Njia 3 muhimu katika ujenzi wa uchumi wa gesi Tanzania
Na Dk. A. Massawe
YA KWANZA
Mojawapo
ya njia zitakazofanikisha matumizi ya gesi yetu asilia hapa chini yawe
yenye tija zaidi ni ile ya kuisambaza maeneo yote nchini kwa kuanzia na
miji mikuu ya kanda au mikoa kwa ajili ya matumizi ya majumbani na
viwandani na kuzalisha umeme kwa ajili ya matumizi ya pale pale
unapozalishwa.
Kusafirisha
gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam itakakotumika kuzalishia
umeme, majumbani na viwandani ni sahihi tu kama umeme wote
utakaozalishwa utatumika ndani ya ukanda wa Dar es Salaam.
Yaani, ni
sehemu kidogo tu ya gesi asilia inayowasili Dar es Salaam ingebaki hapo
hapo kwa ajili ya kuzalisha umeme na matumizi ya majumbani na viwandani
ndani ya ukanda wa Dar es Salaam na kitakachosalia kiendelee na safari
yake hadi kanda nyingine za Tanzania kuzalisha umeme na kwa ajili ya
matumizi mengine ya moja kwa moja majumbani na viwandani kuendana na
mahitaji ya kila kanda.
Lengo ni
kuondokana upotevu mkubwa wa umeme na gharama kubwa ya kuusafirisha
umbali mkubwa kutoka kanda moja ya Tanzania hadi nyingine, pia
ikizingatiwa kwamba, zaidi ya umeme, kila kanda hapa Tanzania pia
inahitaji gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya moja kwa moja majumbani
na viwandani kama Dar es Salaam.
Hivyo ni
kosa kuzalisha umeme wa megawati 3000 hapa Dar es Salaam kutokana na
gesi asilia ya Mtwara kwa ajili ya matumizi ya ukanda wa Dar es Salaam
na kanda nyingine zilizoko mbali na Dar es Salaam kwani njia sahihi ni
kusambaza uzalishaji wa umeme utokanao na gesi asilia kote nchini kwa
kusambaza gesi asilia kote nchini kwa njia ya mabomba na kufunga mitambo
midogo midogo ya uzalishaji wa umeme wa gesi asilia kwenye kila kanda
kuendana na mahitaji halisi ya kanda.
Hivyo,
cha muhimu zaidi kwenye kufanikisha matumizi ya gesi asilia hapa nchini
yawe yenye tija tosha ni kujenga miundo mbinu ya mabomba kwa ajili ya
usambazaji gesi asilia kikanda kote nchini itakakozalisha umeme na
kutumika moja kwa moja majumbani na viwandani kikanda kuendana na
mahitaji halisi kikanda ili kukwepa upotevu mkubwa wa umeme na gharama
kubwa za kuusafirisha umbali mkubwa kutoka kanda hadi kanda, huku
ikizingatiwa kwamba, zaidi ya umeme, kanda zote pia zinahitaji gesi
asilia kwa ajili ya matumizi ya moja kwa moja majumbani na viwandani
kama Dar es Salaam.(P.T)
YA PILI
Njia ya
pili itakayofanikisha matumizi yenye tija ya raslimali ya gesi asilia
iliyogundulika hapa nchini ni kutumia hisa za Serikali kwenye raslimali
hiyo iliyoko ardhini ikisubiria kuanza kuvunwa kama rehani kuchukulia
mikopo kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya kuzalishia umeme wa maji huko
Stigler's na wa makaa ya mawe huko Mchuchuma na kwingineko. Ni matumizi
yanayowezesha kurudisha mikopo na kuleta faida hata kabla uchimbaji wa
gesi asilia iliyotumiwa kama rehani haujaenda mbali sana, huku
ikizingatiwa kwamba maelfu ya megwati za umeme wa maji ambazo
hazijavunwa huko Stiglers na kwngineko hapa nchi huwa zikipotea kila saa
miaka nenda rudi wakati gesi asilia na makaa ya mawe yanaweza kusubiri
ardhini hadi uvunwaji wake kwa ajili ya uzalishaji wa umeme utakapoanza.
YA TATU
Njia ya
tatu itakayofanikisha matumizi yenye tija tosha ya raslimali ya gesi
asilia iliyogundulika hapa nchini ni kuwekeza mapato ya serikali
yatokanayo na uvunwaji wa ralimali yake ya gesi asilia kwenye mfuko
endelevu ''Sovereignity Fund''wa kutolea mikopo yenye riba nafuu kwa
sekta za umma (kwa ajili ya kuwekeza kwenye ujenzi na uendelezaji wa
miundo mbinu ya kitaifa na kwenye makampuni ya kimataifa yaliyo mihimili
mikuu ya maendeleo ya uchumi wa dunia kisayansi na kiteknolojia
(kuiwezesha Tanzania kuwa sehemu ya wahimili wakuu wa uchumi wa dunia
kisayansi na kitknolojia na kuwa mmojawapo ya wanaonufaika sana), na kwa
sekta binafsi (kuwezesha ukuwaji wa ujasiriamali hapa nchini).
Ni
kuzingatia kwamba raslimali ya gesi asilia hapa nchini ni urithi usio
endelevu wa vizazi vyote vya Tanzania, na njia ya kuhakikisha matumizi
yake ni yenye manufaa makubwa zaidi kwa vizazi vyote vya Tanzania ni
kutumia mapato ya serikali yatokanayo na uvunwaji wake kama kianzio
endelevu cha mikopo yenye riba nafuu kwa sekta binafsi na za umma kote
nchini.
Chanzo:wavuti.com
No comments:
Post a Comment