TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Thursday, January 30, 2014

TANZANIA YAZIDI KUNG'ARA KIMATAIFA 

Mwakyembe_accb2.jpg
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
TANZANIA imeendelea kupata miradi mikubwa ya maendeleo ya kimataifa, ambapo sasa imeibuka kuwa mshindi kimataifa na kukubaliwa kuanzisha mradi mkubwa wa Kanda ya Kati wa Uchukuzi. Mradi huo utakaohusisha miundombinu ya reli, barabara na bandari unatarajiwa kuanza kutekelezwa wakati wowote nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alisema mradi huo ulishinda miradi 51 ya nchi zingine za Afrika katika mkutano wa Uchumi wa Dunia (WEF) uliofanyika Januari 22 jijini Davos, Uswisi.
Kabla ya ushindi huo, mradi huo uliingia kwenye miradi 16 bora kati ya 51 ya Afrika na kushindanishwa katika mkutano huo uliohudhuriwa na nchi kubwa kiuchumi, kampuni za kimataifa na mashirika makubwa ya fedha duniani.
“Kwa kweli ilikuwa neema na furaha kubwa kwa Tanzania kupewa heshima hii, kwani miradi mingine 16 iliyowasilishwa katika mkutano huo nayo ilikuwa na sifa nzuri, lakini mradi huu wa Kanda ya Kati ambao takribani asilimia 95 ya utekelezwaji wake itanufaisha Tanzania, ulionekana bora zaidi,” alisema Dk Mwakyembe.
Kutokana na ushindi huo, Dk Mwakyembe alimwomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aunde Tume maalumu ya kitaifa, itakayosimamia na kushughulikia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo, ili uwe wa mfano Afrika na duniani kote.
Sifa zilizochangia mradi huo kutangazwa mshindi kati ya miradi bora 16 ya Afrika na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, ni pamoja na mikakati iliyowekwa na Serikali ya Tanzania chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ya kuendeleza Ukanda wa Kati wa Uchukuzi.
Nyingine ni dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania iliyoonekana, pamoja na mfumo iliyojiwekea katika utekelezaji wa mradi huo unaolenga kupanua bandari za Tanzania na kufungua zaidi milango ya kiuchumi kwa nchi jirani.
Alipopewa nafasi ya kuzungumza baada ya mradi huo kutangazwa kushinda katika mkutano huo, Mwakyembe alishukuru washiriki wa kila pembe ya dunia, kwa kuiamini Tanzania na kuelezea mikakati ya utekelezaji wa mradi huo ambapo hata hivyo alibainisha upungufu wa fedha uliopo.
Alisema baada ya kuelezea changamoto zilizopo katika hotuba yake, Brown alimtaarifu kuwa mwaka huu viongozi wakuu wa nchi duniani, watakutana Abuja, Nigeria, kupokea tathmini ya utekelezaji wa mradi huo ambapo pia itafanyika warsha ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi mwanzoni mwa Aprili nchini.
“Tuna mpango wa kumwomba Rais Jakaya Kikwete awe mgeni rasmi katika ufunguzi wa warsha hii, ili tuuthibitishie ulimwengu utayari wa Tanzania kuleta mapinduzi katika sekta ya uchukuzi,” alisisitiza Dk Mwakyembe.
Aidha, alisema kupitia warsha hiyo, Tanzania imejipanga kuionesha dunia kuwa na mipango mizuri na ndiyo maana akaombwa Waziri Mkuu aunde Tume itakayofanya kazi kwa saa 24 kusimamia utekelezaji wa mradi huo.
Alisema alipendekeza tume hiyo ya watu wanane ihusishe wataalamu kutoka wizara za Uchukuzi, Ujenzi, Fedha, Shirika la Reli Tanzania (TRL) na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mradi huo kwa Tanzania utagusa Bandari ya Dar es Salaam, maeneo ya Mashariki, Magharibi na Kaskazini mwa nchi na utahusisha nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Burundi.
Miradi mingine Mradi huo mkubwa ni kielelezo kingine cha heshima ya Tanzania kimataifa, ambapo mwaka jana wakati wa ziara ya Rais wa Marekani nchini, Barrack Obama, nchi ilipata heshima nyingine ya kutekeleza mradi mkubwa wa umeme unaojulikana kama ‘Power Africa’, utakaoinufaisha nchi na kuwa kitovu cha uzalishaji wa nishati hiyo.
Katika mradi huo unaowezeshwa na Marekani kwa kushirikisha Serikali na sekta binafsi, una lengo la kuiwezesha nchi kuongeza kiwango cha uzalishaji sambamba na kupata umeme wa uhakika, utakoongeza ajira. Serikali ya Marekani ilitoa dola bilioni 7 kusaidia kupatikana megawati 10,000 za nishati hiyo, huku sekta binafsi ikitoa dola bilioni 9.
Moja ya kampuni kubwa zinazohusika na mpango huo ni General Electric (GE), ambayo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mradi unaendelea kwa kuahidi kutoa megawati 5,000 kwa gharama za kawaida kwa Tanzania na Ghana.
CHANZO:HABARILEO

No comments:

Post a Comment