ZITTO: UBUNGE SASA BASI!
Zitto Kabwe |
Na: Frank Sanga na Anthony Kayanda, Kigoma, MWANANCHI.
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amesema hana mpango wa kugombea ubunge mwaka 2015 badala yake anajipanga kuwania urais. Zitto alisema hayo jana alipozungumza na wananchi katika mjadala ulioandaliwa na asasi ya kiraia ya Meza ya Duara uliokuwa unafanyika maeneo ya Soko la Mwanga, mjini Kigoma. Zaidi ya watu 200, ambao walihudhuria katika mjadala huo wa wazi walimuuliza maswali mbalimbali mbunge huyo, huku mmoja akigusia kuhusu tetesi za mara kwamba Zitto anataka kugombea urais katika uchaguzi ujao.
“Nimefanya
kazi kubwa katika kazi yangu ya ubunge, nimeleta mabadiliko mengi
kuanzia bungeni mpaka jimboni. Nadhani inatosha na hata nikiongezewa
miaka mingine sitaweza kufanya yale yaliyonishinda katika kipindi cha
miaka kumi.
“Kama Mungu ataniweka mpaka mwaka 2015, sitagombea ubunge tena kwa
sababu kazi niliyofanya inatosha. Natangaza rasmi kuwa nitagombea urais
kupitia chama changu cha Chadema, bila kusababisha msuguano wowote na
sitaki kuingia katika historia ya kurudisha nyuma harakati za upinzani
kushika dola,” alisema Zitto.
“Nataka
kuleta changamoto mpya, nitawaeleza watu wa chama changu nia hiyo na
nitatoa hoja za msingi. Hata kama sitapata ridhaa yao, lakini huo ndio
msimamo wangu.
“Iwapo chama kikiona sistahili au sifai, nitakubaliana na uamuzi huo.
Watu wengi wanadhani urais ni cheo, hawajui kuwa ni nafasi ambayo
inakufanya ufanye vitu ambavyo ni vikubwa na vya maendeleo kwa
wananchi.”
Atangaza kugombea urais
Katika hatua nyingine Zitto alisema ana mpango wa kuwania urais kupitia
Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Kwanza nataka niwahakikishia watu wa Kigoma msiwe wanyonge…mna uwezo wa
kutoa rais wa nchi hii,” Zitto alianza kujibu swali hilo na kuendelea.
Hata
hivyo Zitto alipoulizwa baadaye na Mwananchi kuwa mwaka 2015 atakuwa na
miaka 39, hivyo kukosa sifa ya kugombea urais kwa mujibu wa katiba
alijibu; “Nadhani nina uwezo wa kuwa rais, sidhani kama Katiba inaweza
kumzuia mtu mwenye uwezo asigombee na ndio maana ninaamini kuwa
kipengele cha kuwa na miaka 40 kitabadilishwa katika katiba mpya.”
“Nchi
za Kidemokrasia lazima vyama vibadilishane utawala wa kuongoza nchi
kama ilivyo katika nchi za Ghana na Zambia. Tanzania inatakiwa kuiga
mfano wa nchi hizo,” alisema Zitto
Katika kukazia hilo, Zitto alisema anashangazwa na umaskini uliopo
Tanzania wakati mwaka 1976 uchumi wake ulikuwa sawa na nchi ya Malaysia,
lakini mpaka kufikia mwaka 2001, Malaysia ilipunguza idadi ya watu
wanaoishi chini ya dola moja kutoka asilimia 56 mpaka kufikia asilimia
tatu huku Tanzania ikipunguza kutoka 51 mpaka 46.
Katika hatua nyingine, Zitto alikana kuwa, Chadema ni chama cha udini,
ukanda, ukabila ila akasisitiza kuwa ni chama cha kitaifa.
“Ndugu
zangu naomba mnielewe, Chadema si chama cha ukabila, ukanda wala udini
bali ni chama cha kitaifa. Hizo ni propaganda za wapinzani wetu,”
alisema Zitto baada ya kuulizwa na mmoja wa washiriki kuhusu tuhuma za
chama hicho kuwa cha Kikanda.
“CCM
imewahi kudai CUF ni chama cha Waislamu, na sasa wanasema Chadema ni
chama cha Wakristo, sasa wao CCM ni chama cha wapagani au cha watu
gani?” Alihoji Zitto.
Alisema ili kuthibitisha kuwa Chadema si chama cha Kikanda, matokeo ya
urais wa mwaka 2010, Dk Wilbroad Slaa aliongoza dhidi ya wagombea urais
wengine kwa kupata kura nyingi katika Jimbo la Manyovu mkoani Kigoma na
hivyo kufanya kupata asilimia nyingi kuliko sehemu yoyote Tanzania.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari
No comments:
Post a Comment