustakabali wa matatizo yanayowakabili wananchi.

Onyo hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa Taifa wa ADC, Said Miraji alipohutubia wakazi wa Tanga kwenye mkutano wa hadhara viwanja vya Tangamano, mjini hapa.


Kwa mujibu wa miraji, miongoni mwa kashfa mbaya za Malim Seif ni kubadilisha makubaliano ya muundo wa Serikali ya Umoja Zanzibar ambayo yalitiwa saini na Hamad Rashid kwa upande wa CUF na Kingunge Ngombare- Mwiru kwa CCM.


Alidai kuwa makubaliano hayo yalikuwa yakieleza mgawanyo wa madaraka uanzie ngazi ya taifa hadi shehia.


“Badala yake, ameweka mawaziri watano tu kupitia CUF, je hiyo ni Serikali ya Umoja kweli au kuwageuka wanachama wake kwa kukubali kufunga ndoa na CCM,” alisema Miraji.


Mwenyekiti huyo aliambatana na Mlezi wa ADC Kanda ya Kaskazini, Doyo Hassan Doyo, Mlezi wa Kanda ya Pemba, Shoka Khamis Juma na Masaga Masaga ambaye ni Kamishna wa Kanda ya Pwani.


Miraji alisema ni jambo la kushangaza kuona Maalim Seif kusimama majukwaani kukisakama chama kichanga kama hicho, badala ya kutumia nafasi yake na uzoefu kuviunganisha vyama vya upinzani.


Alisema sera ya ADC siyo kukisakama chama chochote cha upinzani ikiwamo CUF, bali ni kuhakikisha vinashirikiana kikamilifu kukiondoa madarakani CCM.


Kuhusu Katiba ya ADC, Miraji alisema ni chama pekee chenye katiba nzuri tofauti na vyama vingine vyote, kwani inatambua uwapo wa Mwenyezi Mungu na imeweka ukomo wa muda wa uongozi kuwa vipindi viwili.
Alisema katiba yao inatambua na kuweka mbele maslahi ya walemavu, inaelezea itakapopata ridhaa ya kuongoza nchi mwanaume aliyemuoa mwanamke mlemavu atasaidiwa na serikali.


Ziara ya Mwenyekiti wa ADC imefanyika ikiwa ni wiki moja tangu Maalim Seif afanye ziara mkoani hapa.
Katika sehemu ya hotuba zake alizotoa, Maalim Seif alisema ADC hakina ubavu wa kuisambaratisha CUF.


MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment