Rais Obama ataka mgao sawa wa rasilimali
Rais wa
Marekani Barak Obama, amesema Marekani inafanya mabadiliko ya kiuchumi
na kijamii baada ya miaka mingi ya kujirudia kwa mdororo wa uchumi na
vita, huku uchumi ukiongeza ajira kwa kasi kubwa kuliko wakati wowote
tangu mwaka 1999.
Pia amesema Wamarekani wengi zaidi wana bima za afya kuliko wakati wowote kabla ya hapo.
Akihutubia
taifa kupitia baraza la Congress lenye wajumbe wengi kutoka chama cha
Republican, Rais Obama ametumia hotuba hiyo kutangaza mpango wa kujenga
uchumi wa kati kwa wananchi wote wa Marekani, ambapo wananchi wa kipato
cha chini watapata huduma za afya na elimu kwa gharama nafuu.
Rais
Obama ametangaza hatua za kusaidia familia za wafanyakazi kunufaika
kutokana na kukua kwa uchumi.Mkakati wa Bwana Obama anaouelezea kama
uchumi wa daraja la kati, unahusisha kupandisha kodi kwa matajiri.
Hotuba ya
Rais Obama ilibeba mapendekezo kuhusu kodi, vyuo vya jamii, huduma za
internet, usalama katika mtandao wa komputa na likizo ya ugonjwa.
Bwana Obama amesema hali ya kutoka katika mdororo wa uchumi imetoa fursa ya kuongezeka kwa kipato na fursa kwa kila mtu.
Amesema
uchumi wa daraja la kati ni wazo kwamba nchi hiyo inafanya vizuri kabisa
wakati kila mtu anapata haki katika mapato na kila mtu anatendewa haki
kama ilivyoanishwa katika sheria za nchi hiyo.
Mpango
wake wa kuongeza kodi kufikia dola bilioni 320 katika kipindi cha zaidi
ya miaka kumi ni pamoja na kuziba mianya ya kukwepa kodi kwa wenye
vipato vikubwa, ambapo matajiri wakubwa watalipa kodi ya kukua kwa mtaji
kutoka asilimia 23.8% hadi asilimia 28%.
No comments:
Post a Comment