TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, April 15, 2014

Serikali yajitetea ubovu miundombinu 


Wananchi wakipita kwa taabu katika sehemu finyu ya barabara ya Kilwa maeneo ya Mbagala, iliyoharibiwa na maji ya mvua na kusababisha magari kushindwa kupita. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Wizara ya Ujenzi imesema kuwa asilimia kubwa ya miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko haikujengwa chini ya kiwango kama inavyodaiwa, bali ni matokeo ya uharibifu wa mazingira.(MM)
Akizungumza na gazeti hili jana, Msemaji wa wizara hiyo, Martin Ntemo alisema madaraja mengi yaliyoharibiwa na mvua zinazoendelea nchini yameliwa katika makutano na barabara na si kumeguka.
"Mito mingi imechepuka katika mikondo yake ya zamani kutokana na uharibifu wa mazingira unaofanywa na wakazi wa maeneo hayo kila kukicha.," alisema na kuongeza:
"Pia asilimia kubwa ya madaraja hayo yameshuka katika urefu wake wa awali kutokana na mchanga unaosababishwa na mmonyoko wa udongo, hivyo kupunguza sehemu iliyokuwa imekadiriwa kwa maji kupita."
Aliongeza kuwa madaraja na barabara hizo nyingi zilikuwa zimeshakabidhiwa muda mrefu kwa Serikali na kwamba Wizara inaendelea kutafuta suluhu ya kuyarudisha katika hali yake ya kawaida.
Mvua zinazoendelea kunyesha nchini zimeendelea kuharibu miundombinu mbalimbali ya barabara ambapo mawasiliano kati ya Jiji la Dar es Salaam na mikoani yalikatika kutokana na madaraja kuharibika na kufurika maji.
"Tulikuwa na wakati mgumu katika Daraja la Mpiji kutokana na uhaba wa mawe, lakini tayari tumeshapata sehemu ambayo malori yatakuwa yakichukua na kupeleka eneo la ujenzi," alisema Ntemo.
Alisema walifanikiwa kupata mawe eneo la Wazo Hill na viunga vyake ambayo yatasaidia kukamilisha ujenzi wa daraja hilo lililopo Barabara ya Bagamoyo kufikia leo asubuhi au mchana.
Kwa mujibu msemaji huyo, tayari Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Kampuni za Ujenzi za Skol Building Contractors na Estim zinaendelea na ujenzi wa maeneo mbalimbali yaliyoathirika.
Alipoulizwa kuhusu gharama za jumla za uharibifu huo, alisema bado Wizara inaendelea kukusanya taarifa ikizingatiwa kwamba mvua bado zinaendelea kunyesha.
Aliongeza kuwa, Waziri aliagiza madaraja yote kutengenezwa usiku kucha kuhakikisha yanaendelea kuunganisha miji na mitaa kama awali.
"Wanajeshi wanaangalia jinsi ya kuweka daraja la dharura katika Daraja la Mto Kiziga ambalo kalavati liliharibika na pale Kongowe, daraja la Mto Kozi, wanajaza kifusi ili kufungua mawasiliano yaliyokuwa yamesitishwa," alisema.
CHANZO:MWANANCHI

No comments:

Post a Comment