Wiki ngumu Bunge la Katiba yaanza leo
Wajumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba wenye mahitaji maalumu wakishauriana wakati
wa semina ya Jumuiya za Serikali za Mitaa (ALAT) kuhusu marekebisho ya
Rasimu ya Katiba sura ya sita, Ibara ya 68(2) mamlaka ya wananchi na
mapendekezo ya sura mpya ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi kupitia
Serikali za Mitaa.Semina hiyo ilifanyika Dodoma jana. Picha na Salim
Shao
Dodoma
Bunge
Maalumu la Katiba leo linaanza wiki ngumu pale litakapohitimisha mjadala
wa muundo wa Muungano na kupiga kura kupitisha au kukataa.
Hiyo inatokana na ukweli kwamba muundo huo wa muungano ndiyo unaotabiriwa kubeba ajenda zote katika mjadala huo wa Katiba.
Kwa mara
ya kwanza wiki hii Watanzania watashuhudia hatua ya upigaji kura ambayo
awali iliibua mvutano mkubwa wakati wa kupitishwa kanuni ili kuamua
mfumo gani utumike kati ya kura ya siri na wazi.(MM)
Katika
hili, mjumbe atakuwa na uhuru wa kupiga kura ya wazi au ya siri wakati
wa kupitisha sura namba moja na namba sita. Ili zipite, ni lazima zipate
theluthi mbili ya kura kwa kila upande wa Muungano.
Hata
hivyo, leo Bunge hilo litaanza kwa kumpa nafasi Mjumbe wa Bunge hilo,
Tundu Lissu kuendelea kutoa ufafanuzi wa hoja za walio wachache kwenye
Kamati Namba Nne.
Ufafanuzi
huo wa Lissu uliahirishwa juzi baada ya matangazo ya moja kwa moja ya
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kukatika ghafla.
Baada ya
Lissu kumaliza, kamati zilizobaki ambazo ni Namba Sita inayoongozwa na
Steven Wassira, Kamati Namba Saba inayoongozwa na Brigedia Jenerali
mstaafu Hassan Ngwilizi zitawasilisha taarifa zao.
Inatarajiwa
kuwa katika kipindi cha mchana, Kamati Namba 10 inayoongozwa na Anna
Abdallah itawasilisha taarifa yake na kufuatiwa na ufafanuzi wa wajumbe
walio wachache wa kamati hizo.
Kulingana
na hali ya mambo ilivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba, wataanza kuchangia taarifa za kamati zote 12 katika
kipindi cha jioni au kesho asubuhi.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 33 (7), baada ya taarifa ya kamati hizo kuwasilishwa, zitajadiliwa katika kipindi kisichozidi siku tatu.
Kama
mambo yatakwenda kama ilivyo, inatarajiwa kuwa upigaji wa kura kupitisha
sura hizo mbili huenda ukafanyika Ijumaa na hivyo kutegua kitendawili
cha muda mrefu kuhusu aina ya muundo wa Muungano katika Katiba Mpya.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment