TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Thursday, April 24, 2014

Uamsho: wamtaka Lukuvi athibitishe kauli yake

Khamis-Yusuf-Khamis-April25-2014 57014
Na Hudugu Ng'amilo.
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), maarufu kama Uamsho imemjia juu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ikimtaka athibitishe kauli yake ya kuwahusisha na Chama cha Wananchi (CUF) pamoja na vitendo vya uhalifu visiwani humo.
Uhalifu ambao Lukuvi anadaiwa kuihusisha Uamsho ndani ya Bunge Maalumu la Katiba na kanisani, ni pamoja na kuuawa kwa padri, kuchoma makanisa na uharibifu wa miundombinu Zanzibar.
Kutokana na hali hiyo, Uamsho wamemwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kumtaka ambane Lukuvi athibitishe tuhuma hizo, vinginevyo watatumia sheria kumchukulia hatua.
Nakala ya barua hiyo, ambayo imeambatanishwa na nakala ya DVD inayoonyesha kauli zinazodaiwa kuwa ni za uchochezi wa kidini uliofanywa na Lukuvi, imepelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete; Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein; Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Spika wa Baraza la Wawakilishi na wawakilishi wote.
Nakala ya barua hiyo pia imepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Amiri wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Amiri wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar, Ofisi ya Mufti Zanzibar, Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (Jumaza), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Maimamu wote.
Pia imepelekwa kwa Waziri wa Mipango, Sera na Uratibu wa Bunge, Ofisi ya Spika wa Bunge, Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Kamati ya Maridhiano Zanzibar, vyombo vya habari, Waislamu na wapenda amani wote Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa Uamsho, Sheikh Yusuph Hamis Yusuph, alitangaza tamko la jumuiya hiyo, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema wanapeleka nakala za DVD hiyo kwa Sitta ili awaonyeshe wajumbe wa Bunge hilo jinsi zinavyoonyesha uchochezi wa kidini uliofanywa na Lukuvi ndani ya kanisa na bungeni.
Pia jumuiya hiyo inadai kuwa Lukuvi amekuwa ikidai sera za Uamsho ni sera za chama cha CUF na pia wanapenda sana kufanya vurugu.
Alisema wamelazimika kufunga safari kutoka Zanzibari kwenda Dar es Salaam kuzungumza na waandishi wa habari kutokana na kuchoshwa na maneno, ambayo yamekuwa yakitolewa na Lukuvi katika Bunge hilo dhidi ya Uamsho.
"Lukuvi alitakiwa kuzungumzia jinsi katiba mpya itakavyopatikana na siyo kuzungumzia maneno ambayo hana ushahidi nayo juu ya Uamsho," alisema Sheikh Yusuph.
Alisema kutokana na kitendo cha Lukuvi kuuzungumza maneno machafu na ya uchochezi dhidi ya Uamsho bungeni, wanamuomba Sitta atumie nafasi aliyonayo amwamuru atoe ushahidi wowote anaoujua juu ya jumuiya hiyo.
Sheikh Yusuph alisema kama Lukuvi atashindwa kufanya hivyo, watawasiliana na wanasheria na hatua dhidi yake zitafuatwa.
Alisema pia wanataka kujua kauli ya serikali juu ya kauli ya Lukuvi aliyoitoa katika Kanisa la Methodist Jimbo la Dodoma kuwa iwapo serikali tatu zitakuwapo nchi itachukuliwa na wanajeshi, pia makanisa yote nchini yatafungwa na nchi itakosa amani.
Lukuvi alitoa kauli hiyo katika kanisa hilo wakati wa sherehe za kumtawaza Mchungaji Joseph Bundala kuwa askofu.
Sheikh Yusuph pia alisema Lukuvi hakuishia hapo, bali alienda mbali zaidi kwa kudai kuwa wanaotaka nchi yao Wazanzibari hawawezi kujitegemea, bali wanataka serikali ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa nchi ya Kiislamu na kwamba, Uamsho ni taasisi ya Waislamu wenye msimamo mkali.
"Sisi Jumuiya tuna amini hayo ni maoni ya serikali kwa vile yeye amekwenda kwa niaba ya waziri mkuu. Pia ni msemaji wa wizara na mpaka sasa serikali kwa nini imekaa kimya na hiyo inaonyesha kwamba, inaunga mkono ubaguzi wa dini aliouchochea Lukuvu," alisema.
Alisema mwaka 2004 Jumuiya hiyo ilituhumiwa kuhusika na vurugu zilizotokea Zanzibar, ikiwamo milipuko ya mabomu, kuchomwa makanisa, kuchomwa gari la polisi na kuharibiwa kwa miundombinu.
Sheikh Yusuph alisema kwa matukio hayo, ziliundwa tume mbili kwa ajili ya uchunguzi, lakini mpaka sasa ni miaka 10, matokeo ya uchunguzi huo bado hayajatolewa.
Alisema Uamsho inasikitishwa sana pale viongozi wa dini ya Kiislamu wanapozungumza masuala ya kijamii na kisiasa wanaonekana wametekeleza katiba na uhuru wao wa kujieleza.
Lakini akasema kwa bahati mbaya inapotokea kwa viongozi wa Kiislamu kutoa maoni yao juu ya mambo hayo, hutokea baadhi ya viongozi wa serikali kuwalaumu na kuwatuhumu juu ya uvunjifu wa amani, uchochezi, kuchanganya dini na siasa na kutaka kusababisha vurugu.
Alisema Watanzania wanatakiwa kujionea Lukuvi alivyokwenda kuchanganya dini na siasa kanisani.
Sheikh Yusuph alisema kibaya zaidi Lukuvi alileta uchochezi kati ya Waislamu na Wakristo na kutangaza wazi dhamira ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuwa ni uadui na kuukandamiza Uislamu na Waislamu.
Alisema Uamisho ni taasisi iliyosajiliwa kihalali na SMZ na kwamba, tangu ilipopata usajili, imekuwa ikifanya kazi zake kisheria na haijawahi kupatikana na hatia ya aina yoyote ya uvunjifu wa sheria.
Sheikh Yusuph alisema mbali na hayo, hata viongozi wa Uamsho hawajawahi kupatikana na hatia zaidi ya kufunguliwa kesi, ambazo hadi hazijathibitishwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment