Lukuvi: Tukipitisha serikali tatu jeshi litatawala nchi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi.PICHA|MAKTABA
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi
ameanza kampeni kanisani kuwataka wananchi kupinga serikali tatu
zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo nchi
itatawaliwa na jeshi kwa kuwa Serikali ya Muungano itashindwa kuwalipa
mishahara wanajeshi.
Alisema hayo jana katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Katika
hotuba yake, Lukuvi aliwaeleza waumini waliofurika katika ibada ya
kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa askofu wa kanisa hilo katika
jimbo kuwa waendelee kuliombea Bunge lifanye uamuzi sahihi wa serikali
mbili.(MM)
Aliwataka
Watanzania kuipuuza Rasimu ya Katiba katika suala la Muungano na
Serikali tatu kwa madai kuwa kutaka kuwapo mfumo huo ni kutaka
Watanzania waingie vitani.
"Serikali
tatu zikipita ni wazi kuwa hata makanisa yatafungwa kwani nchi haiwezi
kuwa na amani tena, angalieni nchi ya Korea Kusini na Korea Kaskazini
ambao waligawanyika na sasa ni maadui wakubwa wanaokaa mipakani
wamenyoosheana bunduki," alisema na kuongeza:
"Waumini
ndugu zangu wapendwa, kwa sasa tupo katika hali mbaya sana hapo bungeni,
tunaomba mtuombee kuna watu ambao wanataka madaraka kwa nguvu na
wameanza kutafuta jinsi ya kuvunja Muungano na kudai kuwapo kwa Serikali
tatu, nawaomba sana wapuuzeni wale wote ambao wanataka serikali tatu."
Alisema
watu wa aina hiyo wanaonekana kuwa wana huruma na Watanzania na wanadai
kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika wakati hiyo Tanganyika wanayoidai ni
jina tu ambalo Wajerumani walikaa mezani wakabuni na kutuletea.
Lukuvi
alisema Wazanzibari wanaotaka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea,
bali wanataka Serikali ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa ni nchi ya
Kiislamu.
Alisema
wanaopiga kelele wana ajenda za siri na nia yao kutaka kufanya fujo na
kusababisha machafuko... "Kwani ukiwa na mke mmoja akakushinda unafikiri
utatuzi ni kuoa mke mwingine?"
Baadaye
alipotakiwa kufafanua kauli yake, Lukuvi alisema alichokizungumza
kanisani hapo ni mawazo yake binafsi ambayo yanafanana na Watanzania
wengi, akiwamo Rais Jakaya Kikwete.
"Unajua
jeshi haliwezi kukaa na bunduki bila fedha. Hiyo Serikali ya tatu ambayo
jeshi litakuwa chini yake haina vyanzo vya mapato vya kueleweka, sasa
hao wanajeshi watalipwa nini? Wenye mitutu watakubali kuishi bila
fedha?"
Alisema
hata vyanzo vya mapato ambavyo vimeandikwa katika Rasimu ya Katiba ni
lazima visimamiwe na pande mbili za Muungano, akiwa na maana ya
Tanganyika na Zanzibar na kwamba kama upande mmoja ukishindwa kuchangia
hali itakuwa mbaya.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment