Taarifa kuhusu bei mpya za umeme zitakazoanza kutumika tarehe 1 Januari 2014
            
Tarehe 11 Oktoba 2013, Shirika la 
Umeme Tanzania (TANESCO) liliwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya 
umeme kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). 
TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia tarehe 1 
Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na asilimia 
9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015.
Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa
 kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei 
za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya 
kitanzania. Aidha, TANESCO iliomba kuidhinishwa viwango vya gharama za 
kuunganisha umeme vinavyozingatia ruzuku inaliyotolewa na Serikali, na 
kuidhinishwa tozo mbalimbali kwa huduma zitolewazo na TANESCO.
Kwa mujibu wa TANESCO, kupitishwa kwa 
maombi haya kutaliwezesha Shirika (a) kupata fedha za uendeshaji na 
uwekezaji wa miundombinu, (b) kulifanya Shirika liweze kukopesheka na 
hivyo kuwezesha kupata mikopo yenye masharti nafuu, (c) kuliwezesha 
Shirika kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya umeme kwenye Gridi ya 
Taifa, na (d) kuongeza uwezo wa
kufanya matengenezo ya mara kwa mara 
ya miundombinu iliyopo ili kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa huduma
 za umeme wa uhakika kwa wateja.(P.T)
 
            
Itakumbukwa kwamba bei za umeme 
zinazotumika hivi sasa ziliidhinishwa mwezi Januari 2012. Bei hizo 
zilipanda kwa asilimia 40.29 ikilinganishwa na maombi ya TANESCO ambapo 
ilipendekeza bei zipande kwa wastani wa asilimia 155. Sababu ilikuwa ni 
kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kulikosababishwa na hali ya ukame 
katika maeneo yanayotiririsha maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme, 
toka mwaka 2011. Hali hiyo ilipelekea TANESCO kulazimika kununua umeme 
kwa gharama kutoka kwa wazalishaji wa dharura (Emergency Power 
Producers). Hali ya maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme bado sio 
nzuri na hivyo TANESCO itaendelea kununua umeme kutoka kwa wazalishaji 
wa dharura (Emergency Power Producers).
USHIRIKISHWAJI WA WADAU
Kulingana na Kifungu Na. 19(2) (h) cha
 Sheria ya EWURA, Mamlaka ilifanya Taftishi ili kupata maoni juu ya ombi
 la kurekebisha bei za umeme. Ukusanyaji wa maoni ulihusisha pia 
mikutano minne (4) iliyofanyika Iringa na Shinyanga tarehe 15 Novemba 
2013, Bagamoyo tarehe 20 Novemba na kuhitimishwa Dar es Salaam tarehe 22
 Novemba 2013. Aidha, tarehe 6 Desemba 2013, EWURA iliitisha mkutano wa 
mwisho wa wadau wakiwemo wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati na 
Madini(MEM), TANESCO, Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO), Shirikisho la
 Wenye Viwanda Tanzania, Baraza la Watumiaji na Baraza la Ushauri la 
Serikali, Umoja wa Wazalishaji wa Saruji wa Afrika Mashariki, na kiwanda
 cha ALAF. Katika mkutano huo EWURA iliwasilisha mwelekeo wa maamuzi 
kuhusu maombi ya TANESCO na namna zilivyokokotolewa. Wadau walipewa 
fursa ya kutoa maoni yao kuhusu mwelekeo wa bei na maoni yao 
yamezingatiwa katika kufikia maamuzi ya mwisho.
UCHAMBUZI NA UAMUZI
Kwa kufuata sheria na kanuni 
zinazoelekeza kuhusu uchambuzi wa bei ya umeme, EWURA ilifanya uchambuzi
 wa kifedha na kiufundi ili kubaini uwezo wa TANESCO katika kutekeleza 
majukumu yake ya kila siku. Uchambuzi uliangalia utendaji wa Shirika la 
TANESCO katika miaka iliyopita na pia iliangalia majukumu yanayoikabili 
TANESCO katika miaka mitatu ijayo. EWURA imebaini kwamba hali ya kifedha
 ya Shirika la Umeme sio nzuri. Shirika limeendelea kupata hasara, 
ambayo iliongezeka kutoka shilingi bilioni 47.3 katika mwaka 2010 na 
kufikia shilingi bilioni 223.4 mwishoni mwa mwaka 2012. Pamoja na 
mapungufu ya kiufanisi, sababu kubwa ya ongezeko la hasara ni kuongezeka
 kwa gharama za uzalishaji wa umeme ambao TANESCO inanunua kutoka kwa 
wazalishaji binafsi. Hali hii imelifanya shirika kushindwa kulipa madeni
 yake ya muda mfupi na ya muda mrefu, ambayo yamelibikizwa na kufikia 
TZS 456.8 bilioni tarehe 22 Novemba 2013, hali ambayo inatishia 
uendelevu wa huduma ya umeme hapa nchini.
Mamlaka imetumia Kanuni ya Ukokotoaji 
wa Bei kama ilivyopendekezwa na AF-MERCADOS wakati wa kukokotoa mahitaji
 ya mapato ya TANESCO. Kanuni hiyo inawezesha kukokotoa bei 
zinazolandana na gharama halisi kwenye mfumo wa umeme na kuzigawa kwenye
 makundi ya watumiaji umeme, kadiri kila kundi linavyosababisha gharama 
kwenye mfumo wa umeme kwa mujibu wa mahitaji ya Sheria ya Umeme ya 2008 
Kifungu cha 23(2)(f).
EWURA imejiridhisha kwamba, ufumbuzi wa matatizo ya kifedha ya TANESCO, unahitaji njia/mikakati miwili itekelezwe kwa pamoja:
kuongeza bei ya umeme ili kufikia bei inayokidhi gharama halisi (Cost Reflective Tariff); na
TANESCO kupata mkopo wa gharama nafuu ama ruzuku kutoka Serikalini ili kulipa limbikizo la madeni ya Shirika.
Bodi ya Wakurugenzi wa EWURA, katika 
kikao chake cha tarehe 10 Desemba 2013 pamoja na mambo mengine, ilitoa 
maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa viwango mbalimbali kwa makundi 
mbalimbali ya wateja, kama ifuatavyo:
Kundi D1: Hili ni kundi la wateja 
wadogo wa majumbani, hasa vijijini, ambao hutumia wastani usiozidi wa 
Uniti 75 kwa mwezi. EWURA imeongeza wigo wa mahitaji ya umeme na kufikia
 uniti 75 kwa mwezi, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya wateja wa TANESCO
 wanaoweza kulipa kidogo kwa matumizi ya umeme kwa kiwango hicho, na pia
 kuwahamasisha kutumie zaidi umeme. Awali kundi hili lilikuwa linatunia 
wastani wa matumizi ya uniti 50 kwa mwezi. Bei mpya ni shilingi 100 kwa 
uniti moja, kutoka shilingi 60 za sasa, sawa na ongezeko la shilingi 40.
Kundi T1: Hili ni kundi la watumiaji 
wakubwa wa umeme majumbani, biashara ndogondogo, mashine za kukoboa na 
kusaga nafaka, taa za barabarani, mabango n.k. Bei iliyoidhinishwa ni 
shilingi 306 kwa uniti moja, ikiwa ni ongezeko la Shilingi 85 ya bei ya 
sasa. TANESCO ilipendekeza ongezeko la shilingi 131.
Kundi T2: Hili ni kundi la watumiaji 
umeme wa kawaida ambao hupimwa katika msongo wa volti 400, na ambao 
matumizi yao ya wastani kwa mwezi ni zaidi ya uniti 7,500 wateja 
wafanyabiashara kubwa, viwanda vya kati. Bei ya nishati iliyoridhiwa ni 
shilingi 205 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 73 ya bei ya 
sasa. TANESCO walipendekeza ongezeko la shilingi 145 ya bei ya sasa.
Kundi T3-MV: Hili ni kundi la wateja 
wakubwa kama viwanda vikubwa waliounganishwa katika msongo wa kati 
(Medium Voltage). EWURA imeidhinisha bei ya nishati kwa kiwango cha 
shilingi 166 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 45 ya bei ya 
sasa. TANESCO walipendekeza ongezeko la shilingi 148 kwa uniti moja.
Kundi T3-HV: Hili ni kundi la wateja 
wakubwa waliounganishwa katika msongo wa juu (High Voltage – Voti 66,000
 na zaidi) ikiwa ni pamoja na ZECO, Bulyanhulu, na Twiga Cement. Bei 
iliyoidhinishwa ni shilingi 159 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la 
shilingi 53 la bei ya sasa. TANESCO waliomba ongezeko la shilingi 80 kwa
 uniti moja.
Bei ya umeme itakuwa inarekebishwa 
kila baada ya miezi mitatu kulingana na mabadiliko ya kiwango na bei za 
mafuta; mfumuko wa bei, mabadiliko ya thamani ya fedha, na upatikanaji 
wa ruzuku toka Serikalini.
Vilevile, TANESCO inatakiwa kutekeleza
 miradi ya uwekezaji iliyoainishwa kwa kutumia fedha zitakazokusanywa 
kutokana na bei zilizoidhinishwa. EWURA inaweza kurekebisha bei ya umeme
 ya TANESCO kila mwisho wa mwaka 2014 na/au mwaka 2015 endapo TANESCO 
itashindwa kutekeleza miradi iliyotajwa katika Jedwali husika. 
Marekebisho hayo yatatokana na makadirio ya gharama za miradi ambayo 
haikutekelezwa.
Kutokana na matazamio ya kuwa na 
mabadiliko makubwa katika uzalishaji wa umeme (generation mix) katika 
mwaka 2015 na kuendelea, kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa kwa 
upatikanaji wa gesi asilia, EWURA itafanya utafiti kubaini gharama 
halisi (Cost of Service Study) ya huduma ya umeme kwa wakati huo. Hivyo,
 bei zilizoidhinishwa zitatumika mpaka mwaka 2016, kama utafiti 
unaotazamiwa kufanywa hautakamilika kabla ya mwisho wa mwaka 2015.
EWURA ililinganisha bei za umeme kwa 
kila Uniti, katika nchi za Afrika ya Mashariki, na kuona kuwa bado bei 
za umeme za Tanzania zipo chini ukilinganisha na bei za katika nchi 
jirani kama inavyoonyeshwa hapa chini, kwa makundi mbalimbali ya 
watumiaji umeme.
Pamoja na maamuzi hayo, Bodi ya Wakurugenzi wa EWURA, pia iliagiza TANESCO kutekeleza yafuatayo:
kuzalisha umeme kwa kutumia mitambo 
yenye gharama nafuu ("least cost merit order") na kuwasilisha ripoti kwa
 Mamlaka katika kila mwezi ikionyesha uzalishaji halisi na mpango wa 
uzalishaji kama ilivyoidhinishwa na EWURA;
kuhakikisha kuwa zabuni za miradi ya 
uzalishaji umeme zinatolewa kulingana na mahitaji kama ilivyoidhinishwa 
kwenye Mpango wa Umeme wa Taifa (Power System Master Plan). Miradi yote 
mipya lazima ipatikane kwa njia ya ushindani kwa kufuata Sheria ya 
Umeme, "Public Private Partnership Act", Sheria ya Manunuzi ya Umma na 
Kanuni husika;
kuwasilisha ripoti kila baada ya miezi
 mitatu kuhusu viashiria vya takwimu za ubora na uhakika wa umeme 
(supply and reliability) katika misongo ya 11kV, 33 kV, 66 kV, 132 kV, 
na 220 kV kwa kila mkoa kwa ajili ya uhakiki. Takwimu husika zinatakiwa 
kuonyesha jumla ya masaa mteja aliyokosa umeme kwa kila njia ya umeme 
("feeder"), kukosekana kwa umeme kulikopangwa (planned outages), na 
ambao haukupangwa (unplanned outages), idadi ya matukio ya kukosa umeme 
katika kila "feeder", idadi ya wateja wanaohudumiwa na kila "feeder", 
idadi ya wateja walioathirika na katizo la umeme katika kila "feeder" na
 kiasi cha umeme kilichokosekana kutokana na katizo hilo (total unserved
 energy in kWh);
kuwasilisha kwa Mamlaka, katika 
kipindi cha miezi mitatu baada kuanza kwa Agizo hilo la Mamlaka, mpango 
wa utekelezaji wa "Demand Side Management Programme" ili uidhinishwe;
kupunguza kiwango cha upotevu wa umeme
 (technical and non-technical losses) katika mtandao wa usambazaji 
kutoka asilimia 19 ya mwaka 2012 hadi asilimia 15.1 ifikapo mwisho wa 
mwaka 2015;
kubuni mikakati ya kupambana wizi wa 
umeme utokanao na uunganishaji umeme usio halali, na kuondoa 
ucheleweshaji usio wa lazima katika kutunganisha wateja wapya;
kuhamisha wateja walio katika kundi la D1 kwenda T1 endapo matumizi yao ya mwezi yatazidi uniti 75 kwa miezi mitatu mfululizo;
kuwasilisha kwa Mamlaka, kabla au 
tarehe 31 Machi, 2014, Mpango wa kuwawekea wateja wake mita za LUKU na 
AMR ili kupunguza wateja wanaotumia mita za zamani (conventional 
meters);
kuwasilisha kwa Mamlaka, kila baada ya
 miezi mitatu, taarifa/ripoti ya ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wateja 
wake ili kuongeza mapato ya Shirika;
kutoa elimu kwa wateja wake kuhusu 
haki na wajibu wa wateja kwa mujibu wa Mkataba wa Huduma kwa Wateja na 
kushughulikia kero za wateja kama inavyoelekezwa katika Mkataba husika 
na Kanuni za Umeme;
kuwasilisha kwa Mamlaka, maombi ya 
marekebisho ya bei yatokanayo na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa
 bei na ubadilikaji wa thamani ya fedha; Ukokotoaji wa marekebisho hayo 
utakuwa kama ulivyoainishwa katika Kanuni za Kupanga Bei za Umeme za 
mwaka 2013 (Electricity (Tariff Setting) Rules, 2013);
kuendelea kutoa taarifa kwa Mamlaka 
kuhusu hali ya kifedha na kiundeshaji. Taarifa hizi zitatumiwa na 
Mamlaka katika kutathmini utendaji wa TANESCO ikilinganishwa na 
mashirika mengine ya umeme katika nchi jirani ili kuboresha utendaji 
wake. Tathmini hii pia itatumiwa na Mamlaka katika kubaini uhalali wa 
maombi ya baadae ya kurekebisha bei;
kuwasilisha kwa Mamlaka, kabla au tarehe 31 Machi 2014, mpango wa utekelezaji wa kila sharti katika Agizo la EWURA.
Bei mpya za umeme zitaanza kutumika 
tarehe 1 Januari 2014. Ni matarajio ya EWURA kwamba TANESCO watatumia 
fursa hii kutoa huduma bora zaidi za umeme na kuhakikisha kuwa 
wanashughulikia malalamiko ya wateja kila yanapojitokeza ili kurejesha 
imani kwa Shirika la Umeme la TANESCO.
AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
Source: http://www.wavuti.com