MWANDISHI WA CHANEL TEN DAUDI MWANGOSI AZIKWA KIJIJINI KWAO
MAZISHI
ya Mwandishi wa Habari, Daud Mwangosi yalifanyika jana katika Kijiji
cha Busoka kilichoko wilayani Rungwe, Mbeya na kuhudhuriwa na mamia ya
waombolezaji wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi
Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod
Slaa. Katika mazishi hayo, viongozi hao wawili kila mmoja alitangaza
kuwasomesha watoto wa marehemu Mwangosi ambaye alifariki dunia Septemba
2, mwaka huu baada ya kupigwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu wakati
polisi walipokuwa wakisambaratisha mkutano wa Chadema.
Akitoa
salamu zake katika mazishi hayo, Profesa Mwandosya alisema yupo tayari
kumsomesha mtoto wa kwanza kati ya wanne wa Mwangosi, Nehemia ambaye
anasoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Malangali.
Alisema
atamsomesha mtoto huyo kidato cha tano na sita na ikiwa atafaulu na
kukosa mkopo wa elimu ya juu, atamsomesha mpaka atakapomaliza elimu yake
ya juu.
Dk
Slaa kwa upande wake, alisema amewasiliana na rafiki yake ambaye yupo
tayari kuwasomesha watoto wawili wa Mwangosi ambao wote wapo shule ya
msingi. Mtoto wa mwisho wa marehemu hajaanza masomo.
Pamoja na kuwasomesha watoto hao, alisema Chadema kimetoa Sh2 milioni za rambirambi kutokana na msiba huo.
Vijembe msibani
Awali,
Profesa Mwandosya na Dk Slaa walitoa kauli zinazoonyesha kupigana
vijembe vya kisiasa, baada ya waziri huyo kumtaka Dk Slaa aache kufanya
kampeni za kuingia Ikulu mwaka 2015 msibani.
Kauli
hiyo ya Profesa Mwandosya ilikuja baada ya Dk Slaa kutaka polisi
waliohusika na mauaji hayo wachukuliwe hatua za kisheria kwa sababu
wanajulikana.
“Tunashangaa
wamekamatwa watu wengine na kuwaacha waliohusika na mauaji hayo,
tunawajua kwa sababu wameonekana hadharani, hakuna siri kwa hilo,”
alisema Dk Slaa.
Akizungumza
baada ya kauli hiyo ya Dk Slaa, Profesa Mwandosya aliwataka wanasiasa
wa vyama vya upinzani kuacha kutumia misiba kutafuta kura za urais mwaka
2015.
“Natoa
pole sana kwa familia na tasnia nzima ya habari nchini. Hiki ni kipindi
kigumu, lakini tuviachie vyombo husika vifanye uchunguzi wa mauaji
haya,” alisema Profesa Mwandosya na kuongeza:
“Lakini
nichukue fursa hii kuwaomba wanasiasa waache kutumia misiba ili
kujipatia umaarufu katika kutafuta kura za urais mwaka 2015.”
Katika
mahubiri yake msibani hapo, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Busoka, Mathayo Mwanjemele alikemea mauaji
hayo na kuwaomba wahusika wajitokeze hadharani kabla Mungu hajawaumbua.
“Waliohusika
na mauaji haya wajitokeze na kutubu kwa wananchi kabla adhabu ya Mungu
haijawakuta,” alisema. Alisema ufike wakati Serikali iwe inakiri uzembe
unaofanywa na watendaji wake ambao umekuwa ukitokea mara kadhaa.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment