DR.KHAMIS KINGWANGALLAH ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA URAIS 2015
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya serikali za Mitaa na Mbunge wa jimbo la
Nzega Dr. Khamis Kigwangallah akitangaza nia yake ya kugombea urais
waJamhuri ya Muungano ya Tanzania wakati alipokutana na waandishi wa
habari kwenye ambapo amesema hajasukumwa na mtu yeyote ila ni yeye
mwenyewe ameamua kwa moyo wake.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya serikali za Mitaa na Mbunge wa jimbo la
Nzega Dr. Khamis Kigwangallah akimtambulisha mke wake Dr Bayoum Awadh
wakati wa mkutano huo.
Mzee Nasser SAid Mussa baba mzazi wa Dr. Khamis Kigwangallah na mama yake mzazi Mama Bagaile Lumola.(P.T)
Mzee
Nasser SAid Mussa baba mzazi wa Dr. Khamis Kigwangallah na mama yake
mzazi Mama Bagaile Lumola. na watoto wake Sheila kulia ni Hawa.
Mchungaji Patrick Saso akifanya maombi kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
Sheikh Abubakary Mwita akiomba dua kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
Ndugu viongozi mlioko hapa, wageni waalikwa, wanahabari na watanzania wenzangu mnaonisikiliza;
Ni
heshima kubwa sana kwangu kupata fursa hii. Ni katika nchi chache sana
duniani, mtoto wa maskini kama mimi, aliyewahi kutembea mitaani akiuza
karanga, Big G, maandazi, jerebi na samaki ili kusaidia wazazi kupata
chochote kwa ajili ya kulisha familia anaweza kuota kuwa Rais wa nchi
yake. Kwamba, mtoto aliyeenda shule bila viatu anaweza kuwa Daktari.
Hii
inamaanisha misingi ya haki na usawa kwa wote iliyowekwa na waasisi wa
Taifa hili haikuwa ndoto za alinacha, bali ukweli na uhalisia, na
inafanya kazi. Kwamba, siyo lazima uwe mtoto wa tajiri ndiyo uoneshe
kipaji chako.
Hili peke
yake linanipa sababu ya ziada ya kwa nini nitamani kuota kuwa Rais –
nataka niwe mfano hai wa mafanikio ya Ndoto ya waasisi wa Taifa letu,
kuwa sote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuna haki na fursa
sawa bila kujali nani anatokea familia ipi. Hii ni Tanzania ya ndoto za
waliotutangulia. Ni lazima atokee kiongozi wa kizazi hiki anayetamani
kuiongoza Tanzania itakayodumu kwenye misingi hii:
kwamba
sisi sote ni ndugu, na tuna fursa sawa. Kwamba, kuendelea kimaisha na
kibinafsi ni haki ya binadamu na si hisani. Kwamba, mtoto wa mama ntilie
kama nilivyokuwa mimi hapa, ana haki na fursa ya kuwa mbunge ama Rais
wa nchi, sawa kabisa na mtoto wa Mbunge.
Kwa namna
ya kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza waasisi wa
Taifa letu kwa kusimamia tunu hizi. Niwashukuru pia viongozi wote
walionitangulia kwa kuzilinda, na niahidi nitakuwa wa mwisho kuisaliti
nchi yangu kwenye mambo haya.
Leo
nimefika hapa kwa sababu chama change kina mfumo mzuri ulioasisiwa na
Mwl. Nyerere na umelindwa na Wenyeviti waliomfuatia mpaka na sisi
tumeukuta.
Leo
nimefika hapa kwa sababu Rais Jakaya Kikwete na wajumbe wenzake wa
Kamati Kuu na Halmashauri Kuu walitumia misingi imara iliyowekwa na
waasisi wa Chama changu kuamua kuwa nami nina haki ya kuwa Mbunge. Leo
nazungumza hapa nikiamini kuwa ni misingi hiyo hiyo itatoa uongozi wa
Taifa letu katika awamu ijayo.
Babu
yangu Kizaa Baba aliishi Kijijini Goweko, Mlimani, na alikuwa mfugaji
mkubwa wa ng’ombe na mrina asali mashuhuri. Yeye na mkewe waliishi
maisha ya heshima sana pale kijijini. Hawakuwahi kusoma wala kuajiriwa
japokuwa Babu yangu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama
Cha TANU na baadaye CCM katika ngazi ya Kata.
Babu
yangu na Bibi yangu kizaa mama waliishi Nzega, na ndiyo walionilea baada
ya ndoa ya mama yangu na baba yangu kuvunjika. Walinifundisha mambo
mengi, kubwa likiwa ni kujiamini, pia kufanya mambo yangu kwa bidii,
uadilifu, umakini na kwa nidhamu ya hali ya juu. Bibi yangu huyu
hakusoma shule ya kizungu japokuwa alijifunza kusoma na kuandika. Babu
yangu alikuwa mjukuu wa Chifu na hivyo alipata fursa ya kusoma Tabora
School miaka miwili mbele ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Alifanya kazi mbalimbali chini ya serikali ya wakoloni, na alishiriki
harakati za kuanzishwa na kusambaa kwa chama cha TAA na baadaye TANU.
Babu yangu aliamini kuwa “binadamu wote ni sawa na kwamba kila mtu
anastahili kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”, na kwamba ukoloni
haukuwa kitu cha sawa, na hivyo kujitawala wenyewe dhidi ya wazungu
ilikuwa ni haki yetu; pia aliamini katika elimu, na hivyo alifanya
juhudi kusomesha mabinti zake watatu, mama yangu aliishia kwenye ualimu
kabla ya kuingia kwenye ndoa. Babu aliamini kuwa Tanzania ya mabinti
zake itahitaji wasomi, ndoto ambayo ninaishi kuitekeleza kwa ajili ya
mabinti zangu wawili na Kaka yao, HK Jr.
Japokuwa bibi na babu yangu wameishatangulia mbele ya haki, naamini wananitazama na kutabasamu huko waliko.
Ninaishi
nikiamini kuwa hadithi ya maisha yangu ni mfano hai kwa maisha ya
watanzania wengi. Na kwamba, nina deni la kulipa kwa vizazi vijavyo kwa
kuwa mimi ninafaidi matunda ya mti uliopandwa na vizazi
vilivyonitangulia. Naliona jukumu la kuhakikisha vizazi vijavyo
vinafaidi urithi wa Tanzania kuwa ni la kwangu na wenzangu wa kizazi
hiki.
Kazi
yangu imenifikisha sehemu nyingi sana za nchi yetu – vijijini na kwenye
majiji, imenikutanisha na watu wa kila aina – matajiri kwa maskini,
wazee kwa vijana – hakuna hata mmoja kati ya watu hawa anayetegemea
Serikali itamtatulia kero zake zote. Wanajua wanapaswa kufanya kazi kwa
bidii ili wasonge mbele – na wana nia ya kufanya hivyo.
Nenda kwa
wafanyabiashara wakubwa kule Pugu Road viwandani, kwa watumishi pale
hospitali ya Taifa Muhimbili, ama pale sokoni Kariakoo kwa
wafanyabiashara, wote watakuambia hawapendi kuona kodi zao zikitafunwa
na wachache pale TRA, ama kulipa posho za bure kwa wabunge na mawaziri
kule Bungeni, kulipia mashangingi ya viongozi na watendaji, kulipia
tiketi za ndege daraja la kwanza kwa ajili ya safari za viongozi na
wataalamu wetu kwenda kujifunza kupambana na umaskini wakati wakirudi
wanauacha uzoefu uwanja wa ndege, ama kulipia semina, warsha na
makongamano ya wataalamu ya kuandika sera za MKUKUTA, MKURABITA na
kuandaa bajeti zisizotekelezwa kila mwaka.
Watanzania wanataka kupata huduma bora za afya, elimu, maji, miundombinu.
Nenda
kule kwa watani zangu, Nanyumbu, ama Tandahimba, ama kwa ndugu zangu
kule Nduli, Kyela, wazee kule watakuambia hawategemei Serikali
itawaletea ubwabwa kwenye sahani za fedha, wanajua Serikali
haitowafanyia kila kitu, lakini wanajua kabisa kuwa wanapaswa kufanya
kazi kwa bidii na wamekuwa wakifanya hivyo siku zote.
Wanachohitaji
wao ni kujengewa mazingira wezeshi kushiriki shughuli zao za kilimo ama
biashara, waelekezwe namna ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia njia za
kisasa za kilimo chenye tija na ufanisi, waelekezwe wanapataje pembejeo,
wanapataje mikopo yenye riba nafuu, wanahitaji, mwisho wa siku, wajue
wapi watauza mazao yao kwa uhakika na bila kudhulumiwa wala
kucheleweshewa malipo.
Watu
hawatarajii serikali itabeba mizigo yao yote. Lakini wanaamini kabisa,
kwamba tukibadili kidogo tu vipaumbele vyetu, tukibadili namna
tunavyoendesha serikali, tukibadili kidogo namna tunavyoendesha uchumi
wetu, tutaweza, kwa kiasi kikubwa, kubadili muelekeo mzima wa maisha ya
baadaye ya watoto na wajukuu zetu. Tutatoa uhakika wa kuiondoa nchi yetu
kutoka miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani.
Na mimi,
kama watanzania wenzangu wengi, nina imani kubwa kabisa, kwamba tunaweza
kubadili mustakabali wa Taifa letu. Tunaweza kufungua milango ya maisha
bora zaidi kwa watanzania. Tutatoa fursa sawa kwa kila mtanzania kuishi
kwa matumaini, kwamba atabadili maisha yake wakati wowote ule kuanzia
leo.
Tutaweza
kuamsha ari ya kila mtanzania kuongeza bidii kwenye kazi akitumaini na
kuamini kuwa kesho yake itakuwa bora kuliko jana yake, kuwa naye ataishi
kwa heshima, raha na starehe ndani ya nyumba yake.
Ninaamini,
kutokea ndani kabisa ya mifupa yangu, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa
vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha serikali yetu, haya
ninayoyasema si ndoto za mchana. Ni mambo yanayowezekana.
Watanzania
wengi wanaamini, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu,
mabadiliko makubwa, na ya haraka yatatokea kwenye uchumi wetu. Wanaamini
tukichagua kiongozi sahihi mwakani, anayejua mahitaji ya nchi yetu kwa
sasa na baadaye, tutafanikiwa.
Nyote
mliopo hapa na wanaotusikiliza kutokea nje ya hapa mna jukumu la
kututazama kwa ukaribu sana, kututathmini na kutupima sote;
tuliojitokeza hadharani, walioanza safari za matumaini, wanaotajwa
tajwa, na wale wanaosubiri kuoteshwa ili wakati muafaka ukifika muwape
taarifa sahihi watanzania, kuwa kati yetu sote, ni nani anafaa
kutuongoza kuelekea Tanzania ya ndoto zetu!
Kuwa, ni
nani kati yetu ataweza kuwa Amiri-jeshi-mkuu, siyo kwa uanajeshi wake
bali kwa uwezo na utayari wake wa kuwashirikisha wataalamu wa majeshi na
kuamua kwa busara kutumia nguvu za kijeshi pale inapolazimika baada ya
kupima na kuchambua aina nyingine zote za kutafuta suluhu za migogoro
kabla ya kuamua vita.
Kuwa, ni
nani kati yetu anayeamini katika uhuru, haki na usawa na wajibu wa watu
wote, kama unavyolindwa na Katiba, anayeamini katika haki ya kuabudu
lakini asiyekuwa tayari kuitumia haki hiyo kuwagawa watanzania kutokana
na dini zao.
Kuwa, ni
nani kati yetu anayeamini katika Haki ya kupata huduma bora za afya,
elimu, maji, kama wanavyopata wabunge na mawaziri wetu, kama wanavyopata
mahakimu na majaji wetu, kama wanavyopata wafanyabiashara na
wakurugenzi wetu.
Kuwa, ni
nani kati yetu ataweza kuhakikisha kuwa watanzania wote wanapata haki
hizi bila kutazama hali zao kiuchumi ama daraja zao kijamii.
Kuwa, ni
nani kati yetu anaamini zaidi katika uhuru na kujitegemea kwenye masoko
na malighafi ili kudhibiti uchumi wetu mpana wa ndani, kujitegemea
kwenye masoko ya pamba na nguo, kwenye mafuta ya kula, kwenye chakula
cha uhakika kwa ajili ya watu wetu, kwenye mafuta na gesi ili tukwepe
mtego wa kuwa sehemu ya uchumi, masoko na biashara za hasara na faida za
makampuni makubwa ya kimataifa nje ya mipaka yetu.
Ili
tulinde thamani ya fedha yetu, ili tuwe na uhakika wa ustawi wa maisha
ya watu wetu ndani ya nchi bila athari kubwa kutoka nje ya nchi yetu.
Kuwa, ni
nani miongoni mwetu anaakisi taswira sahihi zaidi ya watanzania walio
wengi, historia yake, rekodi yake, wajihi wake, mtazamo wake, ndoto
zake, zinaakisi ‘utanzania’ halisi. Kuwa, yeye ni hitaji sahihi la
watanzania.
Wakati ukifika, muwaeleze watanzania ukweli, wafanye uamuzi unaotokana na taarifa sahihi, wachague mtu sahihi.
Mimi, Ndugu zangu, natangaza rasmi sasa, kuwa ninatia nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Na
nimefikia uamuzi huu bila kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa, kupangiwa
ama kupanga na mtu ama na kikundi cha watu, bali kwa utashi na utayari
wangu. Na ninayasema haya, haswa baada ya kutafakari mambo mengi kwa
kina:
mahitaji
ya sasa na baadaye ya Tanzania ya ndoto zangu, uwepo wa fursa ya
kugombea na kushinda uchaguzi ujao, uwezo wangu wa kuchambua mambo,
kutafakari, kufanya maamuzi sahihi, kuchukua hatua za utekelezaji na
kusimamia utekelezaji, uadilifu na uzalendo wangu, na zaidi nia yangu ya
kuwa sehemu ya watanzania wengi tunaotaka kuona mapinduzi ya kifikra
katika nchi yetu – mapinduzi ambayo yatatia chachu ya mabadiliko ya
namna tunavyochagua vipaumbele vyetu kama Taifa na namna tunavyosimamia
utekelezaji wa mambo mazuri tunayojipangia kama Taifa.
Ninatangaza
nia ya kugombea Urais nikiwapa fursa watanzania wanipime na kunitazama
mwenendo na uwezo wangu, nikiamini kabisa nitapimwa na kuungwa mkono ama
kutoungwa mkono si kwa rangi ya ngozi yangu, si kwa jinsi yangu, si kwa
umri wangu, na wala si kwa daraja langu kwenye jamii, dini yangu, ama
kabila langu. Ninaamini nitapimwa kwa sifa na uwezo wangu, kama
mtanzania.
Watanzania
tuna sifa moja kubwa; kwenye mambo ya msingi ya kitaifa, tunakubaliana
kuwa maslahi ya Tanzania hupanda juu ya maslahi yetu binafsi. Tudumishe
utanzania wetu.
Ninaamini
katika Ndoto ya Tanzania. Kuwa leo miaka 50 ya kuwa Jamhuri ya Tanzania
tuna kila sababu ya kuwa Taifa la dunia ya kwanza, viongozi
waliotutangulia wameandaa misingi ya kuifikisha Tanzania kwenye
matamanio yetu. Kizazi chetu cha kina jukumu na wajibu wa kuikimbiza
Tanzania kufikia kwenye ahadi inayotokana na ndoto za wazee na waasisi
wa Taifa letu. Binafsi, niko tayari kulibeba jukumu hilo bila woga wala
wasiwasi, maana naamini tusipojitokeza watu kama mimi, tutajikuta
tunaongozwa na watu wasiostahili. Nina suluhu ya changamoto kubwa za leo
na kesho:
kupigana
na njaa na kuhakikisha usalama wa chakula kwa watu wetu, tatizo la
ajira kwa vijana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni
mwa mambo ambayo kizazi chetu kitapaswa kuyafanyia kazi kwa haraka na
umakini wa hali ya juu.
Mimi
ninaamini kwamba, kama hata mimi nimefika hapa, basi kila mtanzania
anaweza, na ana haki ya kufika hapa na kwenda mbele zaidi yangu.
Mafanikio siyo haki ya wachache, ni tunu ya Mwenyezimungu kwa kila mtu.
Ninaamini ni haki ya kila mtanzania kuota ndoto yake, kuifanyia kazi na
kuifikia. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina wajibu wa kutoa fursa kwa
watu wake kuota ndoto zao na kufikia mafanikio bila kukwama.
Na ndugu
watanzania wenzangu, amini nawaambia, kuwa, mbele yetu tuna kazi ya
ziada ya kufanya. Kazi ambayo ninaamini tunaiweza tukiamua; uwezo tunao,
sababu tunazo na nia tunayo – sema tuna mapungufu makubwa kwenye
kuchukua hatua za kutenda.
Mimi naamini kwamba; E Pluribus unum. Baina ya wengi, mmoja!
Kwamba;
Mimi ni mmoja kati ya uwingi wetu. Siwezi kuwa salama kama wengine
hawako salama, siwezi kuwa na raha kama wengine wanateseka. Ninaongozwa
na ile dhana kwamba, matatizo ya mwenzangu, ni ya kwangu, na si yangu
peke yangu, ni yetu sote kama jamii moja.
Hivyo:
- kitisho
cha njaa ya familia fulani maskini kule Sakasaka, wilayani Meatu, ni
kitisho changu na familia yangu, hata kama siyo familia yangu.
- Kucheleweshewa haki ya kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kule Sombetini, ni kitisho kwangu pia, hata kama kesi siyo yangu.
- Mzee
Makame wa kule Wete, Pemba, aliyefiwa na watoto wake akakosa msaada na
yeye hana nguvu za kuzalisha tena, anavyokula mlo mmoja kwa siku ili
asukume siku, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye siyo babu
yangu.
- Mama
John ni mpishi mzuri wa wali nazi kwa maharage, na ana wateja wengi
mtaani kwake maeneo ya Mtaa wa Sikukuu, Sokoni Kariakoo; akifukuzwa,
akapigwa virungu, akanyang’anywa pesa zake, akadhalilishwa na kumwagiwa
chakula chake na mgambo wa jiji la Dar es salaam kwa kuwa anafanya
biashara mahala pasiporuhusiwa, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama
yeye si mama yangu.
- Kama
kuna mtoto asiyejua kusoma na kuandika kule Mrijo Chini kwa watani zangu
warangi, hiyo inaniuma na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si
mwanangu.
- Bwana
Kalumanzila ni mmachinga nguo za mitumba mitaani. Yeye huchukua nguo
zake kumi kwa kuaminiwa na mwenye belo kutokea soko la Karume, akiuza
anachukua kifaida kidogo cha juu kinachozidi hapo juu na kurudisha pesa
ya mwenye mali Karume jioni ya siku hiyo. Elfu mbili ama tatu anayopata
inamfanya aishi yeye na mkewe na watoto wake.
Akifukuzwa
barabarani na akanyang’anywa mali, anakosa kazi ya kufanya na
analazimika kumtumikia bosi mwenye mali mpaka atakapofidia mali
iliyopotea bila kupata cha juu. Shida na madhila anayoyapata bwana
Kalumanzila zinaniumiza na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si
mjomba wangu.
Tarehe 4,
Agosti 2014, Rais Kikwete akihutubia kwenye Kituo cha kimataifa cha
maendeleo (Center for Global Development) alisema: “…Nataka na natamani
kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi masikini.
Raslimali
ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na
umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu
kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri…” Mimi nasema hivi: nataka na
natamani kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kuongoza nchi Tajiri. Kama
nitafanikiwa kuwa Rais, nitatumia miaka ya awali ya uongozi wangu
kuikimbiza Tanzania kuelekea kwenye ndoto hii.
Mungu awabariki. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika.
No comments:
Post a Comment