Watanzania waingia, waishi China kinyemela
Balozi wa Tanzania nchini China, Abdulrahman Shimbo.
WATANZANIA
wengi wametajwa kuingia na kuishi nchini China kinyemela na kusababisha
wanapopata matatizo yanayohitaji msaada wa serikali kushindikana
kupewa, kwa kuwa hawamo katika utaratibu wa Diaspora.
Balozi wa
Tanzania nchini China, Abdulrahman Shimbo alisema lipo tatizo kubwa
kutokana na Watanzania wengi kuingia kinyemela kuishi, wakifanya
biashara zisizo na vibali na wengi wao ni mama lishe na wafanyabiashara
ndogo.
Aidha,
amehadharisha juu ya Watanzania kujikuta wakisoma kwenye vyuo visivyo na
ubora nchini hapa kwa kutaka wanaosoma vyuo vikuu mbalimbali wasaidie
kutoa taarifa muhimu.
Shimbo
alisema hayo jana alipozungumza na viongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa
Tanzania Beijing (TZ-SUB) katika kikao cha makabidhiano ya uongozi mpya
na utoaji vyeti kwa Tume ya Uchaguzi ya Jumuiya hiyo.
Kikao hicho kilifanyika ubalozini na uchaguzi ulifanyika Aprili 5, mwaka huu ubalozini pia.
Akizungumzia
Watanzania wanaoingia kinyemela China, Shimbo alisema, “Wanaishi hapa,
hawakamatwi ingawa hawana nyaraka muhimu, kwa kuwa wengi wao wanasaidiwa
na Wachina wenyewe wasio waadilifu. “Wengi ni mama lishe, wakipata
shida sasa wanaanza kuitafuta serikali, unaanzia wapi kumsaidia mtu wa
aina hii, ni shida na suala la vibali kwa wenzetu hapa wapo makini kweli
kweli.”
Alitaja
miji yenye tatizo hilo kwa kiwango kikubwa ni Guangzhou na Hong Kong.
Aliwataka Watanzania kujiandikisha ubalozini wanapofika nchini hapa na
pia kuhakikisha wana vibali muhimu vya kuwawezesha kuishi ugenini.
Kuhusu
masuala ya elimu, Balozi aliwataka wanafunzi Watanzania wanaosoma katika
vyuo vikuu mbalimbali nchini hapa, kusaidia taasisi za elimu na wizara
kutoa taarifa muhimu kuhusu vyuo nchini hapa kusaidia kupunguza wimbi la
watu wanaotumia vibaya nafasi hiyo kuwapotosha watu na kujikuta
wanasoma katika vyuo visivyo na ubora.
“Wasaidieni
nyumbani kujua vyuo bora, kuna watu wanakuja hapa wanasoma miaka minne
lugha, hawana hati wala maendeleo yao hayajulikani. “Wengine wanaishi
maisha yasiyoeleweka, hujui kama ni wanafunzi ama la, hii ni hatari kwao
na mustakabali wa elimu kwa taifa letu, nyie mmekuwa hapa mnaijua nchi
hii vizuri, wasaidieni tafadhali,” alisisitiza Balozi Shimbo. CHANZO: BBC (Muro)
No comments:
Post a Comment