NYALANDU AKARIBISHA WAFANYABIASHARA WA SAUDI ARABIA KUWEKEZA SEKTA YA UTALII NCHINI
Waziri wa
Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu (wa pili kushoto) akimsikiliza
kwa makini Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudi Arabia Dk.
Abdulrahman Al-Zamil (wa tatu kushoto) jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Wengine katika picha kutoka kulia ni Mshauri wa Ushirikiano wa Kimataifa
wa Mamlaka ya Wanyamapori ya Saudia Mohammad Sulayem; Katibu Mkuu wa
Maliasili na Utalii Dk. Adelhelm Meru na Balozi wa Tanzania nchini Saudi
Arabia Prof. Abdillah Omari.
Waziri wa
Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu (kushoto) katika mazungumzo na
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudi Arabia Dk. Abdulrahman
Al-Zamil jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Mhe.
James Lembeli (kushoto) akikaribishwa na Mwenyekiti wa Chemba ya
Biashara ya Saudia Dk. Abdulrahman Al-Zamil jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Waziri
Kivuli wa Maliasili na Utalii Mhe. Peter Msigwa (kushoto) akikaribishwa
na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudia Dk. Abdulrahman Al-Zamil
jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Ujumbe wa
Serikali ya Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.
Lazaro Nyalandu (wa tano kushoto) ukiwa katika picha ya pamoja na
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudia Dk. Abdulrahman Al- Zamil (wa
sita kushoto) mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina ya pande
mbili jijini Riyadh, Saudi Arabia. Wengine pichani kutoka kushoto ni
pamoja na Mkurugenzi wa Wanyamapori Herman Keraryo; Mkurugenzi Mkuu
TANAPA Allan Kijazi; Mhe James Lembeli; Mhe Peter Msigwa; Katibu Mkuu
Maliasili na Utalii Dk. Adelhelm Meru pamoja na maafisa kutoka Chemba ya
Biashara ya Saudia.
Waziri wa
Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu amewakaribisha wafanyabiashara
kutoka Saudi Arabia kuwekeza katika sekta ya utalii nchini ambayo ina
fursa nyingi za uwekezaji. Nyalandu alitoa wito huo kufuatia mazungumzo
yake na Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara ya Saudi Arabia Dk.
Abdulrahman Al-Zamil yaliyofanyika Riyadh, Saudi Arabia jana.
Waziri
Nyalandu ambaye anaongoza ujumbe wa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini
Saudia alibainisha kuwa mazingira ya uwekezaji nchini yanavutia na
kutaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli na loji za kisasa
zitakazoweza kuvutia watalii wengi zaidi katika maeneo ya mijini pamoja
na ndani ya maeneo ya uhifadhi.
Alisema
kuwa utalii wa Tanzania unakua kwa kasi nzuri kutokana jitihada
zinazofanywa na serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kutangaza
vivutio vya utalii na kuwa juhudi hizo lazima ziende sambamba na
upatikanaji wa huduma bora za malazi. "Upatikanaji wa huduma nzuri za
malazi ya bei nafuu utasaidia kuvutia watalii wengi zaidi nchini na kwa
maana hiyo tunawakaribisha kuja kuzitumia fursa zilizopo ili kuweza
kukuza uchumi wa nchi yetu", alisema Nyalandu.
Waziri
Nyalandu ambaye anaongoza ujumbe wa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini
Saudia, alisema kuwa Tanzania ni ya pili ulimwenguni baada ya Brazil
kwa kuwa na vivutio vizuri vya asili vya utalii na kuwa rasilimali hizi
zinapaswa sasa kutumiwa vema ili kuinua uchumi na njia pekee ni pamoja
na kuvutia wawekezaji na mitaji kutoka Saudia ili kufikia azma hiyo.
Kwa
upande wake Dk. Al-Zamil aliahidi kuwashirikisha wafanyabiashara wenzake
kutikia wito huo na kwa kuanzia timu ya wafanyabiashara pamoja na
mawakala wa utalii watafika nchini katika siku chache zijazo ili kuona
namna gani wataweza kuzitumia fursa zilizopo kikamilifu. Aidha, katika
eneo la utalii Al- Zamil alisema kuwa Chemba yake itafanya kila
liwezekanalo kubadilisha mtazamo wa Wasaudia wanaotembelea kwa wingi
maeneo mbalimbali ya utalii duniani ili waweze kuitembelea Tanzania na
kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana nchini.
Aidha,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Adelhelm Meru alisema
kuwa serikali itaandaa Kongamano Maalum la Uwekezaji nchini Saudi Arabia
ili kuweza kutangaza fursa mbalimbali zzilizopo nchini ambazo
zikitumika vema zinaweza kuinua uchumi wa taifa.
Hivi sasa
Tanzania inategemea idadi kubwa ya watalii kutoka Mataifa ya Ulaya na
Amerika na kwamba japokuwa idadi ya watalii kutoka nchi za kiarabu
haizidi 15,000 kwa mwaka, bado jitihada za utangazaji na uwekezaji
zikifanywa vizuri idadi ya watalii kutoka mataifa ya kiarabu itaweza
kuongezeka nchini.
Ujumbe wa
Tanzania unajumuisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk.
Adelhelm Meru; Balozi wa Tanzania Saudi Arabia Prof. Abdillah Omari;
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
Mhe. James Lembeli, Waziri kivuli wa Maliasili na Utalii Mhe. Mchingaji
Peter Msigwa; Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Allan Kijazi pamoja
na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Herman Keraryo.
No comments:
Post a Comment