SITTA APOKEA MESEJI ZA MATUSI  
            
Mwenyekiti
 wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta amesema anapokea meseji za simu zaidi 
ya 50 kwa siku za kumtukana na kusisitiza ataendelea kupambana 
kuhakikisha Katiba inayopendekezwa inapatikana.
Sitta 
alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma jana wakati akielezea 
kutoridhishwa kwake na kile alichodai ni namna hukumu ya kesi 
iliyofunguliwa na Saed Kubenea inavyopotoshwa na wanaomchukia.
"Kuna 
baadhi ya vyombo vya habari wananichukia mimi binafsi. Wasichanganye 
chuki hizo na mchakato wa Bunge Maalumu," alisema Sitta na kuongeza;
"Mimi 
napokea matusi kila siku. Meseji zisizopungua 50 viongozi wa Chadema 
wameweka namba zangu katika tovuti nitukanwe kila siku hilo mimi niko 
tayari na mnaniona niko safi tu wala sihangaiki nalo."
"Lakini 
sasa Bunge Maalumu ni chombo cha kikatiba, kiko tofauti na mwenyekiti 
wake. Huwezi kuliadhibu Bunge Maalumu kwa sababu hupendi sura ya 
mwenyekiti wake," alisema.(P.T)
 
            
Sitta 
alienda mbali zaidi na kusema, "Kwa hiyo wale wanaoendeleza hayo 
mapambano tuendelee na tutaendelea kupambana, lakini kazi ya Bunge 
Maalumu itaendelea na ndugu zangu Watanzania mjue tunaandaa Katiba safi 
na rafiki kwa wananchi na itapatikana."
Sitta 
alisema baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo ya kesi ya Kubenea dhidi ya 
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kumekuwa na tafsiri alizosema ni 
potofu.
Baada ya maelezo hayo alimpa ruksa AG, Jaji Frederick Werema kutoa ufafanuzi.
Jaji 
Werema alisema Mahakama Kuu, katika kutafsiri kifungu cha 25(1) (2) 
inakiri kwamba kuna tofauti kati ya kifungu kilichoandikwa Kiswahili na 
kile kilichoandikwa Kiingereza.
Alisema 
Mahakama Kuu katika hukumu hiyo imesema mamlaka ya kuandika Katiba Mpya 
ina maana ni mamlaka ya kuandika na kupitisha katiba inayopendekezwa kwa
 ajili ya kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.
Takukuru yalitesa Bunge
Wakati 
hayo yakiendelea suala la kuingizwa ama kutoingizwa kwenye katiba, 
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), linaonekana 
kulitesa Bunge la Katiba baada ya kamati 10 kati ya 12 kulirejesha tena 
jana.
Rasimu 
iliyowasilishwa bungeni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ililiacha suala
 hilo kwa maelezo kuwa siyo moja ya mambo ya Muungano na msimamo huo 
ukaungwa mkono na Kamati ya Uandishi ya Bunge hilo.
Chanzo:Mwananchi