ALIUZA FIGO KWA KUVUNGWA KUWA INGEOTA NYINGINE
Katika mitaa ya Jiji la Kathmandu, nchini Nepal kukutana na watu wakiomba msaada wa matibabu ya figo ni jambo la kawaida.
Duniani
kote, tatizo la figo siyo jambo geni masikioni mwa watu. Wapo wengi
wanaosubiri kubadilisha na wengine kupata matibabu ya kawaida.
Hata
hivyo, kwa Nepal ni habari nyingine kabisa. Siyo kwamba watu hawa
wanataka kubadilishwa figo kama wale wengine duniani ambao wana matatizo
ya kawaida. Hawa hawana kwa sababu walirubuniwa na zikachukuliwa bila
wao kujua.
Hivi sasa
wanaugua magonjwa mbalimbali kwa sababu hawana uwezo wa kugharimia
matibabu ya figo (dialysis) kutokana na umaskini uliotopea.(P.T)
Inakadiriwa
kuwa watu wapatao 300 katika kipindi cha miaka mitano, wameingia katika
mtego wa wafanyabiashara wa figo na wamezitoa bila wao kujua.
Mwathirika
wa biashara hiyo, Nawaraj Pariyar anasimulia jinsi alivyodanganywa kuwa
nyama wanayoitoa tumboni mwake ingeota tena bila kujua kinachotolewa ni
figo.
Kama
walivyo wakazi wengi nchini humo, Pariyar naye alikuwa akiishi kwa
kutegemea biashara ya maziwa kutoka katika ng'ombe wawili anaowamiliki.
Pariyar
ni maskini ambaye hakwenda shule hata darasa moja, mbali na kumiliki
ng'ombe hao. Analo shamba dogo ambalo halimtoshelezi kulima mazao
yatakayompa chakula cha angalau kwa miezi sita.
Katika kujiongezea kipato, alikuwa akienda mji mkuu wa nchi hiyo, Kathmandu kutafuta vibarua vya ujenzi.
Akiwa
katika moja ya vibarua hivyo mwaka 2005, kiongozi wa ujenzi katika jengo
alilokuwa akifanya kibarua alimfuata kumpa 'mchongo' ambao ungemfanya
apate chapchap Dola 30,000 za Kimarekani 30,000.
"Aliniambia
kuna kipande cha nyama kitatolewa tumboni nami nitapewa kiasi hicho cha
pesa. Nilipotaka kuhoji zaidi aliniambia nisiwe na wasiwasi kwani
kipande hicho kitaota tena baada ya muda," anasema Pariyar.
"Nilifikiria kama nyama itaota tena kwa nini nisikubali tena ninapata pesa nyingi kiasi hicho."
Anasema
kabla ya kukubaliana naye alimuuliza itakuaje kama atakufa wakati wa
kuitoa nyama hiyo, lakini alimhakikishia kuwa itatolewa na wataalamu
waliobobea hivyo asiwe na wasiwasi.
Anasema
maisha yalibadilika kuanzia pale alipokubali kwani alipewa nguo nzuri na
chakula. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake alipelekwa katika jumba
la sinema.
Wahalifu hao walimpeleka katika hospitali moja nchini India katika mji wa Chennai.
"Tulipofika
hospitali daktari aliniuliza kama nina undugu na mgonjwa, nilikubali
kwa kuwa ndivyo nilivyoambiwa niseme," anasema Pariyar.
"Nilisikia mara kadhaa wakisema kidney (figo) lakini sikuelewa kwa sababu katika lugha yetu huwa inaitwa mirgaula," anaongeza.
Anasema kama angejua kama kinachozungumziwa ni figo, asingekubali kuendelea na zoezi hilo.
Baada ya
kutolewa figo, Pariyar aliondolewa na kurudishwa kwao huku akiambulia
Rupee 20,000 tu ambazo hazifikii hata robo ya makubaliano yao.
"Baada ya
muda nilipata wasiwasi. Nikaamua kurudi kwa daktari kuulizia kwa sababu
hata wale watu sikuwaona tena, ndipo nilipogundua kuwa figo yangu
imechukuliwa," anasema Pariyar.
Hivi sasa Pariyar anaugua mara kwa mara. Ana matatizo katika mkojo na mgongo unamuuma mara kwa mara.
"Najua
nitakufa hivi karibuni. Natumaini nikifa leo Serikali itanisaidia
kuwatunza watoto wangu wawili. Sijui kama nitakufa leo au kesho lakini
siku zangu zinahesabika," anamalizia.
Wito wake kwa serikali ya nchi hiyo ni kuwaelimisha wananchi wake ili wasirubuniwe kwa sababu ya umaskini wao na kukosa elimu.
Kwa mwaka jana pekee, watu 10 walikamatwa katika majaribio ya kutaka kuwasafirisha watu ili wakawatoe figo na kuziuza.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment