RIBERY AWAPONDA FIFA KUMPA RONALDO BALLON D'OR
NYOTA wa Bayern Munich, Franck Ribery
ameuponda mfumo wa upigaji kura za kuchagua Mwanasoka Bora wa Dunia wa
FIFA, Ballon d'Or na kusema alistahili zaidi kushinda tuzo hiyo kuliko
Cristiano Ronaldo, kwa sababu alishinda mataji matano mwaka 2013, wakati
mpinzani wake wa Real Madrid hakushinda chochote.
Mfaransa huyo alikubali kushika nafasi ya tatu nyuma ya mshindi, Ronaldo na Lionel Messi aliyekuwa wa pili katika sherehe za tuzo zilizofanyika mjini Zurich, Uswisi Jumatatu iliyopita na pia amesema tuzo binafsi si muhimu kwake.
Ribery alitwaa mataji ya Bundesliga,
Kombe la Ujerumani, Ligi ya Mabingwa, Super Cup ya UEFA na Klabu Bingwa
ya Dunia akiwa na Bayern mwaka 2013.
Nyota huyo wa Ufaransa pia alisema
kwamba yalifanyika mabadiliko katika mfumo wa upigaji kura mwaka huu
kumsaidia Ronaldo, kwa kuongeza muda wa kupiga kura wakati nyota huyo wa
Ureno alikuwa kwenye mazingira ya kuiwezesha nchi yake kuitoa Sweden
katika kinyang'anyiro cha tiketi ya Kombe la Dunia.
Tarehe ya mwisho ya kupiga kura
ilisogezwa mbele kwa wiki mbili. Hii haikuwahi kutokea kabla. Haikuwa
kwa ajili ya soka. Ulikuwa uamuzi wa kisiasa,"aliponda Ribbery.
Hasira zake hazikuishia kwenye tuzo hiyo tu, bali pia uteuzi wa kikosi bora cha wachezaji 11 wa FIFA wa mwaka- kuhusisha wachezaji watatu tu wa Bundesliga, licha ya Fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2013 kuzikutanisha Bayern na Borussia Dortmund. Chanzo: binzubeiry
No comments:
Post a Comment