IPTL yazua Kizaazaa Mahakamani
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPTL na PAP, Harbinder Singh Sethi
Kampuni
za Pan Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP) na Independent Power
Tanzania Ltd (IPTL), zimewasilisha maombi ya kutaka Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato (TRA) akamatwe kwa kukiuka amri ya Bodi ya Rufaa za
Kodi (TRAB) kwa kufuta Hati za Malipo ya Kodi za Mauzo ya Hisa (Capital
Gain Certificate).
Kampuni
hizo mbili, ambazo ziko kwenye mgogoro wa umiliki, ndizo zinahusika
kwenye sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta
Escrow iliyofunguliwa kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya kuuza umeme
unaofuliwa na IPTL, kwa Shirika la Umeme (Tanesco), wakati wa kusubiri
uamuzi wa mahakama katika kesi ya kupinga tozo hilo.
PAP,
ambayo inadai imenunua hisa zote za IPTL, ndiyo iliyolipwa fedha zote
zilizokuwa kwenye akaunti hiyo na kuamsha mjadala mkubwa bungeni
ulioisha kwa Bunge kufikia uamuzi wa kuwawajibisha kisheria wote
waliohusika, wakiwemo mawaziri.
Lakini
uamuzi huo wa Bunge haukuwa tamati la sakata hilo baada ya kampuni hizo
mbili kukata rufaa TRAB dhidi ya Kamishna wa TRA na Msajili wa Kampuni
na Leseni (Brela) zikipinga kusudio la kufuta hati hizo.(P.T)
Jana
kampuni hizo mbili ziliwasilisha maombi ya hati ya kutaka Kamishna Mkuu
wa TRA akamatwe, zikidai kuwa amepuuza amri hiyo iliyomzuia kutekeleza
azma yake ya kufuta Hati za Malipo ya Kodi ya Mauzo ya Hisa.
Katika
maombi hayo walalamikaji hao wanadai kuwa licha ya TRAB kutoa zuio hilo
Novemba 26, 2014, Kamishna Mkuu wa TRA, ambaye ni mlalamikiwa wa kwanza,
alitoa amri ya kuziondoa hati hizo siku iliyofuata, yaani Novemba 27,
2014, bila kujali amri hiyo.
Walalamikaji
hao pia wanaiomba TRAB, baada ya kumkamata Kamishna Mkuu wa TRA, itoe
amri afungwe kwa kudharau amri halali iliyotolewa na bodi na pia
imwamuru akidhi matakwa ya amri ya TRAB ya Novemba 26.
Pia
walalamikaji hao wanaiomba TRAB imwamuru mlalamikiwa huyo, kulipa
gharama za uendeshaji wa shauri hilo pamoja na amri nyingine ambazo
itaona kuwa zinafaa.
Maombi
hayo ya PAP na IPTL ya hati ya kumkamata na kuamuru Kamishna Mkuu wa TRA
afungwe yamepangwa kusikilizwa leo na Katibu wa TRAB, Respicius
Mwijage.
Hati ya
kiapo inayounga mkono maombi hayo inaeleza kuwa mlalamikiwa, akiwa ni
raia wa Tanzania, siyo tu kwamba alipaswa kuwa mtiifu kwa mamlaka ya
bodi hiyo, bali pia alipaswa kutekeleza sheria za nchi ambazo bodi hiyo
ni sehemu yake.
Hati hiyo
ya kiapo ya mkurugenzi wa operesheni wa IPTL, Parthiban Chandrasakaran,
inaeleza kuwa kwa kitendo hicho cha kutotii amri ya bodi hiyo,
mlalamikiwa amepoteza sifa ya kuwa mtumishi wa umma katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Pia
inaelea kuwa kama bodi hiyo isipotumia mamlaka yake kukubali maombi hayo
ya kutoa amri inayoombwa, basi walalamikaji watapata hasara isiyoweza
kufidiwa.