Rais wa Chama cha Walimu Tanzania Gratian Mukoba.
UCHAGUZI
wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Simiyu uliofanyika jana,
nusura uvunjike baada ya baadhi ya wagombea, kuanza kutuhumiana ndani ya
ukumbi wakati wakijieleza kwa wajumbe.
Mmoja wa
wagombea hao ambaye alikuwa akigombea nafasi ya Uwakilishi wa Kamati
Tendaji Taifa, Chananja Buluba alipopewa nafasi ya kujieleza, alidai
kuwa uchaguzi huo umegubikwa na vitendo vya rushwa.
Alidai
kuna baadhi ya wajumbe walipewa Sh 50,000 hadi Sh 100,000 kutoka kwa
wagombea wa nafasi za Uwakilishi wa Kamati Tendaji Taifa, Mwenyekiti na
Mweka Hazina.
Akiwa
anazomewa na baadhi ya wajumbe hao, mgombea huyo alieleza kuwa mbali na
kupewa fedha, baadhi ya wajumbe walilipiwa sehemu za kulala kwa siku
tatu pamoja na chakula.
Hali hiyo
ilionekana kuwakera wajumbe wa uchaguzi huo na kumtaka athibitishe
mbele yao na kuwataja watu ambao walipewa pesa, kulipiwa sehemu za
kulala pamoja na chakula.
Akiwa
tayari kutaka kuwataja wahusika wa vitendo hivyo, mgombea huyo
alizuiliwa na Mratibu wa Uchaguzi huo ambaye ni Katibu wa CWT mkoani
hapa, Fatuma Bakari kwa madai kuwa alikuwa amekiuka taratibu za
uchaguzi.
Kitendo
cha kuzuiliwa na katibu huyo, kilionekana kumkera mgombea huyo na kuacha
kujieleza mbele za wajumbe hao, ambapo aliamua kuwaita waandishi wa
habari nje ya ukumbi wa mkutano ili kuwaeleza hali hiyo.
"
Nimechukia sana kitendo cha Mratibu ambaye ni Katibu CWT Mkoa
kunizuia...hali ya uchaguzi huu imechafuliwa sana na rushwa, wagombea
wamegawa pesa kama karanga na sijui wametoa wapi wakati wao ni walimu
kama mimi," alisema Buluba.
Alibainisha
kuwa pesa walizokuwa wakizitoa wagombea hao, zilikuwa na ufadhili
kutoka katika vyama vikubwa vya siasa, alivyovitaja.
Alisisitiza
kuwa hakuna mwalimu ambaye anaweza kumpatia mwalimu mwenzake, kiwango
hicho kikubwa cha pesa. " Nina muda mrefu katika taaluma hii ya
walimu...hizi pesa ni nyingi, wajumbe wote walipewa pesa hasa nafasi
hizo za juu...watu wanalipiwa sehemu za kulala, chakula bure kwa siku
tatu...tuligundua kuna ufadhili mkubwa wa vyama," alisema.
Hata
hivyo, licha ya baadhi ya wajumbe kupewa kiasi hicho, alibainisha kuwepo
kwa baadhi ya wagombea waliojitoa kugombea nafasi mbalimbali baada ya
kupewa Sh 500,000. Buluba aliitaka Takukuru kuchunguza hali hiyo, kabla
hajachukua maamuzi mengine, huku akitishia kuachana na chama hicho na
kuanzisha chama kingine mbadala wa CWT.
"
Najipanga kuanzisha mbadala wa CWT kwa sababu chama hiki ni rushwa kila
sehemu kila mara.. CWT ya sasa imeshindwa kuwatetea walimu na badala
yake kimegeuka kuwa chama cha kisiasa," alisema.
Katibu wa
chama hicho ambaye ndiye alikuwa Mratibu wa uchaguzi huo, Fatuma Bakari
alikiri kupata taarifa za kuwepo kwa vitendo hivyo, huku akidai kuwa
hakuna mtu ambaye ametajwa kufanya vitendo hivyo.
" Taarifa
hata sisi tumepewa kuwepo kwa vitendo hivyo, ndiyo maana kwenye
uchaguzi nimemzuia mgombea huyo kuwataja wahusika kwa sababu kanuni za
uchaguzi zinakataza, lakini ningeliruhusu kikao kilikuwa kinavunjika
kutokana na hali niliyoiona," alisema Bakari.
Uchaguzi
huo ulifanyika na Dwese Kulwa alichaguliwa kuwa Mwenyekiti kwa kura 52.
Mweka Hazina ni Joyce Nkomangwa aliyepata kura 45 na Mwakilishi wa
Kamati Tendaji Taifa ni Julius Mategemeo, aliyepata kura 50.CHANZO:HABARI LEO (Muro)