MANULA AIPELEKA AZAM FC NUSUFAINALI KAGAME CUP

Wachezaji
 wa Azam FC wakimpongeza golipa wao Aishi Manula baada ya kudaka penati 
iliyopigwa na Hajji Mwinyi na kuivusha timu yake hadi kwenye hatiua ya 
nusu fainali ya Kagame
Timu Azam
 FC ‘Wanalambalamba’ wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya 
michuano ya Kagame baada ya kuitupa nje ya mashindano timu ya Yanga 
kwenye mchezo wa robo fainali uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa.
Timu hizo
 zililazimika kufika hadi kwenye hatua ya mikwaju ya penati kufuatia 
kumalizika kwa mchezo huku timu hizo zikiwa sare ya bila kufungana. Kwa 
mujibu wa kanuni za mashindano ya Kagame, hatua ya robo fainali 
inapomalizika ndani ya dakika 90 bila timu kufungana zinakwenda moja kwa
 moja kwenye changamoto ya mikwaju ya penati.
Aishi 
Manula alipangua penati ya Haji Mwinyi ambayo ilikuwa ni penati ya tatu 
kwa upande wa Yanga na kufanikiwa kuivusha timu yake hadi kwenye hatua 
ya nusu fainali ya michuano hiyo ambapo penati za Azam zote ziliwekwa 
kambani.(P.T)
Kipre 
Tchetche, John Bocco, Himid Mao, Pascal Wawa na Agrey Morris walifunga 
mikwaju yao kwa upande wa Azam wakati Salum Telela, Nadir Haroub 
‘Cannavaro’ na Godfrey Mwashiuya walifunga penati zao huku Hajji Mwinyi 
yeye penati yake ikidakwa na mlinda mlango wa Azam FC Aishi Manula.
Mpira 
ulianza kwa kasi sana dakika za mwazo za kipindi cha kwanza, huku Azam 
wakifanya shambulizi kali dakika hiyohiyo ya kwanza ambapo Kipre Tchethe
 alishindwa kufunga goli baada ya Shah Farid Mussa kupiga krosi 
iliyowapita walinzi wa Yanga na kumkuta yeye ambae aliukosa mpira.
Azam 
hawakuishia hapo waliendelea kufanya mashambulizi lakini wachezaji wa 
Azam hawakuwa makini kwani hadi kipindi cha kwanza kinamalizika walikuwa
 wamekosa takribani nafasi nne za kufunga.
Kwa 
upande wa Yanga, kipindi cha kwanza hakikuwa kizuri sana kwao kwasababu 
hawakufanya mashambulizi mengi ambayo yaliwashtua Azam. Shambulizi 
lililofanywa na Yanga lilitokana na mpira wa kurusha ambapo Mbuyu Twite 
alirusha mpira uliookolewa kwenye mwamba wa pembeni wa goli na mlinda 
mlango Aishi Manula.
Wachezaji
 wa Azam walikuwa wakitumia nguvu nyingi sana kuwakaba wachezaji wa 
Yanga hali ilyopelekea mwamuzi kuwatuliza kwa kuwapa kadi za njano. 
Kheri Abdullah Salum, Frank Domayo, Jean Mugiraneza na Ame Ally 
walioneshwa kadi za njano baada ya kuwachezea vibaya wachezaji wa Yanga.
 Wakati kwa upande wa Yanga Juma Abdul na Mbuyu Twite walioneshwa kadi 
za njano.
Kipindi 
cha pili kilianza kwa Azam kufanya mabadiliko kwa kumtoa Kreri Abdullah 
Salum na nafasi yake ikachukuiwa na Said Morad wakati Frank Domayo 
‘Chumvi’ alipumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Ame Ally ‘Zungu’. 
Yanga wao wakamuingiza Salum Telela kuchukua nafasi ya Deus Kaseke 
wakati Juma Abdul alitoka kumpisha Joseph Zutah na Malimi Busungu 
akaingia baada ya Amis Tambwe kupumzishwa.
Kipindi 
cha pili bado Azam waliendelea kukosa magoli kwani Kipre Tchetche, Ame 
Ally na Shah Farid Mussa walikosa goli baada ya kujichanganya wao kwa 
wao na mpira kunyakwa na mlinda mlango Ally Mustafa ‘Barthez’
Kwa 
matokeo hayo, Azam FC inakamilisha timu nne zilizofuzu kucheza hatua ya 
nusu fainali ya michuano ya Kagame kwa mwaka 2015 ambapo Ijumaa 
itakutana na KCCA ya Uganda iliyofuzu kucheza hatua ya nusu fainali leo 
mchana kwa kuibanjua timu ya Al Shandy ya Sudan kwa goli 3-0 huku Yanga 
wakiwa wameyapa mkono wa kwaheri mashindano ya Kagame kwa mwaka 2015.
Chanzo:Shaffihdauda.com
No comments:
Post a Comment