Dar es
Salaam. Wakati wananchi wakisubiri vigogo wa serikalini na mawaziri
wanaotuhumiwa kuhusika kwenye kashfa ya uchotaji fedha kwenye Akaunti ya
Tegeta Escrow kufikishwa mbele ya vyombo vya umma, ni watumishi watano
tu wa umma waliofikishwa mahakamani, lakini Mkurugenzi wa Takukuru, Dk
Edward Hoseah ana jibu la suala hilo; kazi yao ni kufikisha mahakamani
'vidagaa'.
Katika
kashfa hiyo ya Sh306 bilioni, mawaziri wa sasa na zamani pamoja na
makatibu wakuu wa wizara, wanatuhumiwa kwa njia moja au nyingine
kuhusika kwenye kufanikisha kwa makusudi au uzembe uchotwaji wa fedha
hizo, kuikosesha mapato Serikali na kupokea mgawo wa fedha hizo, lakini
hadi sasa ni watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Wizara ya Nishati na
Madini, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Tanesco na Benki Kuu
(BoT) pekee waliofikishwa mahakamani.
Wote
watano, ambao ni vigogo kwenye taasisi zao, wameshtakiwa kwa kosa la
kuomba na kupokea rushwa ili kufanikisha mkakati huo ulioibuliwa na
gazeti la The Citizen na baadaye Bunge kulidaka na kufikia maazimio ya
kutaka wahusika wote wawajibishwe na mamlaka zinazowahusu.
Juzi,
mkurugenzi huyo wa Takukuru aliliambia gazeti hili kuwa taasisi yake
itaendelea kuchunguza watu wote waliohusika katika kashfa ya escrow bila
ya ubaguzi, lakini akabainisha kuwa kazi ya kuwapeleka mahakamani
mawaziri na vigogo inatakiwa ifanywe na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP).
Dk
Hoseah, ambaye aliwahi kuingia kwenye mzozo wa DPP wa zamani kutokana na
madai yake kuwa mafaili mengi ya kesi za rushwa hayafanyiwi kazi,
alisema sheria haiwaruhusu kuwapeleka mahakamani mawaziri iwapo
watabainika kuhusika kwenye vitendo vya rushwa.
Kwa
mujibu wa kifungu cha 57 cha Sheria Namba 11 ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa ya Mwaka 2007, endapo vigogo na mawaziri watabainika kuhusishwa
na vitendo vya rushwa, jalada la uchunguzi wao litakabidhiwa kwa DPP ili
achukue hatua ya kuwapeleka mahakamani.
Dk Hoseah
alisema kwa sasa Takukuru inaendelea na uchunguzi wake mpaka
itakapojihakikishia ushahidi wa kutosha dhidi ya vigogo hao.
"Bunge
lilitoa maazimio yake na likaagiza kuchukuliwa hatua...Takukuru
tulishaanza na tunaendelea na uchunguzi. Taratibu zote zikishakamilika
kisha ushahidi ukapatikana kwa vielelezo vyote, basi watafikishwa
mahakamani wala hakuna tatizo lolote," alisema.
"Lakini
watafikishwa mahakamani baada ya sisi kuwasilisha jalada letu la
uchunguzi kwa DPP ambaye ndiye mamlaka ya kuwafikisha mahakamani kama
sheria inavyotuagiza."
Udhaifu
huo wa sheria pia ulizungumziwa na Bunge wakati wa kujadili kashfa ya
escrow na kuazimia kuwa sheria inayounda Takukuru ifanyiwe kazi ili iwe
na mamlaka hayo ya kufikisha mahakamani vigogo wa rushwa kubwa.
Waliohusishwa na rushwa
Mawaziri
waliotajwa kwenye sakata hilo ni Profesa Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ambaye aliingiziwa
Sh1.6 bilioni na mwanahisa wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James
Rugemarila. Tibaijuka alivuliwa wadhifa huo kutokana na sakata
hilo.Wengine ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
ambaye Rais Jakaya Kikwete alisema amemuweka kiporo baada ya Bunge
kumuona kuwa hakushughulikia vizuri suala hilo na kuisababishia Serikali
kukosa mapato.
Wengine
ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na ambaye alikuwa Mwanasheria
Mkuu, Andrew Chenge, ambaye aliingiziwa pia Sh1.6 bilioni kwenye
akaunti yake na Rugemarila; waziri wa zamani wa Nishati na Madini,
William Ngeleja, aliyeingiziwa Sh40.4 milioni; aliyewahi kuwa Waziri wa
Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4 milioni), mbunge wa zamani wa
Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh40.4 milioni) na aliyekuwa mjumbe wa
Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni).
Vigogo
waliotajwa kwenye sakata hilo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliackim Maswi, ambaye amesimamishwa, Fredrick Werema, ambaye
alijiuzulu kwa maelezo kuwa ushauri wake kuhusu suala la kodi kwenye
fedha hizo haukueleweka na ulisababisha tafrani.
Awali, Dk
Hoseah aliliambia gazeti dada la The Citizen kwamba katika uchunguzi
wake, hakuna kiongozi wala kigogo yeyote ambaye atapona.
"Yeyote
yule ambaye atabainika katika uchunguzi wetu, lazima afikishwe mbele ya
sheria, hakuna kigogo wala kiongozi yeyote ataweza kukwepa endapo
ushahidi utaonekana wazi," alisema.
Alipoulizwa
kama uchunguzi huo unamjumuisha Profesa Tibaijuka, mkurugenzi huyo
alisema hawezi kutaja jina la mtu kwa kuwa ni kinyume cha sheria kutaja
jina au taarifa ambazo ziko kwenye uchunguzi."
Waliofikishwa
mahakama ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi sasa ni Mhandisi Mkuu
wa Mradi wa Umeme Vijijini (Rea), Theophillo Bwakea na Mkurugenzi wa
Huduma za Kisheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Rugonzibwa Mujunangoma, ambao kwa pamoja wanadaiwa kupokea rushwa ya
Sh485.1 milioni.
Wengine
ni Meneja Misamaha ya Kodi wa TRA, Kyabukoba Leonard Mutabingwa,
Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Roman Urassa na Mkurugenzi wa
Fedha BoT, Julius Rutta Angello wanaokabiliwa na mashtaka ya kuomba na
kupokea rushwa ya jumla ya Sh1.923 bilioni.
Maoni ya wasomi
Akizungumzia
suala hilo, Profesa Gaudence Mpangalla kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha
alihoji sababu za Serikali kushindwa kuchukua hatua za haraka kuijengea
uwezo Takukuru ili iweze kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa aina hiyo.
"Kama
tunavyoona hivi sasa inawapandisha kizimbani watumishi wengine, sasa
kuna tofauti gani na waziri atakayebainika kukutwa na kosa kama hilo?
Sioni tofauti yoyote kwa wakosaji hao," alisema.
"Udhaifu
huo unaweza kujenga imani kwamba Serikali inawabeba mafisadi kwa mgongo
wa ofisi ya DPP kwa sababu mashtaka mengi hayafanyiwi kazi katika ofisi
hiyo."Mara kadhaa Dk Hoseah amekuwa akitoa kauli zinazoonyesha kuwa
ameshawasilisha majalada mengi ofisi ya DPP, lakini amekuwa akiyakalia
au kuyarudisha kutaka uchunguzi ukamilike.
Hata hivyo, Profesa Chris Maina wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anaona hilo halitafanyika kwa hivi sasa.
"Kwa
jinsi sakata hilo lilivyoibuliwa na ushahidi kuwekwa wazi na Rais
akaonyesha hisia zake, lazima DPP ajaribu kuwa makini sana na mawaziri
au vigogo watakaofikishwa mbele yake," alisema.
"Inamlazimu
achukue hatua za haraka. Hili suala siyo sawa na mashtaka mengine...
lakini tusubiri kwa sababu ni kiongozi mpya aliyeingia ofisi hiyo
hatujui itakuwaje."
CHANZO:MWANANCHI