MKUTANO JUU YA SERA YA KUDHIBITI POMBE KUFANYIKA TANZANIA
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi |
MKUTANO wa Kimataifa kujadili umuhimu wa nchi za Afrika Mashariki kuwa na sera ya kudhibiti ulevi unaanza Arusha kesho. Mkutano huo wa siku mbili utakaofanyika katika hoteli ya Naura Springs utahudhuriwa na watu 80 ambao kwa namna moja au nyingine kazi zao zinaguswa na madhara ya ulevi. Mkutano huo wenye kauli mbiu “Ulevi ni matatizo chukua hatua sasa” utafunguliwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi.
Balozi wa Sweden nchini Dk. Lennrth Hjelmaker atatoa mada kuu kuhusu madhara ya ulevi na jinsi ya kuwa na umuhimu wa kuwa na sera ya kudhibiti matumizi mabaya ya pombe. Ulevi una madhara makubwa kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuchochea migogoro majumbani na kusababisha ajali zinazouwa watu wengi na kuacha wengine vilema. Washiriki wa mkutano huo wanatoka nchi za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi, Sweden, Norway na Tanzania.
Mada zitakazowasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na zile zitakazojadili hatua zilizofikiwa na nchi za Afrika Mashariki katika kuweka sera ya kudhibiti vilevi. Mwakilishi wa Malawi ambaye nchi yake imechukua hatua kutunga sera ya kudhibiti ulevi atawasilisha mada kuzungumzia fursa na changamoto zake. Siku ya pili mkutano huo utafanya warsha nne ambazo zitazungumzia mada mbalimbali zote zikilenga kuelimisha na kuhamasisha washiriki kuona umuhimu wa nchi za Afrika Mashariki kuwa na sera ya kudhibiti ulevi.
Mkutano huo umeandaliwa na Shirika la Kimataifa lisilokuwa la Kiserikali IOGT ambalo linahamasisha maendeleo kwa kushirikiana na mashirika mengine ya kijamii Afrika ya Mashariki. Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani hapa nchini Dk. Neema Kileo na mwakilishi IOGT katika ngazi ya kimataifa Kristina Sperkova watatoa ujumbe maalum kwenye mkutano huo. Mkutano huo utafungwa rasmi na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Dk. Richard Sezibera.
Chanzo: http://www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment