African Sports yakwapua beki wa Simba kujipa makali
AFRICAN
Sports iliyopanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, imeanza
usajili kwa kumnasa beki wa zamani wa Simba, Hassan Khatib na winga wa
Kurugenzi ya Daraja la Kwanza, Jafar Kibaya.
Akizungumza
na Mwanaspoti, Meneja wa timu hiyo, Abdulhalim Hemed, alisema wapo
kwenye hatua nzuri ya mazungumzo na wachezaji hao ambao wana sifa za
mahitaji ya timu yao.
"Hao ni
wachezaji kati ya watano ambao tuna uhakika wa kumalizana nao, kwani
wengine tunaogopa kuwaweka wazi tunahofia hujuma za timu zenye fedha zao
kwani wakisikia tu tunawasajili watataka wawasajili kwenye timu zao,"
alisema.(P.T)
Baada ya
Khatibu kutemwa Simba , alijiunga na Friends Rangers ya Ligi Daraja la
Kwanza , iliyopo chini ya katibu Herry Mzozo, anayeaminika kuibua
wachezaji wengi wanaokipiga Ligi Kuu Bara, akiwemo Salum Abubakar 'Sure
Boy' wa Azam FC.
Mbali na
hilo alisema hawana mpango wa kuwasajili wachezaji wa Simba, Yanga na
Azam FC kwa sababu hawataki ugomvi na timu hizo zenye sifa za kutumia
fedha nyingi katika usajili isipokuwa wanaangazia macho yao katika timu
ya Mtibwa Sugar.
"Hatuna
haja na wachezaji wa Simba, Yanga na Azam FC, kwani timu yetu haina
uwezo wa kushindana nao kifedha ili tutasajili wasio na majina makubwa,
lakini wenye uchu wa mafanikio yao pamoja na timu kwa ujumla," alisema.
Mbali na
hilo pia alisema wapo kwenye harakati ya kusaka wadhamini ambao ndio
watakaowawezesha kukamilisha mpango wao wa usajili wa wachezaji ambao
wamewaona ndio watakaoisaidia timu kufika pazuri.
"Kuna
mambo mengi yanaendelea katika kikosi chetu ya kuhakikisha tunaanza ligi
msimu ujao timu ikiwa imejipanga kwa ajili ya kufanya kazi na si
vinginevyo," alisema.
http://www.mwanaspoti.co.tz/
No comments:
Post a Comment