WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA AKAGUA ATHARI ZA MAFURIKO MKOANI DODOMA
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitazama sehemu ya jengo la Kituo cha
Polisi cha kijiji cha Chipogoro wilayani Mpwapwa ambayo imeporomoka
kufuatia mafuriko yaliyokikumba kijiji hicho kufuatia mvua kubwa
zianazoendelea kunyesha mkoani Dodoma januari 17, 2014. Kulia kwake ni
Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dr. Rehema Nchimbi.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikagua athari za mafuriko yaliyokikumba
kijiji cha Chipogoro wilayani Mpwapwa Januari 17, 2014. Kulia kwake ni
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na Mbunge wa Mpwapwa, Gregory Tewu
na kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dr. Rehema Nchimbi.
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akikagua daraja ambalo lilizibwa na maporomoko ya maji yaliyoambatana na magogo , mawe na udongo na kusababisha mafuriko katika kijiji cha Chipogoro wilayani Mpwapwa januari 17,20134.(P.T)
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akikagua daraja ambalo lilizibwa na maporomoko ya maji yaliyoambatana na magogo , mawe na udongo na kusababisha mafuriko katika kijiji cha Chipogoro wilayani Mpwapwa januari 17,20134.(P.T)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikagua
athari za mafuriko katika kijiji cha Fufu wilayani Chamwino, Dodoma,
Januari 17, 2014.Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rehema nchimbi na
kulia kwake ni Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
ametembelea vijiji vya Chipogoro na Fufu katika wilaya za Mpwapwa na
Chamwino, mkoani Dodoma na kukagua maeneo mbalimbali ambayo yaliathiriwa
na mafuriko kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kati ya Januari 2 hadi
Januari 11, mwaka huu.
Akiwa katika kijiji cha Chipogoro
tarafa ya Rubi, Waziri Mkuu alikagua kituo cha polisi na nyumba
zilizobomolewa, choo cha zahanati na kukagua eneo la barabara
inayojengwa ya kutoka Dodoma hadi Iringa katika eneo lenye matatizo ya
makaravati kuziba.
Kwenye kijiji cha Fufu katika
tarafa ya Makangwa ambacho kiko umbali wa kilometa 30 kutoka Chipogoro,
Waziri Mkuu alikagua maeneo ya makazi yaliyoathiriwa kwa mafuriko na
kukagua baadhi ya nyumba zilizobomoka kabla ya kuzungumza na wananchi na
kuwapa pole.
Akizungumza na wakazi wa vijiji
hivyo leo (Ijumaa, Januari 17, 2014), mara baada ya kupokea taarifa za
maafa ya mafuriko hayo, Waziri Mkuu alimtaka Meneja wa TANROADS mkoa wa
Dodoma, Eng. Leonard Chimagu kuhakikisha anasimamia wakandarasi wa
barabara hiyo ambayo ujenzi wake bado haujakamilika na kuainisha maeneo
korofi ili yafanyiwe marekebisho haraka.
“Nimekagua matundu katika daraja
moja pale Chipogoro na kuona ni madogo, mtaalamu anasema uchafu ulioziba
ndiyo umesababisha maji yasipite. Mimi si mhandisi na hizi ni mvua za
kwanza tu, sasa yakija maji mengi zaidi ya haya hali itakuwaje?, alihoji
Waziri Mkuu.
“Hata hapa Fufu, kuna mahali
nimeona maji yanaonyesha yalikuja kwa kasi kubwa lakini upenyo wa
kuingia kwenye makaravati na kutokea upande wa pili ni mdogo sana...
barabara hii ni mkombozi lakini kama haitazingatia uhalisia wa maeneo
itakuwa ni balaa,” alionya.
Alimtaka pia awasimamie wakandarasi
hao ili wanapoweka matoleo ya maji wahakikishe upande wa pili barabara
maji hayo yanakwenda kwenye mikondo ya mto na siyo kuyaacha tu yasambae
kiholela na kuishia kwenye makazi ya watu au mashamba yao.
Waziri Mkuu aliahidi kutoa mifuko
ya saruji 2,600 na mabati 1,560 ambapo kila kijiji kitapata mifuko 1,300
na mabati 780 ili kuwasaidia wakazi waliobomolewa nyumba zao waweze
kujenga nyumba za kisasa.
Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Dk. Rehema Nchimbi kuwashirikisha wadau wengine katika mkoa huo ili
waone wanawezaje kuchangia upatikanaji wa mabati mengi zaidi kwa ajili
ya nyumba zilizoezuliwa.
Kuhusu chakula cha msaada, Waziri
Mkuu alimtaka Dk. Nchimbi aandae makisio ya mahitaji ya chakula yaliyopo
na kuyafikisha Ofisi ya Waziri Mkuu ambako kuna Idara inayosimamia
maafa ili waletewe chakula hicho haraka kwa sababu kipo.
Alisema anakubaliana na ushauri
uliotolewa kuhusu suala la ujenzi wa mabwawa ya kukinga maji ya mvua ili
kupunguza kasi ya maji yanayoporomoka kutoka milimani lakini akasema
Serikali imeanza na ujenzi wa Bwawa la Kidete lililoko wilayani Kilosa
tangu yaliyopotokea mafuriko wilayani humo.
Mapema, akitoa taarifa kwa Waziri
Mkuu, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Bw. Alfred Msovella, alisema
nyumba 129 zilibomoka, vyoo 78 vimebomoka kikiwemo cha zahanati ambapo
wakazi 1,390 wamepoteza vifaa mbalimbali ikiwemo vyakula, magodoro,
vyombo vya ndani na mifugo.
Bw. Msovella ambaye pia ni Mkuu wa
Wilaya ya Kongwa alisema hivi sasa, wakazi hao wanahitaji mahema 400,
magodoro 381, madaftari ya wanafunzi na dawa za matibabu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chamwino,
Bi. Fatma Salum Ally akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu kwenye mkutano
wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Fufu, alisema
jumla ya nyumba 26 zilibomolewa na mali kama vyakula, samani, vyombo vya
nyumbani na bidhaa za biashara kuharibika.
Alisema eneo la kijiji cha Fufu ni
tambarare na liko chini ya safu za milima na maji ya mvua yanayoporoka
kutoka milimani, huondoka polepole. “Hata hivyo, hali hii ya mafuriko
imechochewa na ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha lami ambapo tuta
la barabara mpya na vidaraja vidogo vilivyowekwa vimekuwa kizuizi cha
maji mengi yanayotoka milimani na hivyo kuongeza tatizo la mafuriko,”
alisema.
Mikutano hiyo ilihudhuriwa na Naibu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw. Gregory Teu ambaye pia ni mbunge wa
Mpwapwa pamoja na mbunge wa Mtera, Bw. Livingstone Lusinde.
No comments:
Post a Comment