THRDC wapinga Bunge kupigia kura muundo wa serikali
Na Hudugu Ng'amilo
Mtandao
wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umesema hatua ya wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba kutaka kupiga kura kuamua muundo wa serikali ni
kosa kubwa la kisheria.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Mtandao huo, Onesmo Olengurumwa, alisema hayo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika warsha ya usalama na tathmini
ya athari za kiusalama kwa waandishi wa habari.
Alisema
suala la Muungano ni la wananchi na siyo la wajumbe 639, hivyo hawapaswi
kuliamua kwa kupiga kura kwa kuwa wananchi wameshatoa maoni yao kwenye
Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa kwenye Bunge hilo.
"Chombo
cha kisheria, ambacho ni Tume ya Mabadiliko ya Katiba ndicho kiliwahoji
wananchi na hadi sasa hakuna chombo kingine kilichoeleza kuyakana maoni
ya wananchi hao," alisema.
Olengurumo
ambaye ni mwanasheria kitaaluma, alisema Bunge kupiga kura ya muundo wa
serikali ni kosa kwa kuwa halina mamlaka ya kubadili na badala yake
kufuata rasimu ya wananchi, ambayo ndiyo ya kuaminika siyo kuwaamulia.
"Kuna
nchi, ambazo ziliruhusu mambo yenye utata kupelekwa kwa wananchi na
kupigiwa kura ya maamuzi, suala la Muungano linaweza kusubiri kwanza na
kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya maamuzi," alisema Olengurumwa.
Alisema
wajumbe hao wasijisahau na kuamua mambo ambayo hawana mamlaka nayo kwa
kuwa Muungano wa nchi mbili hauwezi kuamualiwa na watu 639.
Olengurumo
alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni tata kuliko yote duniani,
hivyo unapaswa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa.
CHANZO NIPASHE
No comments:
Post a Comment