TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Friday, August 29, 2014

UGUNDUA WA GESI ASILIA UJAZO WA TRILIONI 50.5 


Na Anitha Jonas – Maelezo
Tanzania imegundua gesi asilia katika maeneo 19 ya mwambao na kina kirefu cha maji baharini ambayo ina ujazo wa trilioni 50.5.
Kati ya maeneo hayo 19 yaligundulika gesi hiyo ,matano yanapatikana katika mwambao na 14 yapo katika kina kirefu cha maji baharini .(Martha Magessa)
Hata hivyo gesi iliyogundulika katika maeneo ya mwambao kama Songo songo na Mnazi Bay kwa sasa inatumika kufua umeme na pia kwa ajili ya matumizi ya viwandani,majumbani na kwenye magari.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro wakati akifungua kongamano la wadau wa mafuta na gesi linalofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa huyo amewataka wadau hao watumie muda wao kutoa maoni yatakayosaidia kuwa Sera ya Mafuta na Gesi asilia itakayowanufaisha watanzania pindi itakapoanza kutumika.
Kandoro ameongeza kuwa ni vema Sera hiyo ikasaidia Serikali kupata mapato yake yatakayotokana na Mafuta na Gesi asilia kwa ajili ya kuleata maendeleo mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wake.
"Uandaaji wa sera hii ulipitia marejeo ya nyaraka mbalimbali ikiwemo sera ya petroli za nchi zilizogundua nishati ya mafuta na gesi asilia zikiwemo Uganda,Ghana,Sierra Leone na Pakistani".
Mpaka Oktoba mwaka jana (2013) Serikali ilikuwa imekamilisha sera ya gesi asilia ,hii ni kwa ajili ya kutoa muongozo wa kusimamia na kuendesha biashara ya gesi asilia katika uchakataji,usafirishaji na usambazaji", alisema Kandoro.
Amesema kuwa Sera hiyo itazingatia na kuangalia kwa ukaribu suala la udhibiti wa mazingira ukomo wa uzalishaji wa rasilimali hiyo pale utakapoanza.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Jiolojia kutoka Wizara ya Nishati na Madini Adam Zuberi amesema lengo la sera hiyo ni kuhakikisha rasilimali ya gesi asilia inawanufaisha watanzania wote kwa mapato yatakayopatikana katika maeneo husika kwani asilimia 3 itabaki Halmashauri kwa matumizi ya wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),Prof. Ibrahim Lipumba ameishauri Serikali kuwa makini katika makubaliano na makampuni yatakayochimba gesi katika mgawanyo wa mapato kama inavyoonyesha katika sera kuwa asilimia 60 ya mapato itapelekwa Serikalini. Pia umakini na uangalifu wa hali ya juu unahitajika kwenye makubaliano hayo.
Mkutano huo wa wa siku moja uliandaliwa na wizara ya Nishati na Madini na kujumuisha wataalam mbalimbali waliobobea katika masuala ya mafuta ,wawakilishi wa ofisi za ubalozi zilizopo nchini ,Vyama vya siasa , viongozi wa dini, Wakuu wa Mikoa na asasi za kiraia .

No comments:

Post a Comment