TAKWIMU SAHIHI NA ZA WAKATI ZITASAIDIA KULETA MAENDELEO KWA HARAKA BARANI AFRIKA.

NA: VERONICA KAZIMOTO
14 JANUARI, 2015
KAMPALA.
WITO 
umetolewa kwa washiriki wote wa Mkutano wa Kumi wa Maendeleo ya Takwimu 
Afrika kuelendelea kutoa takwimu sahihi na kwa wakati ili kuleta 
maendeleo yanayokusudiwa ya kiuchumi na kijamii barani Afrika.
Wito huo 
umetolewa jana na Waziri Mkuu wa Uganda Mhe. Dkt. Ruhakana Rugunda 
wakati akifungua Mkutano wa Kumi wa Maendeleo ya Takwimu Afrika 
uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Speke Munyoyo Kampala, Uganda.
Dkt. 
Rugunda amesema kuwa, ili kupata maendeleo kwa haraka, ni lazima takwimu
 zitolewe kwa wakati na ziwe sahihi kwa ajili ya kusaidia kupanga 
mipango mbalimbali ya maendeleo.
"Ili Bara
 la Afrika liweze kuendelea kwa haraka, linahitaji takwimu sahihi na 
zinazotolewa kwa wakati ili takwimu hizo zisaidie katika kupanga mipango
 mbalimbali ya maendeleo", amesema Waziri Mkuu Rugunda.
Dkt. 
Rugunda ameongeza kuwa ili kuweza kufanikisha hilo, kuna umuhimu kwa 
nchi za Afrika kusaidia program mbalimbali za uzalishaji wa takwimu na 
matumizi yake kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo.
Kwa 
upande wa Waziri wa Fedha wa Uganda Matia Kasaija amesema kuwa, ili 
kuweza kulinganisha takwimu za nchi mbalimbali, ni vyema takwimu 
zinazozalishwa zikafuata mbinu bora za uzalishaji wa takwimu.
Matia 
Kasaija amesema mbinu bora za uzalishaji wa takwimu ni zile zinazofuata 
viwango vinavyopendekezwa na Umoja wa Kimataifa - Kitengo cha Takwimu.
Mkutano 
wa Kumi wa Maendeleo ya Takwimu Afrika umewakutanisha washiriki 
takribani 400 kutoka nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania. Mkutano
 huu ni wa siku tatu na unatarajia kumalizika kesho tarehe 15 Januari, 
2015.
No comments:
Post a Comment