JK awananga wanasiasa wanaotumia mgongo wa dini
Rais
Jakaya Kikwete akiwa kwenye picha ya pamoja na maaskofu wa kanisa la
Katoliki mara baada ya kumalizika kwa ibada ya kumweka wakfu askofu mpya
wa jimbo katoliki Shinyanga, Mhashamau baba Askofu Leberatus Sangu
Shinyanga.
Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa dini nchini kutowaonea haya
viongozi wa kisiasa wanaotaka kugeuza nyumba za ibada kuwa majukwaa ya
kufanyia siasa kwa kuwa hali hiyo inaweza kusababisha vita ya kidini au
waumini kwa waumini.
Rais
Kikwete alisema hayo jana wakati wa ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa
rasmi, askofu mpya wa Jimbo la Shinyanga, Liberatus Sangu katika Kanisa
la Mama Mwenye Huruma, Parokia ya Ngokolo, Shinyanga.
Aliwataka
viongozi hao kuhakikisha makanisa na misikiti inabaki kuwa sehemu ya
ibada na usuluhishi na iwapo watashindwa, inaweza kusababisha makundi na
mapigano.
"Katika
kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, wanasiasa wengi wanapenda
kutumia tofauti za rangi, ukabila na dini nawaomba msiruhusu mambo hayo
ni hatari kwa Taifa, endeleeni kukemea jambo lolote ambalo mnaona
linakwenda tofauti."
Rais
Kikwete pia alizungumzia mauaji ya vikongwe na albino huku alimtaka
Askofu Sangu na maaskofu wengine kuongeza bidii kuwalea waumini wao
katika imani, ili waachane na vitendo vya kishirikina ambavyo ndivyo
chanzo cha mauaji yao.
Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo
alimsimika rasmi Askofu Sangu na kumkabidhi fimbo ya kichungaji huku
akimtaka kuhakikisha anafanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wengine
na kumtakia heri na baraka katika muda wake wote wa kitume.
Kwa
upande wake, Askofu Sangu alisema kazi kubwa iliyo mbele yake ni
kuhakikisha analinda na kustawisha mema yote yaliyoachwa na
waliomtangulia.
"Nitashirikiana
na viongozi wenzangu pamoja na Serikali katika masuala mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kukemea mauaji ya vikongwe na albino. Sala zenu ndizo
ambazo zimesababisha mimi nikateuliwa na baba mtakatifu kuwa askofu na
leo hii nimesimikwa rasmi kuanza kazi katika jimbo hili la Shinyanga,
nawaomba waumini wote tushirikiane kwa pamoja katika kazi hii."
Mwenyekiti
wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa
alimtaka Askofu Sangu kuchunga kondoo wake aliokabidhiwa kwani
wanahitaji upendo pamoja na kushirikiana vizuri na wasaidizi wake katika
kuleta maendeleo na kuwalea waumini kiimani.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.CHANZO: MWANANCHI (Muro)
No comments:
Post a Comment