SIKU 67 ZA MIPASHO, MATUSI,BUNGE MAALUM LA KATIBA

Na Hudugu Ng'amilo.
Bunge 
Maalumu la Katiba linaahirishwa leo baada ya kukutana kwa siku 67 bila 
kupitisha hata ibara moja kati ya 240 zilizomo katika Rasimu ya Katiba.
Badala 
yake Bunge hilo likiongozwa na Samuel Sitta "Mzee wa Kasi na Viwango" 
linaahirishwa hadi Agosti, mwaka huu likiendelea kujadili Sura ya Kwanza
 na ya Sita zenye jumla ya Ibara 19, zinazohusu masuala yanayojenga 
msingi wa aina ya Muungano unaopendekezwa.
Tume ya 
Mabadiliko ya Katiba katika rasimu iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa 
Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba ilipendekeza muundo wa shirikisho 
lenye serikali tatu, pendekezo ambalo limeligawa Bunge hilo vipande 
viwili.
Kutokana 
na mgawanyiko huo, kauli zenye utata, kejeli, matusi, dhihaka na ubaguzi
 ni mambo yaliyoshika hatamu katika mjadala wa sura hizo mbili, huku 
viongozi wa Bunge; Sitta na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan wakilaumiwa
 kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo.
Mwanzoni 
mwa wiki hii, Mjumbe wa Bunge hilo, Ezekiah Oluoch alimshutumu Sitta 
kwamba ameshindwa kudhibiti nidhamu katika Bunge na kwamba ndiye chanzo 
cha kuondoka kwa wajumbe wapatao 200 ambao ni wanachama wa Umoja wa 
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
"Mwenendo
 wa Bunge Maalumu ulikuwa na dalili zote za kuonyesha kungetokea 
matatizo ndani yake kutokana na mipasho ambayo ilikuwa ikitokea kwa 
wajumbe pamoja na lugha ambazo siyo za staha wakati wa kutengeneza 
kanuni," alisema Oluoch na kuongeza:
"Kwanza 
matumizi ya lugha zisizo na staha, mwenyekiti anaruhusu wajumbe 
kuchangia hoja kwa kupeana mipasho bila kujali hoja iliyopo mezani 
kinyume na kanuni," alisema Olouch.
Hata 
hivyo, Suluhu alisema amekuwa akiendesha Bunge hilo kwa umakini mkubwa 
na kwamba kila anaposikia lugha chafu amekuwa akiwabana wajumbe kwa 
kuwaamuru kufuta kauli au kuomba radhi kwa matamshi. "Sipendezwi na 
lugha chafu, kwa hiyo mojawapo ya mambo ambayo huwa najitahidi 
kusikiliza kwa makini kila michango inapotolewa na wajumbe bungeni ni 
kubaini kama wametumia lugha zisizostahili, kisha kuchukua hatua kwa 
mujibu wa kanuni zetu," alisema Suluhu.
Alikiri 
kwamba wapo baadhi ya wajumbe ambao wamekuwa wakigoma au kukataa kuomba 
radhi na kwamba masuala yao hupelekwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo 
ina mamlaka ya kuchukua hatua zaidi kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo.
Matakwa ya Kanuni
Sehemu ya Tano ya Kanuni za Bunge Maalumu inatoa mwongozo wa mambo yanayokatazwa na yale yanayopaswa kufuatwa wakati wa mjadala.
Kanuni ya
 46 imeorodhesha mambo yasiyoruhusiwa ambayo ni pamoja na kusema uongo, 
kutoa taarifa zisizokuwa za kweli, kuzungumza jambo lolote ambalo halipo
 kwenye mjadala na kutumia majina ya marais na waasisi wa Taifa kwa 
dhihaka.Pia inazuia matumizi ya lugha ya kuudhi, kubagua, kunyanyapaa au
 inayodhalilisha watu wengine, kuzomea, kupiga kelele za aina yoyote 
zinazoweza kuvuruga mjadala au mwenendo bora wa shughuli za Bunge hilo.
Licha ya 
makatazo hayo, wajumbe wamekuwa wakikiuka kanuni bila kuchukuliwa hatua 
na hali hiyo imekuwa chanzo cha mivutano, zomeazomea, kelele na mambo 
mengine hadi kundi la Ukawa kususia kikao wakieleza kutokuridhishwa na 
mwenendo wa Bunge.
Kuufyata na kuufyatua
Baadhi ya
 kauli tata zilizojitokeza ni pamoja na ile iliyotolewa na Asha Bakari 
Makame kwa mjumbe mwenzake, Ismail Jussa kuwa anafanana na watu wenye 
mabusha nyuma ambao ndiyo huufyata.
Makame 
ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), 
alikwenda mbali zaidi na kumwambia Jussa kuwa ana matatizo ya kiafya na 
si mwanamume kamili, kwani ameshindwa kuoa na hana watoto wakati ana 
umri mkubwa.
"Huyu 
Jussa anasema kwamba tumeufyata, hapa tuwekane sawa, maana ya kuufyata 
ni mtu kuwa na mabusha pale yanapokuwa nyuma ndiyo kuufyata kwa hiyo 
yeye ndiyo ameufyata, ana busha huyu," alisema Bakari.
Naye 
Profesa Ibrahim Lipumba alichafua hali ya hewa pale alipowafananisha 
wajumbe wa Bunge Maalumu na kundi la mauaji nchini Rwanda, Intarahamwe.
"Tumechoka
 kusikiliza matusi. "Tumechoka kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka 
ubaguzi hatuwezi kuwa sehemu ya kundi la Intarahamwe linalohamasisha 
ubaguzi ndani ya Tanzania hili hatulikubali. Tunawaachia, watu wote 
tunaotaka Katiba ya wananchi tunawaachia Intarahamwe mwendelee na Bunge 
lenu."
Mjumbe 
mwingine ni Mwanakhamis Kassim Said aliyesema: "Mimi nilikuwa namwomba 
baba yangu mdogo Seif (Maalim Seif Sharif Hamad) awarejeshe watu wake 
humu (bungeni) kwa sababu mpira unachezwa huku ndani. Hatutakii mema 
humu, tena ana choyo na husuda. Namwomba baba mdogo atuache, 
alichokitaka amekipata, king'ora anazunguka saa 24 Dar es Salaam, 
Unguja. Mheshimiwa Mwenyekiti Baba mdogo kila mara yuko kwenye pipa 
(ndege) mara Uingereza, mara Canada mara wapi? Hicho ndicho anachokitaka
 amekipata."
Mjumbe 
mwingine, Mohamed Seif Khatibu alisema: "Nimejifunza kuwa baadhi ya 
wanasiasa wa upinzani ni vinyonga. Lakini Maalim Seif ni kinyonga, 
wakipita kwenye mvua wanakuwa na rangi ya mvua, kwenye jua wanakuwa na 
rangi ya jua, baharini wanakuwa na rangi ya bahari."
Tuhuma za rushwa
Mjumbe 
Ezekiah Wenje alisema baadhi ya mawaziri wamewahonga wajumbe wa kundi la
 201 ili waunge mkono msimamo wao, lakini alipotakiwa kufuta kauli hiyo 
alikataa na suala lake kufikishwa kwenye kamati ya kanuni.Kuna wajumbe 
wengine walikwenda hadi kwa waziri mkuu ambako walikula, walikunywa hadi
 saa 7:00 usiku, wengine walikwenda kwa Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi
 na Ajira) na walikula na kunywa na kupewa bahasha."
Kuingia msituni
Kapteni 
John Komba alitangaza kuingia msituni iwapo Bunge Maalumu la Katiba 
litapitisha muundo wa serikali tatu, huku akimshutumu Mwenyekiti wa Tume
 ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na timu yake ni waasi 
kama Adamu na Eva waliomuasi Mungu kutokana na kile walichokifanya cha 
kupendekeza serikali tatu. Mwingine katika orodha ni Bernard Membe 
aliyesema, Tume ya Mzee Warioba itakuja kukumbukwa kwa kuratibu mauaji 
ya Muungano na Bunge nalo litakuja kulaaniwa kwa kubariki mauaji hayo.
Watoto wa shetani
Mjumbe 
Paul Makonda alisema: "Shetani alikuja duniani kuiharibu dunia, 
kuiangamiza na kuteketeza kila kilichostahili kuungana... watoto wake ni
 Mheshimiwa Jussa, watoto wake ni Mheshimiwa Mbowe, watoto wake ni 
Mheshimiwa Lipumba... Hawa ni watoto wa shetani".
Mwingine:
 Waride Bakari Jabu alisema: "Chiku Abwao mimi namshangaa sana anayesema
 bora Muungano uvunjike lakini Tanganyika iwepo. Tunafahamu asili yake 
mwenyewe ni Mkongo mumewe ndiye Mtanganyika, namwambia Muungano huu 
utakuwepo na utaendelea kuwapo."
Mjumbe 
Tundu Lissu alisema: "Tanganyika haikuuawa na makubaliano ya Muungano, 
bali iliuawa kwa amri za Nyerere.... Mwalimu Nyerere hakuwa na mamlaka 
yoyote ya kikatiba ya kutunga amri na kuua Tanganyika."
Imeandikwa na Neville Meena, Daniel Mjema, Sharon Sauwa na Beatrice Moses
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment