JK AOMBWA KUSITISHA BUNGE LA KATIBA
JUKWAA la
Katiba Tanzania (Jukata), limemuomba Rais Jakaya Kikwete asitishe Bunge
Maalumu la Katiba, lakini pia limevionya vyama vya siasa nchini
kuhusiana na vitisho vya kuwashughulikia wanachama wao kuhusiana na
Bunge hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba
Tanzania, Deus Kibamba, alisema kauli ya baadhi ya viongozi wa vyama vya
siasa kwamba watawashughulikia wanachama wao, ambao ni wajumbe wa Bunge
hilo si nzuri na kusisitiza kwa hali ilivyo sasa kuna haja Rais Kikwete
asitishe Bunge Maalumu la Katiba.(MM)
"Yatosha
tu kusema kwa sasa nchi imegawanyika vibaya kuhusu mchakato wa Katiba
mpya na ulipofikia, haikuwa mshangao kushuhudia wajumbe watatu kutoka
kundi la Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) wakitinga bungeni na
kujiandikisha ili kuendelea na vikao vya Bunge, akiwemo Mwatuka (Clara)
kutoka CUF.
"Wengine
ni waheshimiwa Leticia Nyerere, John Shibuda na Said Arfi, wote kutoka
Chadema na Chiku Abwao pia wa Chadema, ambaye baada ya kusoma upepo kuwa
Ukawa wamesusia kiukwelikweli amekanusha na kwamba alikuwa na shughuli
zake binafsi mjini Dodoma na wala hakufika kushiriki vikao vya Bunge.
"Vyama
vyao vya CUF na Chadema vimeahidi kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa
kukiuka maamuzi ya vikao halali vya kichama, lakini jambo moja dhahiri
ni kuwa hawa ni wahanga tu wa tatizo kubwa zaidi la mpasuko wa kitaifa,"
alisema Kibamba.
Alisisitiza
kuwa suala la kuchukuliana hatua au kushughulikiana si zuri na halileti
tatizo la ufumbuzi uliopo kwani hata Ukawa wenyewe wamegawanyika, CCM
nao wamegawanyika na jambo la msingi ni kutafuta ufumbuzi wa kitaifa
kwani kuna mpasuko mkubwa ndani ya Bunge Maalum la Katiba, kijamii na
hakuna maridhiano ya kitaifa.
"Kuna
wajumbe wamechelewa kufika Dodoma kwa kuwa wanaamini Bunge Maalumu
halipaswi kuendelea kwa hali hii, aidha hata miongoni mwa wajumbe wa CCM
kuna mpasuko wa waziwazi kati ya wanaoamini kuwa Bunge Maalumu
halipaswi kuendelea kwa sasa kwa kuwa theluthi mbili haitaweza kufikia
maridhiano yanayohitajika ili Katiba mpya iweze kuandikika," alisema.
Alisema
kuna wajumbe zaidi ya wanne wa CCM wametoa sauti kuhusiana na Bunge hilo
na kwamba wapo wengi na ni ishara kuwa CCM nako kuna mpasuko.
Alidai
kuwa CCM imegawanyika katika makundi matatu kuhusiana na mchakato huo na
kuyataja kuwa ni kundi la wanaoondoka madarakani, kundi la wasio na
upande ambao wapo kimya na kundi la wanaotaka madaraka.
"Pia hata
miongoni mwa wana Ukawa kumetokea mpasuko kati ya wale wanaoamini kuwa
hakuna haja ya kushiriki Bunge Maalumu, ambalo hatima yake hakutazaliwa
Katiba mpya na wale wanaoamini kuwa wana haki ya kimsingi ya kushiriki
vikao Bunge Maalumu la Katiba na kupata posho zao kama wale wa CCM,"
alisema.
Pia alieleza kuwa kuna wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete ambao wameduwaa na hawajui la kufanya.
"Tunashauri
kuwa mchakato wa kuandika Katiba mpya uahirishwe hadi baada ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015 ili uanze tena Januari 2016 na kwamba ili kuokoa
gharama za uchaguzi wa Serikali za Mitaa, chaguzi hizi mbili zifanyike
siku hiyo hiyo moja ya Uchaguzi Mkuu," alisema.
Pia
Kibamba alieleza kitendo cha Ukawa kushindwa kurejea bungeni kinaunyima
mchakato wa Katiba uhalali wa kisiasa na kisheria na kwamba upande wa
wajumbe wa Zanzibar wanafanya kukosekana kwa theluthi mbili
inayohitajika.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment