WARIOBA ATUNUKIWA NISHANI ILIYOTUKUKA
Na Hudugu Ng'amilo
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba juzi
usiku alikuwa miongoni mwa viongozi na watu mashuhuri waliotunukiwa
nishani na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika
maelezo ya kutoa nishani ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano daraja la
kwanza, ilielezwa kuwa Jaji Warioba, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliuenzi na bado anauenzi Muungano huo.
"Katika
kipindi chako, pamoja na nyadhifa nyingine, ulikuwa Waziri Mkuu na
Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani...katika
kipindi hicho na hadi sasa umeendelea kuwa mwaminifu, umeutunza,
umeulinda na umeuenzi Muungano," ilisema sehemu ya taarifa ya kutoa
nishani.
Hivi
karibuni, Jaji Warioba amekuwa akishambuliwa na baadhi ya Wajumbe wa
Bunge la Maalumu la Katiba, pia baadhi ya wana CCM kutokana na Rasimu ya
Pili ya Katiba Mpya iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
aliyoiongoza, kupendekeza muundo wa Muungano wa Serikali tatu.
Hata
hivyo, upande mwingine wajumbe wanaojitambulisha kama Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) wamekuwa wakiunga mkono mapendekezo ya rasimu hiyo.
Mbali na
Jaji Warioba, wengine waliopewa nishani katika daraja hilo ni Aboud
Jumbe Mwinyi aliyekuwa Rais wa Pili wa Zanzibar, Aman Karume, John
Malecela, Cleopa Msuya na Dk Salmin Amour Juma.
Wengine ni Omar Ali Juma na Idrissa Abdul Wakil, ambao sasa ni marehemu.
Walioanza
kupata tuzo na nishani hizo ni waasisi wa Muungano wa Tanzania, Mwalimu
Julius Nyerere na Abeid Karume(wote ni marehemu) na walioendeleza ambao
ni Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Wengine
waliopewa tuzo ni pamoja na viongozi wa majeshi ya ulinzi na usalama
akiwemo Mkuu wa Jenshi la Wananchi (JWTZ), Jenerali Davis Mwamunyange na
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu. Wakuu wa JWTZ wastaafu pia
walikumbukwa akiwemo, Jenerali Mirisho Sarakikya, Jenerali David
Musuguri.
Katika
nishani ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano daraja la nne lilikuwa na
Mama Maria Nyerere na Mama Fatma Karume, Bendi ya Msondo Ngoma pia
ilipewa tuzo kwa kuuenzi Muungano.Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP,
Reginald Mengi alipewa tuzo maalumu akiwa raia wa Tanzania aliyetoa
mchango muhimu katika huduma za jamii.
Wasifu
Mwenyewe
Joseph Warioba aliingia serikalini mwaka 1966, akiwa mwanasheria wa mji
wa Dar er Salaam, nafasi aliyoitumikia kwa muda wa miaka miwili, kisha
kuhamia kuwa mwanasheria wa Baraza la Jiji mpaka mwaka 1970.
Kuanzia mwaka 1976 mpaka 1983 Warioba alitumikia taifa kwa wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Warioba pia aliwahi kuwa Waziri wa Sheria katika awamu ya kwanza iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.
Mwaka 1984 aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, nafasi aliyoitumikia hadi mwaka 1990.
Mwaka 1996 Rais Benjamin Mkapa alimteua kuongoza tume ya kupambana na rushwa.
Mwaka 2007 alioongoza jopo la waangalizi kutoka nchi za Jumuiya ya Madola katika uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Nigeria.
Mwaka 2012 Rais wa awamu ya nne alimteua Warioba kuongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment