NYALANDU AZIMA MARUFUKU MAGARI YA TANZANIA JKIA
WAZIRI wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema serikali ya Kenya
imekubali kuyaruhusu magari ya abiria na watalii kutoka Tanzania,
kuingia ndani ya Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Awali,
Serikali ya Kenya iliyazuia magari hayo kuingia uwanjani hapo huku
ukiyatoza ushuru kwa yale yanayoingia, jambo ambalo lililalamikiwa na
wafanyabiashara wa Tanzania.
Marufuku
hiyo ya Kenya kwa magari ya Tanzania, ilidumu kwa zaidi ya wiki mbili,
ambapo katika kusaka suluhu hiyo Nyalandu alikutana na wafanyabiashara
hao jijini Arusha kisha kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa
Biashara na Utalii wa Kenya, Phyllis Kandie.
Katika
mazungumzo yake na Kandie, Nyalandu alisema kwa sasa magari ya Tanzania
yataendelea kuingia uwanjani hapo wakati ufumbuzi wa kudumu ukitafutwa.
Alisema kutakuwa na vikao vya kazi baaina ya Wizara ya Utalii ya Kenya na wizara yake, ambapo vitaanzia ngazi ya watandaji, watalaamu, makatibu wakuu na mawaziri.
Alisema katika mikutano hiyo masuala mbalimbali kuhusiana na biashara ya utalii yatazungumzwa baina ya nchi hizo mbili.
Hata hivyo, alisema katika vikao hivyo suala la mpaka wa Bolongoja halitajaliwa wala kuwepo kwenye ajenda.
"Kwa sasa
wafanyabiashara wetu wataingia Jomo Kenyatta kama ilivyokuwa awali.
Tumezungumza na kupanga kuwa na vikao kujadili na kuzipatia ufumbuzi
changamoto zote kuhusiana na sekta ya utalii.
"Niwahakikishie
tu katika vikao hivyo maslahi ya pande zote yatazingatiwa, lakini suala
la mpaka wa Bolongoja halitajadiliwa wala kuwemo kwenye ajenda za vikao
vyetu.
"Wataalamu
na watendaji wa wizara yangu watakutana na wenzao jijini Arusha na
maofisa wa Jumuia ya Afrika Mashariki watashiriki ili kutafuta ufumbuzi
wa kudumu," alisema Nyalandu.
Kupatiwa
ufumbuzi kwa tatizo hilo kumekuwa faraja kubwa kwa wafanyabiashara na
wadau wa utalii katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, ambapo
walipongeza jitihada za haraka zilizofanywa na Nyalandu.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, wadau hao wa utalii walisema Nyalandu
ameonyesha utendaji kazi kwa vitendo na kwamba, hilo linapaswa kuwa
mfano kwa viongozi wengine.
Walisema
waziri huyo baada ya kupata taarifa za wafanyabiashara wa Tanzania
kuzuiwa kuingiza magari Jomo Kenyatta, aliwafuata kwenye maeneo yao na
kuwasikiliza kero zinazowakabili kisha kufunga safari kukutana na waziri
Kandie jijini Nairobi.
"Hawa
ndio aina ya viongozi ambao Tanzania ya sasa na inayokuja inawahitaji,
wanaposikia wananchi wana kero na wananyimwa haki ama kunyanyaswa
wanakwenda kuwasikiliza na kutafuta ufumbuzi wa haraka. "Kwa hili Waziri
Nyalandu anastahili pongezi na viongozi wengine waige mfano huu,
wangekuwa wengine wangeanza kuleta siasa na tatizo kuchukua muda mrefu
kupata ufumbuzi," alisema John Mlay, ambaye ni mmoja wa wafanyakazi
kwenye kampuni za usafirishaji watalii.
No comments:
Post a Comment