Israel na Hamas waendelea na mapigano
Mgogoro
kati ya Israel na Palestina unaendelea. Pande zote mbili zimekuwa
zikishambuliana kwa maroketi. Wakati huo huo, Misri inataka mazungumzo
ya kuleta amani yaanze tena.
Hali ya
wasiwasi imerejea tena kwa wakaazi wa Israel na ukanda wa Gaza. Awali
Israel na Hamas walikubaliana kuendeleza muda wa kusitisha mapigano.
Lakini makubaliano hayo hayakuheshimiwa. Israel inasema kuwa hapo jana
Hamas ilianza kurusha maroketi kuelekea Israel na ndipo Israel ilipojibu
mashambulizi.
Wizara ya
afya ya Palestina inaripoti vifo vya Wapalestina wasiopungua 10.
Wengine 68 wamejeruhiwa. Israel kwa upande wake inasema kuwa ilifanya
mashambulizi 60 ya angani. Ni mashambulizi yanayolenga nyumba za
viongozi wa Hamas. Lakini sehemu kubwa ya watu wanaokufa ni raia wa
kawaida. Bwana mmoja aliyeshuhudia mashambulizi kwa macho anaelezea
kusikitishwa kwake na mauaji yanayoendelea. "Familia nzima imeuwawa:
Baba, mke wake aliyekuwa na mimba pamoja na watoto wao watatu. Waisraeli
wamelenga familia nzima bila kutoa taarifa na bila sababu yoyote."
Katika
kisa kingine, watu watatu waliuwawa baada ya nyumba yao kubomolewa na
roketi katika ukanda wa Gaza. Nyumba hiyo inaaminiwa kuwa ya kiongozi wa
kijeshi wa Hamas, Mohammed Deif. Msemaji mmoja wa Hamas amethibitisha
kuwa miongoni mwa waliouwawa walikuwepo mke na mtoto wa Deif. Waziri
mmoja wa Israel amenukuliwa akisema kuwa Mohammed Deif anastahili kufa
kama vile Osama bin Laden alivyokufa. Waziri huyo aliongezea kuwa Deif
ni muuaji na kwamba Israel itatumia kila nafasi itakayojitokeza kujaribu
kumuua kiongozi huyo wa Hamas.
Kwa sasa
hakuna ishara za mgogoro huu kutulia. Israel imewaandaa maaskari 2,000
wa ziada kwa ajili ya kufanya operesheni za ardhini wakati wowote ule.
Hata
mazungumzo ya kuleta amani yaliyokuwa yakiendelea Cairo, Misri
yamesitishwa. Wawakilishi wa pande zote mbili wamegoma kuendelea na
juhudi za kupata suluhu ya mgogoro. Misri imewaasa Hamas na Israel
kurejea katika meza ya mazungumzo, ikisema kuwa inajaribu kushawishi
pande zote mbili kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda.
Kwa mujibu wa viongozi wa Palestina na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa,
zaidi ya watu 2,000 wameuwawa tangu mgogoro huu ulipoanza mwezi
uliopita.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/ap/afp
Mhariri: Saumu Yusuf
CHANZO:DW
No comments:
Post a Comment