TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Friday, December 5, 2014

IPTL yazua Kizaazaa Mahakamani


Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPTL na PAP, Harbinder Singh Sethi
Kampuni za Pan Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP) na Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), zimewasilisha maombi ya kutaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) akamatwe kwa kukiuka amri ya Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) kwa kufuta Hati za Malipo ya Kodi za Mauzo ya Hisa (Capital Gain Certificate).
Kampuni hizo mbili, ambazo ziko kwenye mgogoro wa umiliki, ndizo zinahusika kwenye sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya kuuza umeme unaofuliwa na IPTL, kwa Shirika la Umeme (Tanesco), wakati wa kusubiri uamuzi wa mahakama katika kesi ya kupinga tozo hilo.
PAP, ambayo inadai imenunua hisa zote za IPTL, ndiyo iliyolipwa fedha zote zilizokuwa kwenye akaunti hiyo na kuamsha mjadala mkubwa bungeni ulioisha kwa Bunge kufikia uamuzi wa kuwawajibisha kisheria wote waliohusika, wakiwemo mawaziri.
Lakini uamuzi huo wa Bunge haukuwa tamati la sakata hilo baada ya kampuni hizo mbili kukata rufaa TRAB dhidi ya Kamishna wa TRA na Msajili wa Kampuni na Leseni (Brela) zikipinga kusudio la kufuta hati hizo.(P.T)
Jana kampuni hizo mbili ziliwasilisha maombi ya hati ya kutaka Kamishna Mkuu wa TRA akamatwe, zikidai kuwa amepuuza amri hiyo iliyomzuia kutekeleza azma yake ya kufuta Hati za Malipo ya Kodi ya Mauzo ya Hisa.
Katika maombi hayo walalamikaji hao wanadai kuwa licha ya TRAB kutoa zuio hilo Novemba 26, 2014, Kamishna Mkuu wa TRA, ambaye ni mlalamikiwa wa kwanza, alitoa amri ya kuziondoa hati hizo siku iliyofuata, yaani Novemba 27, 2014, bila kujali amri hiyo.
Walalamikaji hao pia wanaiomba TRAB, baada ya kumkamata Kamishna Mkuu wa TRA, itoe amri afungwe kwa kudharau amri halali iliyotolewa na bodi na pia imwamuru akidhi matakwa ya amri ya TRAB ya Novemba 26.
Pia walalamikaji hao wanaiomba TRAB imwamuru mlalamikiwa huyo, kulipa gharama za uendeshaji wa shauri hilo pamoja na amri nyingine ambazo itaona kuwa zinafaa.
Maombi hayo ya PAP na IPTL ya hati ya kumkamata na kuamuru Kamishna Mkuu wa TRA afungwe yamepangwa kusikilizwa leo na Katibu wa TRAB, Respicius Mwijage.
Hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo inaeleza kuwa mlalamikiwa, akiwa ni raia wa Tanzania, siyo tu kwamba alipaswa kuwa mtiifu kwa mamlaka ya bodi hiyo, bali pia alipaswa kutekeleza sheria za nchi ambazo bodi hiyo ni sehemu yake.
Hati hiyo ya kiapo ya mkurugenzi wa operesheni wa IPTL, Parthiban Chandrasakaran, inaeleza kuwa kwa kitendo hicho cha kutotii amri ya bodi hiyo, mlalamikiwa amepoteza sifa ya kuwa mtumishi wa umma katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia inaelea kuwa kama bodi hiyo isipotumia mamlaka yake kukubali maombi hayo ya kutoa amri inayoombwa, basi walalamikaji watapata hasara isiyoweza kufidiwa.

No comments:

Post a Comment