TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, April 8, 2014

Dk. Slaa: Upinzani hatuna lengo la kuvunja Muungano

Willbroad-Slaa-April8-2014 be37a
Na Hudugu Ng'amilo
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, amewataka Watanzania kutambua kuwa hakuna chama cha upinzani ambacho kina lengo la kuvunja Muungano bali yanayoelezwa ni njama ya kudhoofisha msimamo wa kuwapo kwa serikali tatu.
Alitoa kauli hiyo jana katika viwanja vya Tangamano, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa jiji la Tanga, baada ya kuongoza timu ya viongozi wa juu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mjini hapa na kuwataka wakazi wa jiji hilo kukataa hadaa zinazofanywa kwa lengo la kukanyaga rasimu ya katiba, ambayo waliitolea maoni yao.
Alisema kilichofanywa na Rais Jakaya Kikwete, wakati akilihutubia Bunge Maalumu la Katiba kuiponda rasimu ya katiba ni kumdhalilisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ambaye ni kiongozi mwenye heshima Tanzania na nje ya nchi na kwamba, Ukawa itazunguka nchini kote kumtetea.
Dk. Slaa ambaye ni Mwenyekiti wa Ukawa nje ya Bunge hilo, alisema Rais Kikwete anawahadaa wananchi anaposema wanaotaka serikali tatu wana lengo la kuvunja Muungano na kusisitiza kuwa hakuna chama chochote cha upinzania, ambacho kinataka Muungano uvunjike.
"Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na wananchi wote wa Tanzania Bara na hata visiwani, hakuna anayetaka Muungano uvunjike, bali kinachofanywa na CCM ni kuwachonganisha kwa wananchi ili waonekane ni maadui wa Muungano," alisema Dk. Slaa.
Alisema inasikitisha kuona kuwa kuna baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar ndani ya Bunge hilo wakidanganywa kuahidiwa kupewa fedha za kuwasomesha ili waunge mkono msimamo wa kupiga kura ya serikali mbili jambo ambalo ni kinyume cha malengo ya uwakilishi wao kwa Watanzania.
"Chini ya Umoja wao wa Ukawa wanachofanya ni kutetea maoni ya wananchi yaliyotolewa kwenye Tume ya Katiba kwa kuwa Tanzania ni nchi ya wote na hakuna, ambaye akifa atazikwa nje ya nchi hii. Hivyo, ni lazima kutetea maslahi ya wananchi," alisema Dk. Slaa.
KAIMU KATIBU MKUU WA CUF ANENA
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Shaweji Mketo, alisema Tume ya Maridhiano ya Zanzibar inayoundwa na viongozi kutoka CCM na CUF ikiongozwa na Nassoro Moyo, imetoa tamko la kumtaka Rais asidhani Watanzania ni watu wa kuhadaiwa, bali watatetea serikali tatu kwa kuwa ina lengo la kuimarisha Muungano uliopo.
CHANZO: NIPASHE.

No comments:

Post a Comment