CHADEMA YAKATAA KUKUTANA NA KAMATI YA NCHIMBI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KATIKA
kusimamia
uongozi unaozingatia misingi muhimu ya haki za binadamu, sheria na
utawala bora, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesisitiza
msimamo wake wa kutotoa ushirikiano kwa kamati iliyoundwa na Waziri wa
Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi kuchunguza kifo cha Mwandishi wa Habari
wa Channel ten, Daudi Mwangosi, kilichotokea Septemba 2, 2012, Kijiji
cha Nyololo, mkoani Iringa.
Msisitizo huo umekuja baada ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo kukiandikia
barua (isiyokuwa na Kumbukumbu Namba) CHADEMA, akiomba kamati yake
ikutane na viongozi wa chama Septemba 25, ili kutafakari tukio hilo na
matukio ya aina hiyo yaliyowahi kutokea hapa nchini.
Itakumbukwa
kuwa Marehemu Mwangosi aliuwawa na Jeshi la Polisi akiwajibika kwa
jamii katika shughuli za uandishi wa habari, wakati askari wa jeshi hilo
walipovamia ofisi za CHADEMA Kata ya Nyololo na kuanzisha vurugu wakati
wanachama walipokuwa wakiendelea na shughuli halali za ndani za chama.
Katika barua kwenda kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, CHADEMA kimesema wazi
kuwa hakiko tayari kukaa na kutafakari juu ya kifo cha Mwangosi kama
ilivyopendekezwa na kamati hiyo, kwani imeundwa kinyume cha sheria, huku
pia ikiwa imeundwa na mtu ambaye kanuni za msingi za utawala bora,
zinamtaka awe amejiuzulu au kufukuzwa kazi, kupisha uchunguzi huru juu
ya mauaji hayo yaliyofanywa na jeshi la polisi, linalowajibika kwake
kama Waziri wa Mambo ya Ndani. Kamati hiyo pia inawahusisha polisi ambao
katika tukio hilo ni watuhumiwa namba moja.
Mbali
ya kusisitiza kuwa haiwezi kutoa ushirikiano kwa kamati ambayo haipo
kwa mujibu wa sheria, CHADEMA kimeshangazwa na kusudio hilo la Kamati ya
Nchimbi kutoa mwaliko wa kutaka kukutana na viongozi wa CHADEMA, huku
ikitambua wazi msimamo wa chama hiki juu ya uwepo wa kamati hiyo mara tu
ilipoundwa.
Kutoa
ushirikiano kwa kamati ambayo haina mamlaka ya kisheria ya kuhakikisha
ukweli mtupu unajulikana na haki ionekane ikitendeka kutokana na kifo
hicho na vingine vingi ambavyo vimefanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya
raia wasiokuwa na hatia, kwa masuala mbalimbali yakiwemo ya kisiasa, ni
kuhalalisha uvunjivu wa haki za binadamu, Katiba na sheria za nchi.
CHADEMA haiko tayari kuona hali hiyo ikifanyika.
Katika
kuonesha msisitizo wa kutokubali mwaliko wa Kamati ya Nchimbi inayotaka
kutafakari matukio ya vifo ambapo Jeshi la Polisi limewanyang’anya watu
wasio na hatia haki ya kuishi, katika barua yake ya majibu, CHADEMA pia
kimeambatanisha nakala ya barua ya tarehe 10/09/2012 iliyowasilishwa
kwa Rais, ili kamati hiyo iweze kuelewa msimamo mpana wa chama kuhusu
mauaji ya kisiasa yanayofanyika nchini.
Kwa taarifa hii, CHADEMA kinaendelea kusisitiza maazimio ya Kamati Kuu
ya Chama, ambayo pamoja na mambo mengine, iliazimia kuwa kutokana na
mfululizo wa matukio ya mauaji ya kisiasa yanayofanywa na Jeshi la
Polisi katika shughuli halali za chama, Waziri wa Mambo ya Ndani
Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema, Mkuu wa
Operesheni wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Morogoro, Faustine Shilogile wawajibike kwa kujiuzulu au Rais
awawajibishe kwa kuwafukuza kazi ili wapishe uchunguzi huru na wa haki.
Pia
Kamanda wa Polisi Iringa, Michael Kamuhanda, Kamanda wa FFU Mkoa wa
Morogoro, na askari wote wanaoonekana kwenye picha wakiwa wamemzunguka
Mwangosi muda mfupi kabla hajalipuliwa na kuuwawa, wakamatwe haraka na
kushtakiwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya Mwangosi.
Kinyume
na hapo ni kuchezea akili za wapenda haki na uwajibikaji, ikiwa moja ya
misingi ya amani Tanzania na dunia nzima kwa ujumla.
CHADEMA
inapenda kusisitiza kuwa itatoa ushirikiano kwa chombo kitachoundwa kwa
mujibu wa Sheria huku ikitilia msisitizo wito kwa Rais kuunda Tume ya
Kimahakama/Kijaji kuchunguza vifo vyote vyenye utata na vinavyohusishwa
na masuala ya kisiasa kama tulivyopendekeza kwake hapo kabla.
Imetolewa leo Septemba 24, 2012 Dar es Salaam na;
No comments:
Post a Comment