Wajumbe wa Bunge watishiwa maisha
Siku tatu
kabla ya Bunge la Katiba kuanza kupigia kura Rasimu ya Katiba
inayopendekezwa, watu wasiojulikana wameanza kusambaza vitisho vya
kuwatia hofu wajumbe wa Bunge hilo.
Watu hao
wamesambaza vipeperushi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma usiku
wa kuamkia jana, wakiwataka wajumbe kutoingia bungeni vinginevyo
yatakayowapata watajuta, huku wajumbe kutoka Zanzibar wakitishiwa kwa
ujumbe wa simu kupitia mtandao wa WhatsApp.
Tayari,
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd ametoa kauli
kuhusu vitisho hivyo akisema Serikali itachukua kila hatua kuhakikisha
wajumbe kutoka visiwani humo ambao wamekuwa wakipokea vitisho wanakuwa
salama.
Mbali na
kusambazwa kwa karatasi hizo, maandishi mekundu yamechorwa katika kuta
za jengo la Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma yakisomeka, "No Katiba. No
ufisadi."(P.T)
Vikaratasi
vilivyosambazwa vinasomeka: "Onyo. Dodoma si mahali pa kufuga wezi wa
fedha za umma. Utakayeingia bungeni kuanzia kesho (leo), yatakayokupata
utajuta."
Mkazi wa
Dodoma, Sospeter Samwel alimwambia mwandishi wetu jana kuwa aliokota
baadhi ya vipeperushi hivyo jana saa moja asubuhi katika eneo maarufu la
kuuzia magazeti linalotazamana na Jengo la CCM.
"Tulikuta
hayo makaratasi yametupwa tu ovyoovyo ila baadaye nikasikia maeneo
mbalimbali mengine nayo yameonekana yametupwa. Sijui nani hasa watakuwa
wameyasambaza," alisema.
Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa jana kuhusu na
maandishi hayo alijibu kwa kifupi "No comment" (sina cha kusema).
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime jana alitoa taarifa ya maandishi
kwa wanahabari akisema jeshi hilo linawasaka watu waliosambaza
vipeperushi hivyo.
"Wananchi
na wageni wapenda amani waendelee na shughuli zao kama kawaida kwani
polisi tumejiimarisha ipasavyo kukabiliana na yeyote atakayekiuka sheria
na maelekezo yaliyotolewa.
Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi alitoa onyo kwa watu aliodai wanafanya
mzaha akisema vyombo vya usalama viko macho saa 24. Aliwataka wajumbe
kutoa taarifa kwa vyombo vya dola wanapoona viashiria vya kutokuwa na
usalama.
"Kama
ng'ombe mzima tumeshakula tumebakiza mkia tu, niwahakikishie wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba, usalama umekuwapo na utaendelea kuwapo.
Wazanzibari kulindwa
Akizungumzia
vitisho hivyo hasa kwa wajumbe kutoka Zanzibar, Balozi Idd alisema
Serikali itachukua kila hatua kuhakikisha wanakuwa salama.
Alisema
kuna ujumbe unazunguka katika mitandao ya jamii ukitoa vitisho kwa
wajumbe wa Bunge hilo na watumishi wa sekretarieti ya Bunge hilo.
"Vyombo
vya dola vipo na vitafanya kazi yake. Vinajua vitisho vyote.
Niwahakikishie wajumbe mtakuwa salama na Serikali itachukua kila hatua
kuhakikisha hakuna kitakachotokea.
Hoja 17 za Zanzibar
Akizungumzia
kuhusiana hoja 17 ambazo ziliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar, Othman Masoud Othman zenye masilahi ya visiwa hivyo, Balozi
Idd alisema kati yake 13 zilikubalika na kubakia nne.
Hata hivyo, alisema baada ya kuangalia zaidi Rasimu ya Katiba inayopendekezwa waligundua kuwa zilibakia hoja tatu tu.
Alizitaja hoja hizo kuwa ni ibara 86 ambayo inasema Rais wa Jamhuri ya Muungano atashinda kwa kupata kura zaidi ya asilimia 50.
Hata
hivyo, alisema waliona kwenye Katiba ya sasa jambo hilo liko kimya
kidogo endapo itatokea mgombea hakupata kura upande wa Zanzibar.
"Tukaona
kuwa huyu ni Rais wa Muungano, hivi asilimia 50 yote apate Bara
legitimacy (uhalali) yake kama rais wa Muungano iko wapi?" alisema na
kuongeza kuwa vyema katika Rasimu ikaingizwa kuwa mgombea huyo pamoja na
kwamba anatakiwa ashinde kwa zaidi ya asilimia 50, basi angalau katiba
iweke kiwango fulani cha kupata upande wa Zanzibar.
Alisema
baada ya kutafakari ikakubaliwa Zanzibar angalau mgombea huyo apate
asilimia 10 au 15. Hata hivyo, alisema majadiliano kuhusu suala hilo
bado yanaendelea.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment