WACHIMBAJI WADOGO WAISIFIA SERIKALI
Wadau wa
madini ya vito kutoka sehemu mbalimbali duniani, wakipatiwa huduma
katika Banda la Tanzania katika Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na
Usonara – Bangkok, Thailand.
Mfanyabiashara
wa madini ya vito kutoka Tanzania, Latifah Abdallah akitoa maelezo
kuhusu madini hayo kwa wadau waliotembelea Banda la Tanzania katika
Maonesho ya Vito ya Bangkok.
Baadhi ya
Washiriki kutoka Tanzania katika Maonesho ya Vito ya Bangkok wakipozi
kwa picha muda mfupi kabla ya kuanza kwa siku ya tatu ya maonesho hayo.
Kutoka Kushoto ni Asimwe Kafrika, Iddi Pazzi, Gregory Kibusi, Nelson
Magawa, Teddy Goliama na Matiko Sanawa.
Wachimbaji
wadogo na wafanyabiashara wa madini ya vito nchini, wameishukuru na
kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, kwa jitihada
inazofanya za kuwaendeleza na kuwainua kiuchumi.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti katika Maonesho ya Kimataifa ya Vito na Usonara
yanayoendelea jijini Bangkok, nchini Thailand Viongozi waliowawakilisha
wachimbaji wenzao katika maonesho hayo, Gregory Kibusi na Kassim Pazi
walisema Serikali imewapa fursa adhimu kwa kuwawezesha kujionea na
kujifunza zaidi kuhusu sekta hiyo ili waendane na viwango vya kimataifa
na kumudu ushindani wa soko.
“Hatua
iliyochukuliwa na Serikali kuandaa na kuwezesha ushiriki wa wachimbaji
wadogo na wafanyabiashara wa madini ya vito kuja kushiriki maonesho
makubwa kama haya inastahili kupongezwa,” alisema Pazi.
Alifafanua
kuwa ushiriki wa wachimbaji na wafanyabiashara wa vito utawapa fursa
kupanua mtandao na wigo wa biashara kwa kukutana na wadau wa madini hayo
kutoka sehemu mbalimbali duniani na kubadilishana uzoefu katika kazi
hiyo.
Aliongeza
kwamba fursa hiyo pia imewawezesha kutambua aina ya madini ya vito
yaliyo katika soko ili kuwarahisishia kuzalisha madini hayo kwa wingi
badala ya kuzalisha kwa kubahatisha tu hali inayopelekea kukosa soko na
kupata hasara.
“Siku
za nyuma kwa mfano, kuna madini tuliyokuwa tunayatupa tu kwa kudhani
hayana thamani, lakini tumeshangaa kwamba katika maonesho haya, wadau
wengi wanayaulizia. Tumechukua mawasiliano yao ili tukirudi nyumbani
tuwatumie,” alisema Pazi.
Kwa
upande wake, Kibusi alisema ushiriki wao katika maonesho husika umekuwa
wenye tija kwa kiasi kikubwa kwani mbali na kupanua wigo wa mtandao na
soko, pia wameweza kuuza shehena kubwa ya madini kwa bei nzuri.
“Sisi
kama Viongozi, tunawajibika kuhakikisha wachimbaji wenzetu waliobaki
nyumbani wananufaika pia kwa namna moja au nyingine kutokana na ushiriki
wetu katika maonesho haya, hivyo tutahakikisha tunaandaa semina na
kuwashirikisha tuliyoyaona na kujifunza huku,” alisema Kibusi.
Aidha,
alitoa ushauri kwa Serikali kuwapatia nafasi kubwa ya ushiriki
wachimbaji wadogo katika Maonesho ya Vito yanayotarajiwa kufanyika
Arusha mwezi Novemba mwaka huu ili wapate fursa ya kukutana na wadau wao
kutoka sehemu mbalimbali duniani na kujifunza.
Naye
Kiongozi wa Ujumbe wa Watanzania wanaoshiriki katika maonesho hayo
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya
Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), Archard
Kalugendo alitoa wito kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ya
vito kuyatumia maonesho hayo kuboresha kazi na biashara zao.
Alisema,
lengo la Serikali ni kuona madini ya aina zote yakiwamo ya vito na
usonara yanainufaisha nchi na wananchi wake ipasavyo ndiyo sababu
Serikali inatumia njia na mbinu mbalimbali kuwezesha maendeleo hayo.
“Sisi
kama Serikali, tumefungua njia kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa
madini ya vito nchini. Ni vema sasa wakaanza kusimama wenyewe taratibu
ili kuendelea kujifunza na kufanya shughuli zao kwa viwango vya
kimataifa waweze kumudu ushindani wa soko,” alisema Kalugendo.
Aidha,
Kalugendo aliwataka wachimbaji na wafanyabiashara waliopata fursa
kushiriki maonesho ya Bangkok, kuwa mabalozi wazuri ili wawasaidie
wenzao pasipo ubinafsi wala choyo.
Alisema
ni wakati sasa madini ya vito yaingize fedha nyingi katika uchumi wa
nchi na hivyo alitoa changamoto kwa wachimbaji na wafanyabiashara
kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wanatekeleza mikakati
iliyowekwa ya kuhakikisha wadau mbalimbali wa madini ya vito wanakuja
kwa wingi Tanzania badala ya kuwafuata wao nje ya nchi.
“Ifike
mahala tusilazimike kuleta madini yetu Bangkok, bali Wa-Thailand na
mataifa mengine waone umuhimu wa kuja kwetu,” alisisitiza Kalugendo.
Hii
ni mara ya pili kwa Wizara ya Nishati na Madini kupitia TANSORT
kuratibu na kuwezesha ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa
ya Vito na Usonara ya Bangkok ambapo wachimbaji wadogo na
wafanyabiashara wa madini hayo hushirikishwa.
(Awadh Ibrahim).
No comments:
Post a Comment