TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, August 19, 2014

Uamuzi mgumu CCM katika Kamati Kuu leo

Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya CCM inakutana leo mchana mjini Dodoma chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete huku ikitarajiwa kufanya uamuzi mgumu wa mchakato wa Katiba.
Kikao hicho kinaketi mara ya pili katika muda mfupi, baada ya hivi karibuni kukaa jijini Dar es Salaam na kueleza kuridhishwa na mchakato huo.(I.N)
Hata hivyo, safari hii kikao hicho kinaketi kukiwa na maswali lukuki ambayo hayajapata majibu: Je, Bunge la Katiba liendelee au livunjwe? Je, lisitishwe kwa muda kupisha maridhiano au la? Je, kuna umuhimu wa maridhiano? Kuna ulazima wa kuwapo Ukawa bungeni?
Akizungumzia kikao hicho, mtaalamu wa sayansi ya siasa na utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema jambo kubwa litakalojadiliwa katika kikao hicho ni kauli tofauti zilizotolewa na wananchi kuhusu mchakato wa kupata Katiba Mpya.
"Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba ameshauri yafanyike maridhiano kwanza na wapo wanaCCM waliomuunga mkono. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema naye ameonyesha wasiwasi wake, Ukawa na Jukwaa la Katiba Tanzania nao wamesema yao. Nadhani kuna jambo CCM wameliona na wanataka kuliweka sawa," alisema Dk Makulilo.
Aliongeza, "Kujua nini wataamua ni ngumu lakini kutokana na hali ilivyo kwa sasa ni wazi kuwa wanakutana kuona nini kifanyike."
Kwa upande wake Bashiru Ali alisema, "Tangu mwanzo mchakato wa Katiba haukuwa katika ilani ya CCM, sasa unaweza kujiuliza wanakwenda kujadili nini wakati hata katika mikakati yao ya miaka 10 na 20 ijayo hakuna mpango wa kuandika Katiba."
Habari zilizozagaa mjini Dodoma zinadai kikao hicho pia kinaweza kupendekeza kuwashughulikia wanachama wake waliotoa kauli zinazopingana na msimamo wa chama hicho.
Miongoni mwa waliotoa kauli zinazopingana na chama hicho ni Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba kutokana na matamshi yake ya kuhoji uhalali wa vikao vya Bunge la Katiba kuendelea bila uhakika wa akidi.
Mbali na Mwigulu pia wabunge kadhaa wa CCM akiwamo, Esther Bulaya (Viti Maalumu), Kangi Lugora (Mwibara), Deo Filikunjombe (Ludewa), Ridhiwani Kikwete (Chalinze) nao wamekaririwa kwa nyakati tofauti wakitoa misimamo inayokinzana na chama chao kuhusu uhalali wa Bunge la Katiba kuendelea bila kuwapo maridhiano na Ukawa.
Hata hivyo, habari nyingine zinasema iwapo kuna mpango huo, Mwigulu anaweza kuondolewa kutokana na utaratibu wa chama hicho kuwaondoa kwenye sekretarieti wajumbe wake wanaoteuliwa kushika nyadhifa serikalini.
Chanzo chetu kinasema ikiwa hilo litatokea kwa sababu ya Mwigulu kuteuliwa Naibu Waziri wa Fedha, basi mpango huo hautamwacha nyuma Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje, Dk AshaRose Migiro ambaye pia hivi karibuni aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba.
CHANZO:MWANACHI

No comments:

Post a Comment