KAMATI YA MAADILI NA HAKI YAKWAMA KUMUHUKUMU WENJE
Na Hudugu Ng'amilo
Hukumu
dhidi ya mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Ezekiah Wenje imekwama
kutolewa jana baada ya mjumbe huyo kushindwa kupatikana ili kuwasilisha
utetezi wake.
Wenje
anadaiwa kuwatuhumu mawaziri wanne akiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa
kutoa rushwa kwa wajumbe wa kundi la 201, ili wapitishe kura ya wazi na
kuunga mkono serikali mbili.
Viongozi
wengine waliohusishwa na tuhuma hizo ni Waziri wa Maji Profesa Jumanne
Maghembe, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka.
Mwenyekiti
wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta aliamua kulipeleka shauri
kwenye kamati ya maadili na haki za Bunge, baada ya Wenje kukataa kufuta
kauli yake na kuwaomba radhi wajumbe hao.
Akiwasilisha
taarifa ya kamati hiyo bungeni jana kwa niaba ya mwenyekiti, Pandu
Ameir Kificho, makamu mwenyekiti, Dk Susan Kolimba alisema jitihada za
kumtafuta Wenje bado zinaendelea.
Hata
hivyo Dk Kolimba alisema kamati yake imefanikiwa kuwahoji Dk Kawambwa na
Kabaka pamoja na wajumbe wawili kutoka kundi la 201 waliolalamika,
Esther Mlimba na Dk Eve Semakafu.
"Mwenyekiti
alipomtaka kuomba radhi alisema anaweza kuomba radhi kwa msingi tu
kwamba ukweli aliousema umewaudhi watu, hivyo anaomba radhi kwa ukweli
aliousema," alisema Dk Kolimba.
Alisema
baada ya Wenje kutopatikana, kamati hiyo iliona ni busara kuwasikiliza
mawaziri waliotuhumiwa pamoja na wale waliolalamikia kauli hiyo ya Wenje
ambao ni Semakafu na Mlimba.
"Jitihada
za kumtafuta Maghembe zilishindikana...Tunatarajia baada ya Wenje
kufika mbele ya kamati tutawasilisha mapendekezo yetu mbele ya Bunge
hili,"alisema Dk Kolimba.
Baada ya
kutolewa kwa taarifa hiyo, Sitta alisema suala hilo litaamuliwa hapo
baadaye baada ya kamati hiyo kukamilisha kazi yake ikiwamo kumhoji Wenje
na wengine waliotuhumiwa.
:Chanzo Mwananchi.
:Chanzo Mwananchi.
No comments:
Post a Comment