Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
TANZANIA
imeendelea kupata miradi mikubwa ya maendeleo ya kimataifa, ambapo sasa
imeibuka kuwa mshindi kimataifa na kukubaliwa kuanzisha mradi mkubwa wa
Kanda ya Kati wa Uchukuzi. Mradi huo utakaohusisha miundombinu ya reli,
barabara na bandari unatarajiwa kuanza kutekelezwa wakati wowote nchini.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe, alisema mradi huo ulishinda miradi 51 ya nchi
zingine za Afrika katika mkutano wa Uchumi wa Dunia (WEF) uliofanyika
Januari 22 jijini Davos, Uswisi.
Kabla ya
ushindi huo, mradi huo uliingia kwenye miradi 16 bora kati ya 51 ya
Afrika na kushindanishwa katika mkutano huo uliohudhuriwa na nchi kubwa
kiuchumi, kampuni za kimataifa na mashirika makubwa ya fedha duniani.
“Kwa
kweli ilikuwa neema na furaha kubwa kwa Tanzania kupewa heshima hii,
kwani miradi mingine 16 iliyowasilishwa katika mkutano huo nayo ilikuwa
na sifa nzuri, lakini mradi huu wa Kanda ya Kati ambao takribani
asilimia 95 ya utekelezwaji wake itanufaisha Tanzania, ulionekana bora
zaidi,” alisema Dk Mwakyembe.
Kutokana
na ushindi huo, Dk Mwakyembe alimwomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aunde
Tume maalumu ya kitaifa, itakayosimamia na kushughulikia kikamilifu
utekelezaji wa mradi huo, ili uwe wa mfano Afrika na duniani kote.
Sifa
zilizochangia mradi huo kutangazwa mshindi kati ya miradi bora 16 ya
Afrika na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, ni pamoja na
mikakati iliyowekwa na Serikali ya Tanzania chini ya Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN) ya kuendeleza Ukanda wa Kati wa Uchukuzi.
Nyingine
ni dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania iliyoonekana, pamoja na
mfumo iliyojiwekea katika utekelezaji wa mradi huo unaolenga kupanua
bandari za Tanzania na kufungua zaidi milango ya kiuchumi kwa nchi
jirani.
Alipopewa
nafasi ya kuzungumza baada ya mradi huo kutangazwa kushinda katika
mkutano huo, Mwakyembe alishukuru washiriki wa kila pembe ya dunia, kwa
kuiamini Tanzania na kuelezea mikakati ya utekelezaji wa mradi huo
ambapo hata hivyo alibainisha upungufu wa fedha uliopo.
Alisema
baada ya kuelezea changamoto zilizopo katika hotuba yake, Brown
alimtaarifu kuwa mwaka huu viongozi wakuu wa nchi duniani, watakutana
Abuja, Nigeria, kupokea tathmini ya utekelezaji wa mradi huo ambapo pia
itafanyika warsha ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi mwanzoni mwa
Aprili nchini.
“Tuna
mpango wa kumwomba Rais Jakaya Kikwete awe mgeni rasmi katika ufunguzi
wa warsha hii, ili tuuthibitishie ulimwengu utayari wa Tanzania kuleta
mapinduzi katika sekta ya uchukuzi,” alisisitiza Dk Mwakyembe.
Aidha,
alisema kupitia warsha hiyo, Tanzania imejipanga kuionesha dunia kuwa na
mipango mizuri na ndiyo maana akaombwa Waziri Mkuu aunde Tume
itakayofanya kazi kwa saa 24 kusimamia utekelezaji wa mradi huo.
Alisema
alipendekeza tume hiyo ya watu wanane ihusishe wataalamu kutoka wizara
za Uchukuzi, Ujenzi, Fedha, Shirika la Reli Tanzania (TRL) na Ofisi ya
Waziri Mkuu.
Mradi huo
kwa Tanzania utagusa Bandari ya Dar es Salaam, maeneo ya Mashariki,
Magharibi na Kaskazini mwa nchi na utahusisha nchi za Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Burundi.
Miradi
mingine Mradi huo mkubwa ni kielelezo kingine cha heshima ya Tanzania
kimataifa, ambapo mwaka jana wakati wa ziara ya Rais wa Marekani nchini,
Barrack Obama, nchi ilipata heshima nyingine ya kutekeleza mradi mkubwa
wa umeme unaojulikana kama ‘Power Africa’, utakaoinufaisha nchi na kuwa
kitovu cha uzalishaji wa nishati hiyo.
Katika
mradi huo unaowezeshwa na Marekani kwa kushirikisha Serikali na sekta
binafsi, una lengo la kuiwezesha nchi kuongeza kiwango cha uzalishaji
sambamba na kupata umeme wa uhakika, utakoongeza ajira. Serikali ya
Marekani ilitoa dola bilioni 7 kusaidia kupatikana megawati 10,000 za
nishati hiyo, huku sekta binafsi ikitoa dola bilioni 9.
Moja ya
kampuni kubwa zinazohusika na mpango huo ni General Electric (GE),
ambayo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mradi unaendelea kwa kuahidi
kutoa megawati 5,000 kwa gharama za kawaida kwa Tanzania na Ghana.
CHANZO:HABARILEO